Wednesday 6 December 2017

Watumishi wa Umma Walevi kuchukuliwa hatua



WATUMISHI WA UMMA WALEVI WAONYWA SIHA

Watumishi wa Serikali wanaotumia pombe muda wa kazi Wilaya ya Siha wamepewa karipio la kuacha tabia hiyo mara moja vingenevyo watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Hayo yamesemwa na mkuu wa Wilaya ya Siha  mhe. Onesmo Buswelu katika ukumbi wa Kanisa katoliki  Sanya Juu alipokutana na walimu wa shule za Msingi Wilaya ya Siha siku ya jumatatu tarehe 04 desemba,2017.

Katika kikao kazi hicho kilichokuwa na lengo la kufanya tathmini ya matokeo ya darasa la saba mwaka 2017 pamoja na kutafuta mbinu za kuboresha kiwango cha ufaulu katika shule za msingi.

Mkuu wa Wilaya ya Siha alieleza kuwa wapo watumishi wa umma wakiwemo walimu ambao wanafika kazini wakiwa wamekunywa pombe ,jambo ambalo haliruhusiwi kisheria kwa watumishi wa Umma.

Alitoa wito kwa watumishi wote wa Umma Wilayani Siha wenye tabia ya ulevi kazini kuacha kitendo hicho cha aibu mara moja,kwani wasipofanya ivyo Serikali haitasita kuwachukulia hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi  na hata  kuwafukuza kazi kabisa.

Mhe Mkuu wa Wilaya  Siha aliwataka walimu wa Wilaya ya Siha kuendelea kuwa mfano bora katika kuzingatia maadili ya kazi ya ualimu pamoja na kuchapa kazi kwa bidii na maarifa huku wakijua kuwa serikali na jamii inawategemea walimu katika kujenga jamii imara na mathubuti.

Vile vile, aliwahakikishia walimu wa Wilaya ya Siha, kuwa Serikali ya awamu ya Tano chini ya Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuondoa kero mbalimbali za walimu ikiwa ni pamoja na kuwapa walimu  huduma kwa wakati pale wanapohitaji pamoja na kuboresha maslahi ya walimu.

Kwa upande wa jamii,Mkuu wa Wilaya alitoa wito kwa jamii na wazazi kuhakikisha kuwa wanafuatilia maendeleo ya kitaaluma ya  watoto wao mashuleni kwa lengo la kuongeza ufaulu.

Napenda kutoa agizo kwa watendaji wa Vijiji wakishirikiana na Serikali za Vijiji vyote Siha kuwachukulia hatua za kisheria wazazi wote wanaoacha kuwaandikisha shule watoto wenye umri wa kwenda shuleni alisema Buswelu.

Aidha aliwataka walimu kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika uboreshaji wa elimu hasa kwa walimu kufanya kazi kwa kujituma kama ilivyo katika maadili ya kazi hiyo.

Tuesday 5 December 2017

Kero za Walimu sasa kushughulikiwa




KERO ZA WALIMU KUSHUGHULIWA  SIHA
Kero mbalimbali za walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya siha kuendelea kushughulikiwa kwa karibu zaidi ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa shule za msingi na Sekondari.

Kauli hiyo imetolewa na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Siha Valerian Juwal mapema leo tarehe 4 desemba 2017 katika ukumbi wa mikutano wa RC Sanya Juu alipokutana na walimu wa shule za msingi kwa lengo la kufanya tathmini ya matokeo ya darasa la saba mwaka 2017.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha aliwataka walimu Wilaya ya Siha kufanya kazi kwa bidii na maarifa huku wakizingatia maadili ya kazi ya ualimu kwani taifa na jamii linawategemea walimu.

Alitoa wito kwa walimu wote wenye kero mbalimbali zinazowasumbua kufika ofisi ya mkurugenzi wakati wowote kwani ofisi yake ipo tayari kupokea na kutafutia ufumbuzi kero mbalimbali za walimu Wilaya Siha.

Hata hivyo,alieleza kuwa yapo matatizo na kero za walimu ambazo ofisi yake imekwisha zitatua mara baada ya kuzipokea kero hizo, naomba kutoa wito kwa walimu kutumia hata namba yangu ya simu kunipigia pale wanapoona kuwa hawapati huduma stahiki katika ofisi wanazofanyia kazi alisema Juwal.

Katika Tathmini hiyo ya matokeo ya darasa la saba kwa shule za msingi Siha mwaka 2017 shule zilizofanya vizuri ni pamoja na PUNCMI,SAMAKI,NGARONY,NKYARE,GARARAGUA,KYENGIA,FUKA ENG MED, LOKIRI NA FUKA.


Thursday 9 November 2017

DC SIHA kuwachongea Madiwani Kwa Wananchi




 Viongozi katika Wilaya ya Siha watakiwa kushiriki katika shughuli za maendeleo kikamilifu kwa lengo la kuwapatia Wananchi maendeleo ya kweli Chini ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na mhe. John Pombe Magufuli.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa Wilaya ya Siha mhe. Onesmo Buswelu mapema tarehe 8.11.2017 alipokuwa akikagua ujenzi wa wodi ya wazazi inayoendelea kujengwa hospitalini hapo Kwa michango ya Wananchi wa Wilaya ya Siha pamoja na wadau wengine wa maendeleo.

Alieleza kuwa wapo baadhi ya viongozi ambao bado hawajatoa michango yao hadi Sasa jambo ambapo linashangaza kuwa hawataki shughuli za maendeleo kufanikiwa au wana agenda yao binafsi aliuliza Buswelu.

Alisema kuwa wakati ukifika Kazi yake ni moja tu atawachongea Kwa wapiga Kura wao ili wawatambue kuwa viongozi waliowachagua hawataki maendeleo.

Mimi kama mkuu a Wilaya ya Siha napenda kuwakumbusha tena viongozi wenzangu tusiwaache Wananchi wenyewe katika suala la maendeleo kwani maendeleo ya kweli hayana itikadi za vyama wala ukabila wa Imani zetu za dini.

Aidha ,alieleza kuwa hata kama baadhi ya watu wenye nia mbaya na Siha hawatachangia na kushiriki katika uhamasishaji shughuli za maendeleo,Kazi  zitakwenda tu kwani wanaopinga maendeleo siku zote ni watu wachache.


Buswelu alitoa wito Kwa viongozi wa kuchaguliwa Wilaya Siha  kuendelea na Kazi ya kuwatumia Wananchi na kutimiza ahadi walizotoa wakati wakiomba Kura Kwa wananchi kama anavyofanya mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



Wednesday 1 November 2017

Siha yazindua zoezi la kupiga chapa mifugo Leo tarehe 01.11.2017

 Mkuu wa Wilaya ya Siha mhe.Onesmo Buswelu akizindua zoezi la kupiga chapa mifugo Kijiji cha Magadini Kata ya Gararagua Leo tar 01.11.2017

 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mhe. Valerian Juwal akishiriki katika zoezi la upigaji chapa mifugo katika Wilaya ya Siha leo tarehe 01.11.2017


Katibu Tawala wa Wilaya ya Siha Nicodemus John akishiriki katika zoezi la uzinduzi wa upigaji chapa mifugo katika Wilaya ya Siha.

Sunday 29 October 2017

Kata 3 bora, Kata 3 duni matokeo Darasa la Saba 2017- Siha

Kata 3 bora matokeo Darasa la Saba 2017 -Siha

  1. MITIMIREFU
  2. LEVISHI
  3. KIRUA
Kata 3 duni matokeo Darasa la Saba 2017 -Siha
  1. DONYOMURWAK 
  2. BIRIRI
  3. NDUMET

Thursday 26 October 2017

Shule 10 bora na shule 10 duni matokeo darasa la Saba 2017 Wilaya ya Siha

Shule 10 Bora matokeo darasa la Saba  2017 -SIHA
  1. PUNCHMI
  2. SAMAKI
  3. NGARONY
  4. NKYARE
  5. GARARAGUA
  6. NURU
  7. KYENGIA
  8. FUKA ENG MED
  9. LOKIRI
  10. FUKA
Shule 10 duni matokeo darasa la Saba 2017-SIHA
  1. KIRISHA
  2. SABUKU
  3. KANDASHI
  4. DONYOMURWA
  5. ROSELINE
  6. SANYA JUU
  7. MAKIWARU
  8. KISHISHA
  9. NAIBILI
  10. EMBUKOI



Wanawake Wapatiwa Mikopo




Vikundi 22 Wanawake vyapatiwa mikopo  2016/2017

Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro imefanikiwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi 22 vya wanawake Wilayani Siha katika mwaka wa fedha 2016/2017.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha Valerian Juwal alieleza hayo katika mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha.

Taarifa ya Mkurugenzi mtendaji ilieleza kuwa,katika mwaka wa fedha 2016/2017 halmashauri ya Wilaya ya Siha imetoa mikopo kwa vikundi  22 vya wanawake Wilayani Siha yenye thamani ya shilingi 56 ,000,000/= zikiwa ni fedha kutoka mchango wa Halmashauri wa asilimia tano (5%) ya mapato yake ya  ndani.

