Wednesday 31 May 2017

Walimu Wilaya ya Siha watakiwa kutimiza wajibu wao




Walimu Wilayani Siha Watakiwa kutimiza wajibu wao
Walimu wa shule za msingi na Sekondari Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro wametakiwa kutimiza wajibu wao wa kazi ili kuongeza ufaulu wa Wanafunzi katika shule wanazofundisha.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe.Onesmo Buswelu katika maazimisho ya juma la elimu yaliyofanyika Kiwilaya  katika shule ya msingi Sanya Juu tarehe 30.5.2017.

Mkuu wa Wilaya ya Siha ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika maazimisho ya elimu kwa mwaka 2017 Wilayani Siha, alikagua maonesho mbalimbali ya wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari na kuridhishwa na kazi zilizoonyeshwa na wanafunzi.

Katika hotuba aliyoitoa kwa Wananchi,wadau wa elimu,Walimu na Wanafunzi ,Mkuu  wa Wilaya ya Siha aliwataka Walimu kutimiza wajibu wao na kutambua kuwa wao kama watumishi wa Umma ni sehemu muhimu ya Serikali.

Aliongeza kuwa Serikali ya awamo ya Tano chini ya uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli inawathamini sana walimu na inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Walimu katika kulikomboa Taifa na adui ujinga.

Aidha,Mhe Onesmo Buswelu aliwataka wazazi kuendelea kushirikiana na Serikali yao kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wa Kitanzania wanapata elimu inayostahili kwa maendeleo ya familia,jamii na taifa kwa ujumla.

Wilaya ya Siha yang'ara michezo UMISSETA Mkoa wa Kilimanjaro





Siha yang’ara michezo ya UMISSETA Mkoa wa Kilimanjaro
Timu ya Michezo ya wanafunzi wa shule za sekondari Wilaya ya Siha imekuwa tishio kwa michezo mbalimbali kwa mkoa wa Kilimanjaro iliyomalizika hivi karibuni mjini Moshi.

Katika michezo hiyo Timu ya  Wilaya ya Siha imefanikiwa kutangazwa mabingwa wa Mkoa wa Kilimanjaro katika michezo ifuatayo:-
i)                  Wilaya ya Siha wamekuwa mabingwa wa Mpira wa Wavu kwa wasichana
ii)                Wilaya ya Siha wamekuwa pia mabingwa wa Mkoa wa Kilimanjaro katika  mchezo wa Kikapu kwa Wasichana  
iii)             Wilaya ya Siha pia imechukua nafasi ya kwanza kwa mchezo wa riadha mita 3000 ambapo mkimbiaji wa Siha alivunja rekodi ya mkoa kwa kukimbia kwa kasi zaidi kuliko wakimbiaji wote walioshiriki mwaka 2017
iv)             Wilaya ya Siha pia ilipata nafasi ya pili kwa mchezo wa wavu kwa Wavulana

Aidha, Wilaya ya Siha imefanikiwa kutoa wachezaji 10 wanaounda timu ya Mkoa wa Kilimanjaro itakayoweka kambi yake kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Taifa   ya umoja wa michezo kwa shule za sekondari (UMISSETA 2017)

Tuesday 30 May 2017

Tangazo la Viwanja Halmashauri ya Siha_ Mkoa wa Kilimanjaro


Wanaowapa Wanafunzi mimba watangaziwa Kiama Siha




Halmashauri ya Wilaya ya Siha Mkoa wa Kilimanjaro leo tarehe 30 mei,2017 imefanya maazimisho ya juma la elimu kwa kufanya maonesho mbalimbali ya kielimu na kujumuisha wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari Wilayani hapa.

Maazimisho hayo yamefanyika Kiwilaya katika shule ya Msingi Sanya juu ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Onesmo Buswelu.

Katika hotuba yake katika maazimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe.Onesmo Buswelu alisema kuwa wale wote wanaosababisha mimba kwa wanafunzi sasa wakati umefika wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Mkuu wa Wilaya aliongeza kuwa wapo  baadhi ya wazazi kwa kushirikiana na walimu wamekuwa wakiwaficha wahalifu hao mara baada ya kutenda makosa yao.

Aliongeza kuwa kuanzia sasa mtu yeyote atakayesababisha mimba kwa mwanafunzi wa shule Serikali ya Wilaya ya Siha itamsaka popote atakapokwenda na kuhakikisha mtu huyo anachukuliwa hatua za kisheria.

Mhe Onesmo Buswelu Mkuu wa Wilaya ya Siha ametoa wiki mbili kwa wakuu wote wa shule za Sekondari Wilaya ya Siha kumpelekea taarifa za miaka mitatu iliyopita kuhusu hali ya mimba katika shule.

Aliongeza kuwa iwapo atabaini kuwa tatizo la mimba limekuwa likijirudia katika shule moja kwa miaka miwili au mitatu mfululizo basi hata sita kumchukulia hatua stahiki mkuu wa shule husika.

Mkuu wa Wilaya ambaye pia alikuwa mgeni rasmi wa siku ya Elimu Siha alitoa wito kwa  Wazazi kushirikiana na Walimu ili kuboresha kiwango cha ufaulu cha wanafunzi katika shule za msingi na Sekondari Wilayani Siha. Wilaya ya Siha inajumla ya shule 59 za Msingi na  shule 19 za Sekondari.