Thursday, 1 June 2017

Uandikishaji Darasa la Kwanza 2017 asilimia 99




Zoezi la uandikishaji wanafunzi wa darasa la kwanza katika shule za msingi Wilayani Siha umetia fora kwa mwaka 2017. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa  kwa mgeni Rasmi  Mhe Onesmo Buswelu Mkuu wa Wilaya ya Siha katika maazimisho ya siku ya elimu Wilayani Siha yaliyofanyika katika shule ya msingi Sanya Juu tarehe 30.5.2017.

Uandikishaji wa Wanafunzi katika shule za msingi umefanyika kwa mafanikio makubwa na jumla ya Wavulana 1690 na wasichana 1675  ambapo jumla ya Wanafunzi wote waliandikishwa ni 3365 sawa na asilimia 99 ya lengo la uandikishaji kwa  mwaka 2017.


Taarifa iliyotolewa ilieleza kuwa Kufanikiwa kwa zoezi hili la uandikisha kumetokana na Sera ya Serikali ya Tanzania ya Elimu bila malipo kuanzia kidato awali hadi kidato cha Nne.

Halmashauri ya Wilaya ya Siha ilikuwa imeweka lengo la kuandikisha jumla la wanafunzi 3405 wakiwemo wasichana 1655 na wavulana 1753 kwa mwaka 2017.

Aidha, moja ya sababu ya kutofikiwa malengo ya uandikishaji wa wanafunzi kwa asilimia 100 umetokana na baadhi ya jamii ya wafugaji kuwa na tabia ya kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa lengo la kufuata malisho ya mifugo yao.

Akiongea na wadau wa elimu ,Wanafunzi,Walimu na Wazazi Wilayani Siha Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe.Onesmo Buswelu aliwataka wazazi na Walezi kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuchochea ufaulu wa Wanafunzi katika Shule za Msingi na Sekondari.

Mkuu wa Wilaya ya Siha, alisema kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea kutoa ajira kwa walimu ili kuziba upungufu  wa walimu uliopo katika baadhi ya shule hasa walimu wa masomo ya Sayansi na hisabati.

Halmashauri ya Wilaya ya Siha imesajili jumla ya wanafunzi 23,198 wa shule za msingi kati yao wavulana 11,594 na wasichana 11,604, ambapo kwa shule za sekondari kuna jumla ya wanafunzi 7,121 wakiwemo wavulana 2,919 na wasichana 4,202 hivyo kufanya jumla ya wanafunzi wote  katika shule za msingi na Sekondari  Wilayani Siha kufikia 30,319.

No comments:

Post a Comment