Monday 24 July 2017

Mabingwa wa baseball Tanzania waendelea na mazoezi Siha





Mabingwa wa mchezo wa baseball Tanzania  Shule ya sekondari Sanya Juu (Sanya day) iliyopo wilaya ya siha Mkoa wa kilimanjaro wamewaongoza wanafunzi na walimu wa wilaya za mkoa wa Kilimanjaro katika mazoezi ya mchezo wa baseball yaliyofanyika katika uwanja wa shule ya sekondari Sanya juu.
Wanafunzi wa Sanya day ambao ni mabingwa wa Tanzania kwa mchezo wa Baseball,waliongoza mazoezi hayo kwa muda wa siku tatu mfufulizo kuanzia tarehe mwishoni mwa wiki chini ya mkufunzi wa michezo kutoka Japan Hiroki Iwasaki.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika siku ya kufunga mazoezi hayo,afisa michezo mkoa wa Kilimanjaro ndugu Antony  Ishumi  alieleza kuwa Serikali ya Japan imetoa zaidi ya shilingi milioni 160 kwa ajili ya kuendeleza mchezo huo hapa nchini.
Afisa wa michezo mkoa alieleza kuwa, mchezo wa baseball ni mchezo ambao bado haujulikani sana hapa nchini ndiyo maana Serikali ya Japan kupitia shirika lake la maendeleo JICA limeamua kutoa elimu kwa walimu wa michezo kwa shule za msingi na Sekondari hapa nchini.
Ndugu Ishumi alimweleza mgeni rasmi kuwa mchezo wa baseball  utakuwa miongoni mwa michezo itakayojumuishwa katika michezo ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo Japan 2020.
Pia afisa huyo wa michezo  mkoa  Kilimanjaro alieleza kuwa, mkoa wa Kilimanjaro umechaguliwa na kuwa kituo kikuu cha kambi ya timu ya wachezaji chini ya umri wa miaka 12 ambao kimsingi watakuwa wanafunzi wa shule za msingi. Pia alimweleza mgeni rasmi kuwa kambi ya wachezaji chini ya miaka 23 hapa Tanzania itakuwa katika mkoa wa Mwanza.
Mgeni rasmi katika siku ya kufunga mafunzo hayo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Siha Valerian Juwal  alianza kwa kuipongeza shule ya sekondari Sanya Juu kwa kuwa mabingwa wa Tanzania kwa mchezo wa baseball na kuiletea sifa Wilaya ya Siha na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla wake.
Mkurugenzi mtendaji Siha alisema kuwa ,Halmashauri ya Siha itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha kuwa shule hiyo inaendelea kufanya vizuri katika mchezo huo na shule za jirani kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kuimarisha kikosi cha Wilaya ya Siha kitakachoshiriki mchezo huo mwezi Desemba 2017.
Vilevile, Valerian Juwal alimpongeza mchezaji wa shule ya sekondari Sanya Juu mwanafunzi Noel Mmari kwa kuwa mchezaji bora wa mchezo wa baseball hapa nchini Tanzania na kujumuishwa katika wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania kwa mchezo huo.
Alitoa wito kwa wanafunzi wengine kuiga mfano wa mwanafunzi huyo Noel Mmari kwani ameiletea sifa kubwa Wilaya ya Siha na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.
Mafunzo ya mchezo wa Baseball mkoa wa Kilimanjaro yalianza rasmi tarehe 21/07/2017 na kuhitinishwa  tarehe 24/7/2017 na zaidi ya wanamichezo 60 wakiwemo walimu na wanafunzi kutoka Wilaya za Rombo,Moshi,Siha na Mwanga walishiriki na kutunukiwa vyeti.

DC siha aagiza kufunguliwa kwa duka la dawa hospital ya Wilaya




Mkuu wa wilaya ya siha mkoa wa Kilimanjaro mhe Onesmo Buswelu amemwagiza mganga mkuu wa hospital ya Wilaya ya siha kuhakikisha anafungua duka la dawa katika hospital ya Wilaya ya siha haraka iwezekanavyo.

Mkuu  wa wilaya ya Siha ameyasema hayo hivi karibuni alivyokuwa katika zoezi la kufungua mfumo wa kieletroniki(GoTHOMIS) katika hospital ya wilaya ya siha.

Alieleza kuwa kuwepo kwa duka la dawa ndani ya hospital ya Wilaya kutasaidia kuboresha huduma zilizopo na kwa upande mwingine ni kutimiza agizo la Serikali  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma zilizo katika viwango vya juu.

Mhe Onesmo buswelu aliwataka wataalam wa afya kuhakikisha wanautumia vema mfumo huo katika kuboresha utoaji wa  huduma bora kwa wagonjwa wanaofika katika hospital hiyo.

