Halmashauri ya Wilaya ya Siha Mkoa wa
Kilimanjaro leo tarehe 30 mei,2017 imefanya maazimisho ya juma la elimu kwa
kufanya maonesho mbalimbali ya kielimu na kujumuisha wanafunzi wa shule za
msingi na Sekondari Wilayani hapa.
Maazimisho hayo yamefanyika Kiwilaya katika
shule ya Msingi Sanya juu ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Siha
Mhe. Onesmo Buswelu.
Katika hotuba yake katika maazimisho hayo Mkuu
wa Wilaya ya Siha Mhe.Onesmo Buswelu alisema kuwa wale wote wanaosababisha
mimba kwa wanafunzi sasa wakati umefika wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Mkuu wa Wilaya aliongeza kuwa wapo baadhi ya wazazi kwa kushirikiana na walimu
wamekuwa wakiwaficha wahalifu hao mara baada ya kutenda makosa yao.
Aliongeza kuwa kuanzia sasa mtu yeyote
atakayesababisha mimba kwa mwanafunzi wa shule Serikali ya Wilaya ya Siha itamsaka
popote atakapokwenda na kuhakikisha mtu huyo anachukuliwa hatua za kisheria.
Mhe Onesmo Buswelu Mkuu wa Wilaya ya Siha
ametoa wiki mbili kwa wakuu wote wa shule za Sekondari Wilaya ya Siha
kumpelekea taarifa za miaka mitatu iliyopita kuhusu hali ya mimba katika shule.
Aliongeza kuwa iwapo atabaini kuwa tatizo la
mimba limekuwa likijirudia katika shule moja kwa miaka miwili au mitatu
mfululizo basi hata sita kumchukulia hatua stahiki mkuu wa shule husika.
Mkuu wa Wilaya ambaye pia alikuwa mgeni rasmi
wa siku ya Elimu Siha alitoa wito kwa Wazazi
kushirikiana na Walimu ili kuboresha kiwango cha ufaulu cha wanafunzi katika
shule za msingi na Sekondari Wilayani Siha. Wilaya ya Siha inajumla ya shule 59 za Msingi na shule 19
za Sekondari.
No comments:
Post a Comment