JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS TAMISEMI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU
KAZI ZILIZOTEKELEZWA NA SERIKALI WILAYANI SIHA
Ndugu Wanahabari,na Wananchi
Napenda
kuchukua fursa hii kuwakaribisha sana
katika Wilaya ya Siha ili niweze kukutana
nanyi kwa lengo la kutoa taarifa ya
mambo mbalimbali ya maendeleo yanayoendelea katika Wilaya ya Siha tangu
Serikali ya Awamu ya tano ilipoingia madarakani chini ya Mhe. Dkt John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Kabla sijaanza kutoa taarifa yangu naomba kuishukuru Serikali yetu
kwa kutupatia fedha za kutekeleza miradi
ya maendeleo katika Wilaya yetu ya Siha.
Pili
napenda kuwashukuru Wananchi wote wa Wilaya ya Siha kwa kushirikiana na
Serikali yao katika shughuli za miradi ya
maendeleo pamoja na suala zima la
utunzaji wa Amani katika Wilaya yetu.
Ndugu Wanahabari
Nianze
na hali ya ulinzi na usalama, kwa ujumla Wilaya ya Siha ni salama kabisa na
hakuna tukio lolote ambalo limetokea la kuhatarisha amani na hii imetokana na
tabia njema ya Wananchi wa Wilaya ya Siha
kama walivyo Watanzania wengine kuwa na utamaduni wa kudumisha amani, kipekee
nawashukuru Wananchi na wakazi wa Wilaya ya
Siha kwa kuendelea kudumisha amani wakati wote hasa katika sikukuu ya
Pasaka mwaka huu 2017 iliyofanyika
tarehe 16-17/04/2017, ambapo kuwepo
kwa amani kumesaidia Wananchi kuendelea na shughuli za kiuchumi ambazo
zinawapatia kipato ikiwemo shughuli za Kilimo,Ufugaji na biashara ndogondogo.
Ndugu Wanahabari,
Katika
kutekeleza miradi ya maendeleo Serikali ya awamu ya tano imewezesha miradi
mbalimbali kukamilika na mingine inaendelea kukamilishwa katika hatua
mbalimbali. Miongoni mwa miradi iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya Tano
Chini ya Mhe.Dkt John Pombe Magufuli ni
kama ifuatavyo;-
1. Katika
sekta ya Kilimo,Ushirika na Umwagiliaji,Serikali imewezesha na kuleta fedha
Wilayani Siha kiasi cha Tshs. 165,000,000/= zilizowezesha kukamilisha
ujenzi wa mita 1000 za mfereji wa maji ya Umwagiliaji Kijiji cha Kishisha Kata
ya Ivaeny. Pia Serikali imetoa fedha
kiasi cha Tshs 165,000,000/= kwa
ajili ya ujenzi wa mfereji wa
umwagiliaji Kijiji cha Mowonjamu Kata ya Livishi wenye urefu wa mita 700 na kujenga bwawa la
kuhifadhia maji . Baadhi ya Kazi zimekamilika na nyingine zipo katika hatua
mbalimbali za ukamilishaji. Vile vile
kama mnavyoona mvua kwa sasa ni nyingi na mazao mashambani yanaendelea vizuri
na matajio yetu kama Wilaya ya Siha ni kupat
tani 102,705 kwa mazao ya chakula na Biashara, Pia Wilaya inategemea kupata
tani 10,126 kwa mazao ya Bustani na mbogamboga. Pia kutokana na mvua
zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika Wilaya yetu ya Siha naomba kutoa wito
kwa Wananchi kuchukua tahadhari ili kujiepusha na madhara yanayoweza kujitokeza
hasa kuangalia Wanafunzi wanaokwenda shuleni asubuhi wasije kuzolewa na maji.
2. Mfuko
wa Wanawake na Vijana. Katika kipindi kifupi tangu Serikali ya awamu ya Tano
kuingia madarakani Jumla ya FedhaTsh. 75,000,000/=
zimetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Siha Siha kwa ajili ya Kusaidia vikundi
mbalimbali vya Wanawake na Vijana. Katika Fedha hizo jumla ya vikundi 20 vya
Wanawake vyenye wanufaika 316 wamepatiwa mikopo, Pamoja na vikundi 7 vya vijana
vyenye wanufaika 130 vimewezeshwa kupitia asilimia 10 ya Mapato ya Ndani ya
Halmashauri ya Siha. Hata hivyo Nimetoa agizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa asilimia 5 ya vijana na 5 ya Wanawake
inatolewa katika Makusanyo ya Mapato ya ndani ya Halmashauri ili kuwezesha kuongeza wanufaika wengi zaidi katika Makundi
ya Vijana na Wanawake.
