WATUMISHI WA
UMMA WALEVI WAONYWA SIHA
Watumishi wa Serikali wanaotumia pombe muda
wa kazi Wilaya ya Siha wamepewa karipio la kuacha tabia hiyo mara moja
vingenevyo watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Hayo yamesemwa na mkuu wa Wilaya ya Siha mhe. Onesmo Buswelu katika ukumbi wa Kanisa
katoliki Sanya Juu alipokutana na walimu
wa shule za Msingi Wilaya ya Siha siku ya jumatatu tarehe 04 desemba,2017.
Katika kikao kazi hicho kilichokuwa na lengo
la kufanya tathmini ya matokeo ya darasa la saba mwaka 2017 pamoja na kutafuta
mbinu za kuboresha kiwango cha ufaulu katika shule za msingi.
Mkuu wa Wilaya ya Siha alieleza kuwa wapo
watumishi wa umma wakiwemo walimu ambao wanafika kazini wakiwa wamekunywa pombe
,jambo ambalo haliruhusiwi kisheria kwa watumishi wa Umma.
Alitoa wito kwa watumishi wote wa Umma
Wilayani Siha wenye tabia ya ulevi kazini kuacha kitendo hicho cha aibu mara
moja,kwani wasipofanya ivyo Serikali haitasita kuwachukulia hatua stahiki ikiwa
ni pamoja na kuwasimamisha kazi na
hata kuwafukuza kazi kabisa.
Mhe Mkuu wa Wilaya Siha aliwataka walimu wa Wilaya ya Siha
kuendelea kuwa mfano bora katika kuzingatia maadili ya kazi ya ualimu pamoja na
kuchapa kazi kwa bidii na maarifa huku wakijua kuwa serikali na jamii
inawategemea walimu katika kujenga jamii imara na mathubuti.
Vile vile, aliwahakikishia walimu wa Wilaya
ya Siha, kuwa Serikali ya awamu ya Tano chini ya Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuondoa kero
mbalimbali za walimu ikiwa ni pamoja na kuwapa walimu huduma kwa wakati pale wanapohitaji pamoja na
kuboresha maslahi ya walimu.
Kwa upande wa jamii,Mkuu wa Wilaya alitoa
wito kwa jamii na wazazi kuhakikisha kuwa wanafuatilia maendeleo ya kitaaluma
ya watoto wao mashuleni kwa lengo la
kuongeza ufaulu.
Napenda kutoa agizo kwa watendaji wa Vijiji
wakishirikiana na Serikali za Vijiji vyote Siha kuwachukulia hatua za kisheria
wazazi wote wanaoacha kuwaandikisha shule watoto wenye umri wa kwenda shuleni
alisema Buswelu.
Aidha aliwataka walimu kuendelea kuunga mkono
juhudi za Serikali ya Tanzania katika uboreshaji wa elimu hasa kwa walimu
kufanya kazi kwa kujituma kama ilivyo katika maadili ya kazi hiyo.
No comments:
Post a Comment