Wednesday, 14 June 2017

Serikali Wilaya ya Siha yapiga Marufuku biashara ya mahindi ya kuchoma




Uongozi wa Serikali katika Wilaya ya Siha Mkoa wa Kilimanjaro  umepiga marufuku biashara ya mahindi ya kuchoma katika maeneo yote Wilayani hapa.

Azimio hilo limetolewa leo tarehe 14 Juni,2017 na Wenyeviti wa Vijiji Wilaya ya Siha walipokutana  na Mkuu wa Wilaya ya Siha katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha kwa lengo la kuzungumzia mambo mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Siha.

Wenyeviti hao wa Vijiji  kwa kauli moja walimwomba Katibu Tawala wa Wilaya ya Siha Mhe. Nicodemus John   ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Siha kuwa,kutokana na wizi wa mahindi mabichi unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya Siha wameona ni bora kumwomba Mkuu wa Wilaya kupiga marufuku biashara hiyo hadi mazao ya mahindi  yatakapovunwa mashambani.

Katika Azimio hilo,sababu zilizotolewa na Viongozi hao za kutoa ombi kwa Mkuu wa Wilaya ya Siha kupiga marufuku biashara hiyo ni pamoja na kuzuia wizi wa mahindi mashambani  na sababu nyingine ni jitihada za kuhakikisha chakula kitakachovunwa kinatumika vizuri kwa manufaa ya ustawi wa jamii.

Aidha katika kikao hicho,Mwenyekiti wa Kijiji cha Wiri Mheshimiwa Hamza Munisi aliishukuru Serikali ya Wilaya ya Siha kwa jinsi inavyosimamia kikamilifu sheria mbalimbali hasa za uhifadhi na utunzaji wa mazingira katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Hamza pia alishauri kuwa wale wote wanaofanya biashara ya mahindi ya kuchoma ni vema watafute biashara nyingine kwa wakati huu katazo hilo linapotolewa rasmi.


Akichangia na kujibu hoja mbalimbali za Wenyeviti wa Vijiji katika Mkutano huo,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha Valerian Juwal aliwashukuru Wenyeviti wa Vijiji vyote Wilayani Siha kwa ushirikiano wanaendelea kuutoa kwa serikali kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya Wananchi Wilayani Siha.

Mkurugenzi Mtendaji aliwaahidi Wenyeviti hao kuwa,Halmashauri ya Siha itaendelea kufanya kazi kwa misingi ya kufuata  Sheria zilizopo na kuwataka Watendaji wa umma kuhakikisha wanachapa kazi kwa uadilifu na kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wowote.

Kutokana na sensa ya idadi ya watu na makazi ya mwaka 2012,Wilaya ya Siha inajumla ya watu 116313 kati yao  Wanawake wakiwa 59813 na Wanaume 56500

No comments:

Post a Comment