3. Katika
Sekta ya Afya; Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia fedha jumla ya Tsh. 250,000,000/= kwa ajili ya kukamilisha
jengo la OPD sakafu ya juu katika Hospital yetu ya Wilaya ya Siha. Kazi hii
inafanyika kwa kupitia “force account” na inasimamiwa na Wataalam na Watumishi wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Siha. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwezi Juni,2017.
Serikali ya Wilaya ya Siha imeamua kutumia “force
account” ili kuhakikisha kuwa fedha za Serikali zinatumika vizuri na kutoa
thamani halisi ya fedha. Aidha kwa upande mwingine Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya
Siha kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji imepanga kufanya harambee
ambayo itawezezesha ujenzi wa majengo matatu (Wodi ya Wazazi,Wodi ya Watoto na
Jengo la upasuaji) Majengo haya yana thamani ya Fedha za Kitanzania
880,000,000/=. Mpango huu umeshirikisha Wanannchi wa Wilaya ya Siha, wadau wa
maendeleo wa ndani na nje ya Halmashauri pamoja na Watumishi wa Wilaya ya Siha.
Lengo la mpango huu ni kuwaondolea usumbufu na kuwapunguzia Wananchi wa Siha gharama za matibabu kwa
wagonjwa wao hasa wanapopewa rufaa katika Hospital ya Mkoa Mawenzi na Hospital ya
Rufaa ya KCMC mjini Moshi.
Hata
hivyo hadi sasa Jumla ya Tsh. 52,000,000/=
zimepatikana na vifaa vya ujenzi vyenye
thamani ya Tsh 11,000,000/= vimetolewa
na wadau mbalimbali na Wananchi ,huku ahadi zenye thamani ya Tsh milioni 62
zikitarajiwa kupokewa ili kukamilisha ujenzi huo. Hata hivyo michango
iliyotolewa, ahadi na vifaa vilivyotolewa zinafikia jumla ya Tshs 125,000,000/=.Hadi
sasa ujenzi wa wodi ya wazazi umeanza na
ujenzi wa Msingi umekamilika na kazi ya
ujenzi inategemewa kukamilika mwezi Julai,2017 kama wadau na wananchi waliotoa
ahadi zao watakamilisha kwa wakati. Hata hivyo Serikali imeongeza kiwango cha ununuzi
wa dawa katika Zahanati na vituo vya Afya vya Serikali kutoka asilimia 25%
mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 85% mwaka huu.
Ndg Wanahabari.
Napenda kuwashukuru Wananchi wa Siha kwa ushirikiano wa dhati walionesha katika
ujenzi wa kazi hii muhimu, na napenda
kutoa wito kwa Wananchi,Watumishi na Wadau wengine wa maendeleo kukamilisha
ahadi zao walizotoa ili kufanikisha mpango huu wa ujenzi kwa wakati. Vilevile
natoa wito kwa Wananchi na wadau wengine nje na ndani ya Wilaya kutuunga mkono
katika ujenzi wa Hospital ya Wilaya ya Siha.
4. Sekta ya Elimu. Serikali ya awamu ya Tano
imeendelea kutimiza azma yake ya kutoa elimu bure kuanzia darasa la awali hadi
kidato cha Nne kwa kuhakikisha kuwa Mahitaji muhimu ya shule yanapatikana kama vile vitabu,mishahara ya Watumishi,vifaa
muhimu vya maabara mpya zilizojengwa, mafunzo kwa watumishi hasa Walimu wa
Shule za Msingi na Sekondari yametolewa ili kuwajengea uwezo. Katika sekta ya Elimu,
Serikali ya awamu ya tano imeweza kujenga nyumba mbili za Walimu(Six in one)
katika shule za Sekondari Suumu na Namwai kwa gharama ya Tsh.300,000,000/=, hadi sasa nyumba hizo zimekamilika na zimeanza kutumika na Walimu wa shule husika.
Pia Serikali imetoa fedha jumla ya Tsh. 24,000,000/= za ukarabati wa madarasa matatu katika shule ya Sekondari
Suumu na kazi imekamilika. Vile vile Serikali imetoa Tsh. Milioni 36 kwa ajili
ya ujenzi wa matundu 18 ya vyoo katika shule ya Sekondari Namwai na
Suumu(Namwai matundu 16 na Suumu matundu 2). Kwa kipindi hiki pia Serikali
imetoa Jumla ya Tsh milioni 71 za ujenzi wa Bweni la Wanafunzi katika shule ya
Sekondari Oshara, kazi hii inaendelea na inatarajiwa kukamilika mwezi Julai
2017. Katika kuboresha Elimu Serikali
imetoa jumla ya madawati 537 Wilayani
Siha ili kuonesha kwa vitendo azma ya kuboresha elimu kwa jamii ya watanzania.
