OFISI
YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
HALMASHAURI
YA WILAYA YA SIHA
TAARIFA YA MWENYEKITI WA HALMASHAURI MKUTANO
WA KAWAIDA WA BARAZA LA MADIWANI KATIKA KIPINDI CHA ROBO YA TATU (JANUARI
-MACHI,2017).
v Mheshimiwa
Mkuu wa Wilaya ya Siha,
v Mwakilishi
Ofisi ya RAS-Mkoa wa Kilimanjaro,
v Mh.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Siha,
v Mh.
Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Siha,
v Waheshimiwa
Madiwani,
v Mkurugenzi
Halmashauri ya Siha,
v Viongozi
wa Dini,
v Wageni
Waalikwa,
v Ndugu
Wataalamu,
v Waandishi
wa Habari,
v Wananchi
wa Wilaya ya Siha,
v Mabibi
na Mabwana,
Wasalaam Alekumu,Tumsifu Yesu Kristo,Bwana
Yesu asifiwe
Wah.
Madiwani , na Ndugu Wananchi;
Kwanza
kabisa napenda kuwakaribisha Waheshimiwa Madiwani,Wananchi,Wadau wa
maendeleo,Wataalam wa Halmashauri na Waandishi wa Habari katika Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Madiwani katika
kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2016/2017 (Januari hadi Machi,2017).
Katika kipindi hiki tumeshuhudia Halmashauri yetu ikiendelea na shughuli zake
za kuwapatia Wananchi wa Wilaya ya Siha huduma mbalimbali zikiwemo za
Afya,Elimu,Maji na huduma nyinginezo. Kipekee napenda kuwapongeza Waheshimiwa
Madiwani na Wataalam wa Halmashauri ya Siha kwa kuiwezesha Halmashauri ya Siha
kupata hati Safi na kuwa miongoni mwa Halmashauri za Mkoa wa Kilimanjaro na
Tanzania. Naomba kwa pamoja tuendelee kushirikiana Viongozi na Watumishi ili kuhakikisha kuwa
Halmashauri yetu inaendelea kufanya vizuri na kupata hati safi kwa miaka mingi
ijayo.
(1)UKUSANYAJI WA MAPATO
Waheshimiwa Madiwani,
Kama
mnavyojua Waheshimiwa Madiwani na ndugu
Wananchi wa Siha kuwa bado Halmashauri yetu inakabiliwa na kuwa na
tatizo la kuwa na vyanzo vichache na vya kudumu kwa ajili kukusanya Mapato ya
ndani ya Halmashauri. Nawaomba tena kwa umoja wetu tuendelee kubuni vyanzo
mbalimbali vya kuongeza mapato ya ndani ya
Halmashauri yetu ili itusaidie
kuboresha huduma mbalimbali kwa Wananchi wetu. Ukweli ni kwamba vyanzo vya mapato ya ndani vilivyopo sasa kama vile ushuru wa Masoko,Ushuru wa
mazao,Leseni na Vituo vya Mabasi siyo vyanzo vya kutegemewa sana kwani mapato
tunayopata kutoka vyanzo hivi bado ni kidogo sana. Napenda kutoa Rai kwa
viongozi wenzangu tufikirie zaidi nakuwa wabunifu zaidi hasa namna ya kupata fedha kutoka kwa Mashamba makubwa
yaliyopo Wilayani Siha na tufanye juhudi kuhakikisha masuala ya uwekezaji
katika Wilaya yetu yanaimarika zaidi hasa ule mradi mkubwa wa kituo cha Utalii.
Tusipofanya juhudi za makusudi kwenye suala la kuongezaukusanyaji wa Mapato ya
ndani ya Halmashauri naona uwezekano mkubwa wa Halmashauri yetu kushindwa kutoa
huduma zinastahili za kuwaletea Wananchi maendelea hasa katika Kata na Vijiji
vyetu.
(2)
UTUNZAJI WA MAZINGIRA
Waheshimiwa Madiwani,ndg Wananchi na Wataalam.
