Wananchi wa Kata ya Kirua Wilayani Siha pamoja na Wazazi wa
wanafunzi wanaosoma katika shule ya Sekondari Fuka wamekubaliana kwa kauli moja
kukamilisha kazi ya ujenzi wa maabara tatu za masomo ya Sayansi katika shule
hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Wananchi hao walipokuwa Wakiongea
katika Mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Siha alioufanya katika shule ya Sekondari
Fuka tarehe 16.5.2017.
Awali Mkuu wa Shule hiyo mwalimu Swalehe Kombo alisoma taarifa fupi ya maendeleo ya ujenzi wa
Maabara katika shule hiyo ambapo alieleza kuwa zaidi ya shilingi milioni 5
zimetumika katika kuendeleza ujenzi wa maabara katika kipindi cha Novemba,2016
hadi Mei 15,2017.
Mkuu wa Shule hiyo alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa, Wananchi wa Kata ya Kirua wameweka mpango wa
kupata michango ya Shilingi elfu tano kwa kila kaya ,ambapo kupatikana kwa
fedha hizo kutasaidia kuendeleza ujenzi wa Maabara katika shule hiyo.
Akiongea na Wananchi na Wazazi wa wanafunzi wanaosoma shule
ya Sekondari Fuka iliyopo Kata ya Kirua,Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe.
Onesmo Buswelu aliwapongeza Wananchi kwa kuwa kuonyesha hali ya kujituma na
moyo ya kuchangia maendeleo hasa katika
suala la elimu kwa watoto wao.
Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa Serikali itaendelea na
jitihada zake za kushirikiana na Wananchi pamoja na wadau wa maendeleo katika
kuleta maendeleo, na katika ujenzi wa maabara Serikali imeahidi kuleta vifaa vyote
katika maabara hizo. Alifafanua kuwa
vifaa vya maabara vitakavyoletwa na Serikali ni vya gharama kubwa na vitahitaji
kutunzwa na kuhifadhiwa kwa uangalifu na shule husika zitakazokabidhiwa.
Wilaya ya Siha inajumla ya shule 13 za Serikali ambapo kila
shule inahitaji kuwa na maabara 3 kwa masomo ya Biolojia,Chemia na Fizikia kama
ilivyo agizo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment