Friday 23 June 2017

Ujenzi wa Bweni la wasichana shule ya Sekondari Oshara unaendelea

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Siha Valerian Juwal akishiriki katika ujenzi wa Bweni la Wasichana shule ya sekondari Siha tarehe 22.06.2017

Matukio ya wiki ya Utumishi wa Umma tarehe 23.6.2017

 Watumishi wa umma wakiwa katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha katika wiki ya Utumishi wa Umma

Monday 19 June 2017

DC Siha apiga Marufuku Biashara ya Mahindi Mabichi



Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. onesmo Buswelu amepiga marufuku biashara ya uchomaji,uuzaji na usafirishaji wa mahindi mabichi ndani na Nje ya Wilaya.

Agizo hilo amelitoa leo tarehe 19.06.2017 alipokuwa katika ukaguzi wa ujenzi wa shule mpya ya Msingi inayojengwa katika kijiji cha  Sanya hoyee Kata ya Sanya Juu.

Mkuu wa Wilaya ya Siha ameeleza kuwa sababu kubwa ya kutoa amri hiyo halali ni pamoja na malalamiko mengi aliyoyapokea ya wizi wa mahindi mabichi mashambani kutoka kwa viongozi wa Vijiji na Vitongoji Wilayani hapa.

Alieleza kuwa amri hiyo inatekelezwa kuanzia leo tarehe 19.06.2017 hadi msimu wa mavuno ya  masika kwa mwaka 2017 utakapokamilika. 

Mhe Onesmo Buswelu ametoa wito kwa Wananchi wa Siha kuhakikisha wanaweka akiba na ziada ya chakula kwa ajili ya familia zao na kuepukana na kuuza chakula chote kwa tamaa za kujipatia fedha.

amewataka pia Wananchi wa Wilaya ya Siha kuzingatia agizo la kutotumia nafaka ya mahindi kwa ajili ya utengenezaji wa pombe za kienyezi na badala yake watumia nafaka mbadala kama vile ngano na shairi kama wakiona ni lazima kufanya hivyo.

Kwa msimu wa mwaka 2017,Wilaya ya Siha inategemea kupata msimu mzuri wa chakula hasa zao la mahindi ,viazi na ndizi.

Sanya Hoyee wapongezwa kwa ujenzi wa Shule



Wananchi wa Kijiji cha Sanya hoyee Kata ya Sanya Juu  wapongezwa kwa ujenzi  wa madarasa mawili ya shule mpya ya msingi katika kijiji cha Sanya Hoyee.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Onesmo Buswelu alipofika eneo linapojengwa shule hiyo leo tarehe 19 Juni,2017 na kukagua shughuli za ujenzi zinazoendelea.

Mkuu wa Wilaya ya Siha aliwapongeza viongozi wa Kata na Vijiji kwa kazi nzuri aliyoiona hasa ujenzi wa madarasa na matundu ya choo cha wanafunzi,aliwataka wananchi na Wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kuunga mkono juhudi za Jamii katika kujiletea maendeleo.

Katika ujenzi huo hadi Juni,2017 wananchi wameshachangia zaidi ya shilingi milioni 5 ambazo zimetumika katika shughuli mbalimbali za ujenzi huo.

Hata hivyo mkuu huyo wa Wilaya ya Siha ametoa shilingi laki mbili kama mchango wake wa kuunga mkono juhudi za wananchi  za kujiletea maendeleo.

Hadi sasa ujenzi umefikia katika hatua ya umaliziaji wa kuweka rangi,kuweka vioo pamoja na umaliziaji wa vyoo vya wanafunzi ikiwa ni  pamoja na ujenzi wa choo wa walimu.

Kukamilika kwa shule hiyo kutasaidia kupunguza msongamano wa Wanafunzi katika shule za msingi Meral,Sanya Juu na Kilingi. Shule hiyo mpya ya msingi inatarajiwa kuanza rasmi mwezi januari mwaka 2018.