Napenda
kuendeleza kuwahimiza Wananchi na Wakazi wote wa Wilaya ya Siha kutumia vizuri
baraza za Mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa katika Wilaya yetu kwa kupanda miti ya kutosha ili kuimarisha
mazingira yetu na kurudisha uoto wa asili kama ilivyokuwa hapo miaka ya nyuma. naomba
kurudia tena ombi langu kwa Wananchi na Wakazi wa Wilaya ya Siha kuhakikisha kila kaya kuotesha angalau miti 5 kila mwaka
na kama inawezekana tuweke kwenye sheria ndogo za Halmashauri ambazo zitamtaka
kila mwenye eneo la ardhi kuotesha miti ya kutosha kulingana na ukubwa wa eneo
lake. Kwa hili naomba kurudia kwa kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Siha kuhakikisha kuwa Watendaji wa Kata na Vijiji katika Halmashauri ya
Siha kupitia vikao vya Vijiji na
Vitongoji wanawaelimisha wananchi kuhusu upandaji wa miti katika maeneo yao.
Ndugu Mkurugenzi agizo langu hili nitalifuatilia kwa karibu kuona jinsi gani
Serikali za Vijiji na Kata limelitekeleza kwa Vitendo na wale wote
watakaoshindwa kutekeleza naomba wachukuliwa hatua stahiki kwani wanapinga
suala zima la kuboresha mazingira ya Wilaya yetu. Nawaomba Viongozi wenzangu
tushirikiane kwa pamoja kuwaelimisha Wananchi katika Kata na Vijiji tunapotoka
ili kufanikisha zoezi hili muhimu kwa ustawi wa Wilaya yetu ya Siha..
Aidha,
najua adui mkubwa wa miti ni mifugo,naomba wote kwa pamoja tusaidiane kulinda
mifugo yetu ili isiharibu miti
tunayopanda kila mwaka katika maeneo yetu.
Waheshimiwa Madiwani,Ndugu Wananchi;
(3)ELIMU
Katika
suala la Elimu,Naombakutoa wito kwa wazazi na Walezi kutimiza wajibu wao ili
kuhakikisha kuwa watoto wao mashuleni wanapata mahitaji muhimu kama
vile,Madaftari,Kalamu,Sare za shule pamoja na chakula cha mchana wakiwa
shuleni. Hili nalirudia mara kwa mara kwa kuzingatia umuhimu wa elimu katika
maisha ya kila siku ya binadamu,Jamii na Taifa kwa ujumla wake.Sambamba na hilo
hivi karibuni kumefanyika Mtihani wa
Taifa wa Kidato cha Sita katika shule zetu za Oshara,Nuru,Sanya Juu na
Magadini na taarifa nilizopata ni kuwa mitihani hiyo imefanyika kwa utulivu wa
hali ya juu na hakuna jambo lolote lililo nje ya utaratibu limeripotiwa. Kwa
hili naipongeza ofisi ya Mkurugenzi kwa kusimamia zoezi hili hadi limefanyika
kwa ufanisi Mkubwa,Hata hivyo ni matumaini yetu kuwa matokeo ya Mtihani huo yatakuwa mazuri katika shule zetu za
Wilaya ya Siha pindi yatakapotangazwa na Idara/Wizara husika. Vilevile nimepata
taarifa kuwa Mitihani ya Majaribio ya Mkoa kwa Wanafunzi wa Kidato cha nne
(Mock) inatarajiwa kuanza hivi karibuni katika shule zetu za Sekondari Wilaya
ya Siha. Naomba kuwatakia Wanafunzi wote wa Kidato cha Nne kwa mwaka huu
kujiandaa vema kwa mitahani hiyo na Hatimaye kupata matokeo mazuri
yatakayoiwezesha Wilaya ya Siha kupata ufaulu mzuri. ’’ Elimu ni ufunguo wa maisha kila
mtu atimize wajibu wake ’’.
(4) UTUNZAJI WA BARABARA
Waheshimiwa Madiwani,Ndugu Wananchi;
Naomba tena kuwakumbusha wananchi wa Halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa kila
mmoja anashiriki kikamilifu katika
kuzitunza barabara zilizojengwa na Serikali katika Kata na Vijiji vyetu.
Pamoja na kuwa na Changamoto ya mvua zinazoendelea kunyesha katika Wilaya yetu
bado tunao wajibu wa kuendeleza kuzitunza barabara zilizopo katika maeneo yetu.
Kwa mfano utakuta mfereji wa maji umepasuka na maji yanaelekea barabarani
lakini mara nyingine kwa mshangao Serikali za maeneo husika hazichukui hatua
zinazotakiwa za kuziba maji hayo. Naomba kutoa Wito kwa Watendaji wa Vijiji na
Kata kwa kushirikiana na Wananchi wahakikishe kuwa barabara zote zilizopita
maeneo ya Vijiji na Kata zao zinalindwa hata kwa kuwapa adhabu wale wote
wanaoharibu barabara kwa makusudi.
Naomba kutoa agizo kuwa kuanzia sasa ni
marufuku kwa mtu yeyote kukata barabara
bila kibali cha Mkurugenzi Mtendaji na
yeyote atakayekiuka agizo hili basi achukuliwe hatua ili iwe fundisho kwa wenzake.
Mkutano wa baraza lililopita liliagiza tena hili lakini sijapata taarifa ya
Waharibifu wangapi wa barabara wamechukuliwa hatua za kisheria.
(5)UWAJIBIKAJI KAZINI
Waheshimiwa Madiwani,Ndugu Wananchi;
Kama
ilivyokuwa katika taarifa zangu kwa Baraza la Madiwani,napenda kuwakumbusha
tena Watumishi wa Serikali waliopo Wilaya ya Siha kuwa Serikali ya awamu ya
tano imeshasema kuwa haitawavumilia Watumishi wazembe na wabadhirifu kazini.
Naomba kila mtumishi atimize wajibu wake kwa mujibu wa taaluma aliyosomea na
kwa kufuata sheria na taratibu za utumishi wa Umma.
Aidha
,naomba kumwagiza Mkurugenzi kuwa Watumishi wote waliobainika kuwa na vyeti
visivyo sahihi(vyeti Feki) wasiruhusiwa kuwepo maeneo ya kazi katika
halmashauri yetu kama agizo la Mhe. Dkt John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania alilolitoa siku ya Mei Mosi katika uwanja wa Chuo cha
Ushirika Mjini Moshi. Mheshimiwa Rais aliagiza kuwa watumishi hao wasionekane
maeneo ya kazi ifikapo Mei 15,2017 na atakayeonekana atachukuliwa hatua za
kisheria. Mkurugenzi hili ni lako nakuomba usimamie kwa karibu kama bado
unaipenda kazi yako ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji,mimi kama Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Siha nimeona nikukumbushe hilo ili ufuatilie kwa karibu zaidi.
Waheshimiwa Madiwani na ndg Wananchi;
Kabla
ya kufika mwisho wa Taarifa yangu, napenda
kuwashukuru tena Wananchi wa Wilaya ya
Siha na Waheshimiwa Madiwani kwa
ushirikiano wenu wa dhati mnaoendelea
kunipatia kwa ajili ya kutekeleza majukumu yangu ya Kila siku. Naomba kuchukua
fursa hii kuwahimiza Wananchi wa Siha kuzitumia vema mvua zinazonyesha kwa ajili ya
mazao ya chakula na biashara bila kusahau uoteshaji wa miti katika maeneo yetu
ili kulinda mazingira. Kwani ipo kauli ya mazingira inayosema ’’MISITU NI UHAI’’. Naomba wote kwa umoja
wetu tufanye kazi kwa kushirikiana ili kuharakisha maendeleo yetu pamoja na
maendeleo ya Familia zetu , Wilaya ya
Siha na Taifa kwa ujumla wake.
Mwisho
kabisa ,nichukue fursa hii kwa niaba ya
baraza la Madiwani, kuwashukuru tena kwa usikivu wenu mkubwa mlionesha tangu
mwanzo wa taarifa yangu, naomba usikivu na utulivu huu uendelee hadi mwisho wa
Mkutano wetu na hatimaye tumalize na kuagana kwa upendo na furaha.
Asanteni sana kwa kunisikiliza
Imetolewa na:
Frank K. Tarimo
Mwenyekiti
wa Halmashauri (W)
SIHA
No comments:
Post a Comment