Aidha, Mkurugenzi katika taarifa yake alieleza Baraza kuwa pamoja na changamoto ya halmashauri kukabiliwa na vyanzo vichache vya ukusanyaji wa mapato lakini Halmashauri imejitahidi kutoa kiasi hicho cha fedha kwa vikundi vilivyoomba mikopo na vilivyotimiza vigezo vya kupata mikopo hiyo kwa kuzingatia sheria na taratibu mbalimbali.

Ametoa wito kwa vikundi vya wanawake katika wilaya ya Siha kutumia fursa hiyo ya Serikali  ya kuomba mikopo yenye masharti nafuu  katika kujikwamua kiuchumi katika ngazi ya Familia na jamii kwa ujumla wake.

Hata hivyo,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha ametoa wito kwa vikundi  mbalimbali vilivyopatiwa mikopo kutumia mikopo hiyo kwa shughuli waliojipangia  badala ya kutumia mikopo waliyopewa  katika mambo yasiyoleta tija.
Alieleza kuwa pamoja na jitihada za halmashauri kutoa mikopo hiyo kwa wanawake  lakini wahusika bado wanayo wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa mikopo hiyo inarejeshwa kwa wakati ili iweze kuwasaidia wanufaika wengine katika halmashauri ya Wilaya ya Siha.

Halmashauri ya Wilaya ya Siha katika upangaji wa mipango na bajeti kila mwaka inatenga asilimia 5 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya kuwawezesha wanawake na asilimia 5 ya mapato ya ndani ya Halmashauri  mikopo kwa vikundi vya vijana.


Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri ilitenga bajeti ya Tsh 87,051,850 kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya wanawake. Ambapo hadi kufikia Juni 2017 jumla ya vikundi ishirini na mbili (22) vya wanawake vilipatiwa mkopo wenye thamani ya Tshs 56,000,000/= zikiwa ni fedha kutoka mchango wa Halmashauri wa asilimia tano (5%) ya mapato ya ndani.

Wednesday 25 October 2017

Siha yafanikiwa zoezi la utoaji wa chanjo mwaka 2016/2017




Utoaji wa Chanjo Wafanikiwa  Wilaya ya Siha mwaka 2016/2017
Halmashauri ya Wilaya ya Siha Mkoa wa Kilimanjaro imefikia zaidi ya asimia 96 ya huduma  ya utoaji wa chanjo mbalimbali ya kujikinga na magonjwa kwa watoto Wilayani hapa.

Katika taarifa ya mwaka 2016/2017 iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji  wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha  Valerian Juwal katika mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani lililokutana mwezi Oktoba katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha.

Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji ilieleza kuwa katika huduma ya utoaji wa chanjo mbalimbali kwa watoto, halmashauri ya Wilaya ya Siha imefanikiwa kutoa chanjo ya matone ya vitamin A na dawa za minyoo hadi kufikia asilimia 96.7

Aidha taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji ilieleza kuwa,katika huduma ya utoaji wa chanjo ya kansa ya shingo ya kizazi kwa watoto wa kike wenye umri  chini ya miaka 14,zoezi hilo pia  lilifanikiwa kwa  zaidi ya asilimia 87.

Mkurugenzi Mtendaji alieleza  Baraza la Madiwani kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Siha ni  miongoni mwa Halmashauri za Wilaya hapa nchini zilizofanya vizuri katika usimamiaji wa zoezi zima la utoaji chanjo kwa watoto.

Alieleza kuwa siri ya mafanikio  ya zoezi hilo ni ushirikiana wa dhati  baina ya Wananchi ,viongozi na wadau wengine wa maendeleo katika Wilaya ya Siha.

Hata hivyo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Siha aliwaomba wananchi na viongozi wa Siha kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuboresha afya ya wananchi wake hasa utoaji wa chanjo unaosaidia kutoa kinga mbalimbali kwa watoto.

Vile vile,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha alieleza Baraza la Madiwani kuwa huduma ya chanjo zote alizozitaja hutolewa bure kwa kugharamiwa na Serikali na hivyo kuwataka wananchi kutoa taarifa mara moja iwapo watatokea watu wanaowadai fedha za kulipia huduma hiyo.


Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012 Halmashauri ya Wilaya ya Siha inajumla ya watu 116,313 wakiwemo wanaume 56,500 na wanawake 59,813.