Madawati haya yamegawanywa katika shule za Msingi na Sekondari za Serikali
Wilaya ya Siha na kusaidia kuondoa upungufu wa
madawati uliokuwepo hapo awali. Hadi sasa Wilaya ya Siha inayo madawati
ya ziada 747 kwa kujumuisha Elimu
Msingi na Sekondari. Halmashauri ya Wilaya ya Siha inapokea kila mwezi jumla ya
Kiasi cha Fedha za Kitanzania shilingi 38,093,000/= Katika kutekeleza elimu
bila malipo katika shule za Sekondari na Kiasi cha Shilingi 29,187,000/= hutolewa na Serikali Kila
mwezi ili kugharamia elimu kwa shule za msingi. Pia Serikali imetoa
jumla ya vitabu 6834 kwa shule za
Sekondari Wilaya ya Siha katika masomo ya Sanaa na Sanyansi. Wito wangu
kwa Wanafunzi wote waliopo mashuleni kuhakikisha kuwa wanasoma kwa bidii na
maarifa kwani jamii na Taifa linawategemea wao katika kuleta maendeleo ya familia
zao,Jamii na Taifa kwa Ujumla wake. Pia nawahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii ili
kuondokana na kuwa na vyeti Feki kama baadhi ya watumishi wa Umma walivyogundulika
katika maeneo mbalimbali hapa Nchini kuwa na vyeti feki, hii ilitokana na wao
kutosoma kwa bidii wakati wakiwa wanafunzi.
Ndugu Wanahabari;
Vilevile
katika kuboresha miundombinu ya barabara Serikali ya Awamu ya tano chini ya
uongozi bora wa Mhe John Pombe Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza ujenzi wa barabara ya kiwango
cha Lami kutoka Sanya Juu hadi Elerai
yenye urefu wa Km 32.2 kwa gharama ya fedha za Kitanzania shilingi bilioni 52.3. Ujenzi wa barabara hii kwa
kiwango cha Lami umeanza rasmi mwezi Machi mwaka huu na unatarajiwa kukamilika
mwezi Oktoba,2018. Kukamilika kwa barabara hii kutasaidia kufungua fursa za
uchumi katika Tarafa ya Siha Magharibi na Wilaya ya Siha kwa ujumla, hasa
kusaidia kupitisha watalii zaidi wanaopanda mlima Kilimanjaro kupitia lango la
Londorosi pamoja na kurahisisha kusafirisha mazao mbalimbali yanalimwa kwa
wingi katika mashamba makubwa ya West Kilimanjaro. Pia Serikali imeendelea
kutoa fedha za kuwezesha ujenzi wa barabara
ndani ya wilaya ya Siha kwa viwango vya
Changarawe, miongoni mwa barabara hizo ni kama ifuatavyo;-i)Ujenzi wa barabara
ya Kifufu Mowonjam na Ngirini, Nsherehehe hadi Ngarony yenye urefu wa km 14.6
kwa gharama ya fedha za Kitanzania shilingi 829,954,000/= na kazi ya ujenzi imekamilika. (ii)Barabara ya
Karansi Tanki la maji yenye urefu wa Km
6.4 iliyogharimu kiasi cha Tshs. 633,024,100/=imekamilika (iii) Pia Serikali
imetoa fedha zilizowezesha ujenzi wa Kalvati kubwa la Kisube Kirisha na
ujenzi wa barabara yenye urefu wa Km 2.5 kwa gharama ya shilingi za Kitanzania 920,172,587.50/= kazi hii ya ujenzi
imekamilika na ipo katika kipindi cha uangalizi.
Ndugu Wanahabari:
Aidha,
katika miradi ya Maji Serikali ya awamu ya tano imetoa fedha Kiasi cha Tsh. 1,682,062,000/= Wilayani Siha kwa ajili
ukarabati na upanuzi wa mradi wa maji Magadini Makiwaru katika vijiji vya (Wiri,Mawasiliano,Lekrimuni,kandashi
na Orkolili) na mradi wa Maji lawate Fuka katika vijiji vya
Kishisha,Donyomuruak,Embukoi,Ngaritati na Naibili). Kazi za ukarabati katika
miradi hii ya maji imekamilika na Wananchi wa Siha wanapata maji safi na Salama
katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Siha.