Wilaya ya Siha inajumla ya vituo vya afya 5,zahanati 14 na Hospital 2 ambazo zinawahudumia zaidi ya wakazi wa Siha 116,313.

Friday 21 July 2017

DC siha atoa siku saba hospital ya Wilaya kufunga generator hospital ya Wilaya ya Siha




Mkuu wa wilaya ya siha mhe. Onesmo Buswelu ametoa siku saba kwa mganga mkuu wa hospital ya wilaya ya siha kufunga generator katika hospital hiyo.

Hayo ameyasema tarehe 20.7.2017 katika hospital ya Wilaya ya Siha iliyopo eneo la Sanya Juu ,wakati akizindua mfumo wa kieletroniki kwa ajili ya kukusanya na uboreshaji wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa katika hospital ya wilaya.

Mkuu wa Wilaya aliwataka waganga na wauguzi kufanya kazi kwa juhudi zaidi ili kutimiza lengo la serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ya kuwapatia wananchi huduma bora za afya na siyo bora huduma.

Alieleza kuwa yeye kama mkuu wa wilaya ataufuatilia utendaji kazi wa mfumo huo ili kuona kama wataalam wanautumia ipasavyo katika kuongeza huduma kwa wananchi na kuboresha ukusanyaji wa mapato kwa sehemu nyingine.

Awali mkuu wa Wilaya ya Siha alimpongeza mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha kwa kugharamia ufungaji wa mfumo huo kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri na kutekeleza agizo la Serikali  kuwa kila hospital ya wilaya kufunga mfumo wa kieletroniki kwa ajili ya ukusanyaji wa kumbukumbu na utoaji wa huduma.

Awali,mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Siha Valerian Juwal alieleza kuwa Halmashauri ya Siha itaendelea kutekeleza na kusimamia mfumo huo kwa karibu ili kuhakikisha kuwa unaleta tija kwa manufaa ya wananchi na serikali kwa ujumla.

Halmashauri ya Wilaya ya Siha imetumia jumla ya  fedha za Kitanzania Shilingi 15,642,000 ambazo ni mapato ya ndani katika kukamilisha ufungaji wa mfumo huo katika hospital ya Wilaya ya Siha

Thursday 20 July 2017

picha uzinduzi mfumo wa kieletroniki hospital ya wilaya ya siha tarehe 20.7.2017






picha za uzinduzi wa mfumo wa kieletroniki hospital ya wilaya ya siha

 mkuu wa Wilaya ya siha mhe Onesmo Buswelu akizindua mfumo wa kieletroniki katika hospital ya wilaya leo tarehe 20.7.2017
mkuu wa wilaya ya Siha Mhe Onesmo Buswelu (wa pili kutoka kushoto) akipokea matumizi ya mfumo wa kieletroniki kutoka kwa mganga mkuu wa hospital ya wilaya Dr Andrew Method (aliyesimama kulia)

Mfumo wa kieletroniki wazinduliwa rasmi Hospital ya Wilaya ya Siha





Hatimaye hospital ya Wilaya ya siha yaanza kutumia mfumo mpya wa kieletroniki katika utoaji wa huduma za matibabu hospitalini hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Siha mhe Onesmo Buswelu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tukio hilo ,amezindua mfumo huo rasmi leo tarehe 20.7.2017 katika hospital ya wilaya ya siha na kuagiza mganga mkuu wa Hospital ya Wilaya kuhakikisha kuwa mfumo huo unatumika katika malengo yaliyokusudiwa.
Mhe Mkuu wa Wilaya ya Siha amewataka waganga na wauguzi katika hospital ya Wilaya na maeneo mengine wajitahidi kufanya kazi za kuwahudumia wananchi  kwa uadilifu na kuwaonya wale wachache wanaotumia kauli zisizofaa kwa wagonjwa kuwa siku zao zinahesabika.
Mimi nawaamini sana waganga na wauguzi waliopo katika zahanati na vituo vyote vya kutolea huduma katika wilaya ya siha kwani sijapata malalamiko mengi kuhusu lugha mbaya kwa wagonjwa mnaowahudumia,alisema Buswelu.
Mganga mkuu wa Hospital ya Wilaya ya Siha Dr Andrew Method alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa,mfumo uliozinduliwa umegharamiwa na halmashauri ya Wilaya ya Siha kwa kutumia mapato ya ndani na jumla ya shilingi milioni 15 zimetumika.
Alieleza kuwa kukamilika  kwa mfumo huo kutasaidia kuboresha huduma katika hospital ya wilaya ya siha hasa uhifadhi wa takwimu na kumbukumbu za wagonjwa na kuachana na mfumo wa hapo nyuma ambapo kumbukumbu za wagonjwa zilikuwa zinahifadhiwa katika mafaili  na majalada.
Pia mganga mkuu alisema faida nyingine ya mfumo ni pamoja na kuharakisha utoaji wa vipimo,kuonesha akiba ya madawa iliyopo na kusaidia katika ukusanyaji wa mapato yanayotokana na uchangiaji wa huduma kutoka kwa wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha Valerian Juwal alisema kuwa kuwekwa kwa mfumo wa kieletroniki katika hospital ya Wilaya ya Siha ni agizo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa, kila hospital ya wilaya ifunge na kutumia mfumo wa kieletroniki ifikapo Juni 30 2017.
Valerian Juwal Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Siha alimweleza mgeni rasmi kuwa,japo halmashauri yake inakusanya vyanzo vichache vya mapato lakini wamejibana hadi kufikia hatua za kupata fedha za kutimiza agizo la Serikali.


Tuesday 18 July 2017

Moto wakosesha kaya 18 makazi Kijiji cha Ngarenairobi

 Moto ukiendelea kuwaka kabla ya kuzimwa eneo la tukio tarehe 17.07.2017

Sehemu ya eneo lililoteketezwa na moto huo Kijiji cha Ngarenairobi tarehe 17.07.2017
NB: kaya 18 zenye wakazi 42 zakosa makazi baada ya nyumba mbili zenye vyumba 21 kuteketea kwa moto.wananchi walioathirika wamehifadhiwa kwa majirani zao na kupatiwa huduma mbalimbali muhimu.

Familia 18 zaathirika na Janga la Moto kijiji cha Ngarenairobi

Moto mkubwa ulizuka jana tarehe 17.07.2017 na kuteketeza makazi ya watu katika kijiji cha Ngarenairobi,kata ya Ngarenairobi tarafa ya Siha magharibi Wilaya ya Siha.

Taarifa za awali za kuzuka kwa moto huo zilipatikana kutoka uongozi wa Kijiji cha Ngarenairobi kupitia ofisa mtendaji wa kijiji  hicho ndugu Seif Mwigamba ilieleza kuwa moto huo ulizuka mnamo saa saba mchana na kuteketeza makazi ya familia 18 zenye wakazi 42

Mwenyekiti wa kijiji hicho Stanley Nkini alisema kuwa wananchi walishirikiana kwa pamoja kuuzima moto huo ambao ungeweza kuteketeza nyumba nyingi zilizokuwa katika eneo hilo.

Mwenyekiti huyo aliwashukuru wananchi wa kijiji cha ngarenairobi pamoja na kampuni ya wachina(CGC) wanayojenga barabara ya Lami karibu na eneo hilo kwa msaada wao mkubwa wa kusaidiana na wananchi katika kukabiliana na moto.

 Nyumba moja  ya mbao yenye vyumba 16 na  nyumba nyingine  yenye vyumba vitano iliteketea kabisa na moto huo na kuacha familia hizo 18 zenye wakazi 42 bila ya kuwa na kitu chochote alisema Nkini.

Hata hivyo,kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ilifika eneo la tukio na kujionea uharibifu uliofanywa na moto huo na kutoa maelekezo kwa ofisi ya kata na vijiji kuwapa hifadhi wananchi waliopatwa na janga la moto.
 Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na ufuatiliaji bado unaendelea kujua kiini halisi cha kutokea kwa moto.

Monday 17 July 2017

Oshara yaongoza matokeo ya kidato cha sita 2017 shule za Wilaya ya Siha




Oshara yaongoza matokeo kidato cha sita 2017 Wilaya ya Siha
Shule ya sekondari Oshara iliyopo kata ya Ivaeny,Tarafa ya Siha mashariki imepata matokeo mazuri ya kidato cha sita na kuwa vinara kwa shule za Wilaya ya Siha kwa  mwaka wa pili mfululizo.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana na kutolewa na tovuti ya baraza la mitihani la taifa nectar,matokeo hayo yameonesha kuwa shule ya Sekondari oshara imeendelea kuwa vinara katika matokeo ya kidato cha sita Wilaya ya Siha.
Matokeo hayo ya kidato cha sita yanaonesha kuwa ufaulu wa wanafunzi shuleni hapo ni kama ifuatavyo: daraja la kwanza wanafunzi  ,daraja la pili wanafunzi   ,daraja la tatu wanafunzi  .
Katika matokeo hayo hakuna mwanafunzi aliyepata daraja la nne wala sifuri na shule imeshika nafasi ya 5 kimkoa kati ya shule 43,pia shule hiyo imeshika nafasi ya 55 Kitaifa kati ya shule 449.
Wilaya ya Siha inajumla ya shule 7 za sekondari zilizofanya mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka 2017,kati ya shule hizo shule 4 ni za Serikali na 3 za taasisi za dini.