Friday 16 June 2017

Siha kuwawezesha kiuchumi walemavu wa Ngozi

Wilaya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro itaweka kipau mbele suala la kuwawezesha walemavu wa ngozi kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha Valerian Juwal katika  maazimisho ya siku ya watu wenye Ualbino yaliyofanyika Kiwilaya katika ofisi ya Kijiji cha Lawate tarehe 15.06.2017.
Katika hotuba yake Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Siha aliagiza idara ya maendeleo ya Jamii na ustawi wa Jamii kuhakikisha kuwa walemavu wa ngozi Wilayani Siha wanapewa fursa za kuwezeshwa katika mikono kama wanavyopewa makundi mengine hasa yale ya vijana na wanawake.
Alieleza kuwa fedha hizo zinaweza kutolewa katika asilimia kumi ya Mapato ya ndani ambazo kimsingi hutengwa kila mwaka kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya vijana na Kinamama.
Mkurugenzi Mtendaji alisema kuwa kwa nafasi yake atahakikisha kuwa jinsi hilo muhimu linapatiwa huduma zinazohitajika kama vile Elimu,afya na ulinzi wa kutosha kwa ushirikiano wa wadau wa maendeleo,wananchi na viongozi mbalimbali katika jamii.
Pia Mkurugenzi Mtendaji alitoa wito kwa jamii ya wanasiha kuendelea kushirikiana na Serikali katika suala la ulinzi na usalama kwa watu wenye Ualbino katika Wilaya ya Siha.
Maazimisho ya mwaka huu yamekuwa na kauli mbiu Umuhimu wa Takwimu na Tafiti kwa ustawi wa Watu wenye Ualbino

Wednesday 14 June 2017

Serikali Wilaya ya Siha yapiga Marufuku biashara ya mahindi ya kuchoma




Uongozi wa Serikali katika Wilaya ya Siha Mkoa wa Kilimanjaro  umepiga marufuku biashara ya mahindi ya kuchoma katika maeneo yote Wilayani hapa.

Azimio hilo limetolewa leo tarehe 14 Juni,2017 na Wenyeviti wa Vijiji Wilaya ya Siha walipokutana  na Mkuu wa Wilaya ya Siha katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha kwa lengo la kuzungumzia mambo mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Siha.

Wenyeviti hao wa Vijiji  kwa kauli moja walimwomba Katibu Tawala wa Wilaya ya Siha Mhe. Nicodemus John   ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Siha kuwa,kutokana na wizi wa mahindi mabichi unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya Siha wameona ni bora kumwomba Mkuu wa Wilaya kupiga marufuku biashara hiyo hadi mazao ya mahindi  yatakapovunwa mashambani.

Katika Azimio hilo,sababu zilizotolewa na Viongozi hao za kutoa ombi kwa Mkuu wa Wilaya ya Siha kupiga marufuku biashara hiyo ni pamoja na kuzuia wizi wa mahindi mashambani  na sababu nyingine ni jitihada za kuhakikisha chakula kitakachovunwa kinatumika vizuri kwa manufaa ya ustawi wa jamii.

Aidha katika kikao hicho,Mwenyekiti wa Kijiji cha Wiri Mheshimiwa Hamza Munisi aliishukuru Serikali ya Wilaya ya Siha kwa jinsi inavyosimamia kikamilifu sheria mbalimbali hasa za uhifadhi na utunzaji wa mazingira katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Hamza pia alishauri kuwa wale wote wanaofanya biashara ya mahindi ya kuchoma ni vema watafute biashara nyingine kwa wakati huu katazo hilo linapotolewa rasmi.


Akichangia na kujibu hoja mbalimbali za Wenyeviti wa Vijiji katika Mkutano huo,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha Valerian Juwal aliwashukuru Wenyeviti wa Vijiji vyote Wilayani Siha kwa ushirikiano wanaendelea kuutoa kwa serikali kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya Wananchi Wilayani Siha.

Mkurugenzi Mtendaji aliwaahidi Wenyeviti hao kuwa,Halmashauri ya Siha itaendelea kufanya kazi kwa misingi ya kufuata  Sheria zilizopo na kuwataka Watendaji wa umma kuhakikisha wanachapa kazi kwa uadilifu na kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wowote.

Kutokana na sensa ya idadi ya watu na makazi ya mwaka 2012,Wilaya ya Siha inajumla ya watu 116313 kati yao  Wanawake wakiwa 59813 na Wanaume 56500

Monday 12 June 2017

Siha kuazimisha Siku ya watu wenye Ualbino tarehe 15 Juni,2017



Wilaya ya Siha kuazimisha siku ya watu wenye Ualbino
Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro itaazimisha siku ya watu wenye Ualbino(Albinism)  siku ya Alhamis  tarehe 15 Juni,2017.

Maazimisho ya siku ya watu wenye Ualbino  Kiwilaya yanategemewa kufanyika katika ofisi ya kijiji cha Lawate huku kauli mbiu ya mwaka  2017 ikiwa “Umuhimu wa takwimu na tafiti kwa ustawi wa  watu wenye Ualbino”.

Aidha,maazimisho hayo yatafanyika kwa mara ya kwanza Wilayani Siha kwa mwaka 2017, huku Wilaya ya Siha ikiwa na historia nzuri ya kuwatunza na kuwalinda watu wenye Ualbino.
Hadi sasa Wilaya ya Siha haina tukio lolote lililotokea na kuripotiwa juu ya kitendo chochote cha kuwanyanyasa,kuwajeruhi au mauaji ya walemavu wa ngozi waliopo katika Wilaya ya Siha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha anatoa wito kwa Wananchi na Wakazi wa Wilaya ya Siha kuendelea na moyo huo wa upendo wa kuwatunza na kuwalinda ndugu zetu wenye Ualbino hasa kwa kuwapatia mahitaji yao muhimu kama elimu,huduma za Afya na huduma nyingine muhimu.

Wilaya ya Siha inakadiriwa kuwa na watu wenye Ualbino wapatao 11 ambao wanaishi na jamii katika maeneo tofauti tofauti Wilayani hapa.


Sunday 11 June 2017

Chanjo ya Kichaa cha Mbwa kuanza kutolewa Hospital ya Wilaya



OFISI YA RAIS TAMISEMI
HALMASHAURI YA WILAYA YA SIHA

TAARIFA KWA UMMA
Mganga Mkuu wa Hospital ya Wilaya ya Siha anawatangazia Wananchi wote Wilayani Siha kuwa, Chanjo ya Kichaa cha Mbwa sasa inapatikana katika hospital ya Wilaya ya Siha kwa bei nafuu kabisa ya Shilingi elfu 30 tu.

Hivyo kwa wale wote watakaopata matatizo ya kung’atwa/kuumwa na Mbwa  wafike hospital ya Wilaya ya Siha na watapatiwa matibabu mara moja.

Aidha,kupatikana kwa huduma hii muhimu kutawasaidia Wananchi wa Wilaya ya Siha kuepukana na usumbufu wa kuwapeleka wagonjwa wao katika hospital ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi ,ambapo huduma hizi zilikuwa zinapatika hapo awali.

Wananchi na Wakazi wa Wilaya ya Siha mnaombwa kutumia fursa hii muhimu ya matibabu ili kuokoa maisha ya ndugu, jamaa na marafiki zetu wanaopatwa na janga la kung’atwa na Mbwa.

Matibabu ya Chanjo ya kichaa cha Mbwa yanatolewa kwa binadamu aliyeng’atwa na Mbwa matibabu yanapatikana muda wowote  katika Hospital yetu ya Wilaya ya Siha.

Hata hivyo,Halmashauri ya Wilaya ya Siha inatoa wito kwa Wananchi na Wakazi wa Wilaya ya Siha kufungia Mbwa  nyakati za mchana ili kuzuia  madhara kwa binadamu.

Tunawashukuru Wananchi kwa ushirikiano wetu wa dhati, tunaomba upatapo taarifa hizi umjulishe na mwenzako.

Limetolewa na:-

Kitengo cha Habari na Mawasiliano (W) Siha
Juni 09,2017

Monday 5 June 2017

Watumishi wa Umma Siha waendelea na Uhakiki




ZOEZI LA UHAKIKI KWA WATUMISHI WA UMMA- SIHA
Zoezi la uhakiki wa akaunti za mishahara kwa Watumishi wa Umma Wilayani Siha limefikia siku ya tatu leo tangu lilipoanza  siku ya ijumaa tarehe 02 Juni,2017. Zoezi hili linafanyika katika  Ofisi za Makao makuu ya  Halmashauri ya  Wilaya ya Siha. 

Hadi sasa zoezi  linaendelea kwa mafanikio makubwa hasa baada ya Watumishi wengi wa Umma katika kada mbalimbali kuonekana wakiendelea na kazi kukagua majina yao na kuhakiki kama yanaendana majina yaliyopo katika orodha ya mishahara(payroll).

Zoezi la Uhakiki kwa Watumishi wa Umma katika Wilaya ya Siha linategemewa kumalizika tarehe 06 Juni, 2017.