Ndugu Wanahabari,
Katika
mpango wa Serikali wa kunusuru Kaya Maskini kupitia Mradi wa TASAF III,Jumla ya
Kaya Maskini 1871 Wilaya ya Siha zimewezeshwa na kunufaika na mpango huu wa
Serikali wa kunusuru Kaya Maskini na Jumla ya Fedha za Kitanzania Shilingi 691,638,636/= zimetumika. Kwa niaba ya
Wananchi wa Wilaya ya Siha napenda kutoa shukrani za dhati kwa Serikali yetu
tukufu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusaidia jamii ya Watanzania hasa
kaya zisizo na uwezo. Wito wangu kwa wanufaika wa mpango huu, napenda kuwaasa
wanufaika wote kuwa na nidhamu bora ya matumizi ya fedha wanazopatiwa na
Serikali kupitia mpango huu.
Ndugu Wanahabari:
Soko
la Sanya Juu, katika kuboresha miundombinu ya soko kuu la Wilaya ya Siha yaani soko
la Sanya Juu,Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosimamiwa na Chama
Cha Mapinduzi imetoa jumla ya shilingi 71,161,200/= kwa Halmashauri ya siha
ili kusaidia kuboresha miundombinu katika soko hilo. Kwa sasa taratibu
zinaendelea na kazi hiyo inatarajiwa kuanza mwezi wa Juni,2017. Mimi Mkuu wa
Wilaya ya Siha na msimamizi wa shughuli za Serikali Wilaya ya Siha nimemwagiza
Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa viwango
vinavyotakiwa ili kuonyesha thamani halisi ya fedha za Umma zilizotolewa.
Ndugu Wanahabari:
Katika
hatua za kuharakisha maendeleo ya Wananchi Wilaya ya Siha,Serikali kwa mwaka
huu wa fedha 2016/2017 imetoa Fedha za
mfuko wa Jimbo jumla shilingi 29,084,000/=
kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ya Wananchi katika Kata na vijiji
mbalimbali Wilayani Siha. Kwa niaba ya Wananchi wa Siha napenda tena kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kutuletea fedha za mfuko wa Jimbo ambazo kimsingi zinatusaidia
sana katika maendeleo ya Wananchi ya Wilaya yetu ya Siha.
Ndugu Wanahabari:
Serikali
ya Wilaya ya Siha inapenda kuwashukuru Wananchi na Wakazi wa wote wa Wilaya
Siha, wadau wa maendeleo pamoja na Sekta Binafsi kwa kutoa ushirikiano hasa katika shughuli za
maendeleo bila kujali tofauti za itikadi za Kisiasa ,maeneo watu wanapotoka na
imani zetu za madhehebu ya Dini. Kwa kufuata misingi ambayo baba wa Taifa
mwalimu Julius K Nyerere alituachia, Wilaya ya Siha tunategemea kuendelea kupata maendeleo makubwa ndani ya muda mfupi
ujao. Naomba kutoa wito kwa Wananchi, Wadau wa maendeleo na Viongozi wote Wilayani Siha kudumisha
mshikamano uliopo ili kutimiza malengo ya Serikali ya awamu ya tano katika
kuwaletea Wananchi wake maendeleo ya kweli.
Ndugu Wanahabari:
Vilevile,
kabla ya kufikia mwisho wa taarifa yangu,naomba kutoa wito kwa Watumishi wote
wa Umma kufanya kazi za kuwahudumia Wananchi
kwa uadilifu na weledi mkubwa ili kulinda heshima ya Watumishi wa Umma
na Serikali kwa ujumla. Serikali ya awamu ya tano haipo tayari
kuwavumilia watumishi wazembe,wavivu ,walarushwa pamoja na wale wote wanaofanya
kazi kwa mazoea.
Ndugu Wanahabari,
Mwisho
Serikali ya Wilaya ya Siha kwa kuzingatia muongozo wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (2015-2020) itaendelea kusimamia na kuratibu miradi yote ya
maendeleo ili kuhakikisha kuwa fedha za Serikali zinatumika kwa malengo tu
yaliyokusudiwa. Natoa wito kwa watumishi wote wa Umma Wilayani Siha kuhakikisha
kuwa wanasimamia Ilani ya Chama Tawala na kutimiza malengo yaliyowekwa na
Serikali ya awamu ya Tano chini ya uongozi bora wa Mheshimiwa John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mungu
ibariki Afrika,Mungu ibariki Tanzania na
Mungu ibariki Wilaya ya Siha
asanteni
sana kwa kunisikiliza
Imetolewa
na:-
Mhe; ONESMO M. BUSWELU
MKUU WA WILAYA YA SIHA
Leo tarehe 12/05/2017
No comments:
Post a Comment