Thursday 10 August 2017

Siha kutumia tekinolojia kuendeleza kilimo na ufugaji Bora




Halmashauri ya Wilaya ya Siha kueneza tekinolojia mpya  ya kilimo  na ufugaji bora katika ngazi ya Halmashauri , Kata na  hatimaye katika vijiji vyote. 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha Valerian Juwal alipokuwa katika kilele cha maonesho ya nanenane yaliyofanyika kikanda katika viwanja vya Njiro Arusha ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Siha ilipata fursa ya kuonesha tekinolojia mbalimbali ya kilimo na mifugo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha alisema kuwa Halmashauri ya Siha itahakikisha kuwa mashamba Darasa yaliyopo kila kata yanaendelezwa ili kuwanufaisha wananchi wa maeneo husika na vijiji jirani.

Alieleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Siha itawatumia wataalam wa kilimo na mifugo waliopo katika ngazi ya Halmashauri ,Kata na Vijiji kuhakikisha wakulima wanapatiwa utaalam na ushauri wa kilimo na ufugaji wa kisasa ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na ufugaji.

Juwal aliwataka wananchi kuondokana na kilimo  na ufugaji wa kitamaduni na badala yake wabadilike na kuanza kulima na kufuga kwa kufuata tekinolojia mpya ambazo zitawasaidia kuongeza kipato na kuondokana na kuwa na vipato duni.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Siha ametoa wito kwa viongozi mbalimbali Wilayani Siha kuendelea kuwahamasisha wananchi kuzingatia ushauri wanaopewa na wataalam wa kilimo na mifugo waliopo katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo pia.

Zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Wilaya ya Siha wanategemea kilimo na ufugaji kama shughuli kubwa za kiuchumi kwa wananchi hao.mazao yanayolimwa kwa wingi zaidi ni Mahindi,maharage,viazi,ndizi,ngano,shairi na mazao ya mbogamboga.


Tuesday 1 August 2017

Jukwaa la Wanawake yazinduliwa rasmi Siha



Jukwaa la Wanawake yazinduliwa rasmi Siha
Wilaya ya siha mkoa wa Kilimanjaro limefanikiwa kuzindua jukwa la wanawake kufuatia agizo la serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kuwa kila wilaya kuwa na jukwaa hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Siha mhe Onesmo Buswelu amezindua jukwa hilo rasmi leo tarehe 01 Agosti 2017 ambapo uzinduzi huo umefantika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki uliopo katika Kata ya Sanya Juu.

Katika hotuba aliyoitoa kwa wanawake wa Wilaya ya Siha,mhe Onesmo Buswelu ambaye pia alikuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo aliwataka wanawake kujiamini na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ya Tanzania katika kujiletea maendeleo ndani ya jamii.

Alieleza kuwa Serikali inatambua kuwa mwanamke akipata elimu jamii itakuwa imeelimika kwa ujumla,hivyo wanawake wachangamke katika kujiunga na vikundi mbalimbali ili waweze kupatiwa mikopo na elimu ya ujasilia mali na ukuzaji wa uchumi.

Aidha,mkuu huyo wa Wilaya ya Siha aliwaambia wanawake kuwa Halmashauri ya Siha inatenga bajeti ya asilimia 5 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya wanawake na asilimia 5 ya mikopo kwa vijana  kila mwaka wa fedha.

Katika uzinduzi huo wa jukwaa la Wanawake pia uongozi wa wilaya ulichaguliwa na viongozi waliochaguliwa walikuwa kama ifuatavyo:- Mwenyekiti wa jukwaa la wanawake alichaguliwa Christina P kavishe na Katibu wa Jukwaa la wanawake ni Aisha S.  Mwiru.

Baada ya uchaguzi huo, mwenyekiti wa jukwaa la wanawake wilaya ya Siha Christine Kavishe aliwashukuru kinamama wote waliomchagua na kuahidi kuwaunganisha wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa na imani zao za madhehebu ya  dini.