Monday 27 February 2017

TAARIFA YA MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA SIHA BARAZA LA MADIWANI TAREHE 24.2.2017





OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
HALMASHAURI YA WILAYA YA SIHA


TAARIFA YA MWENYEKITI  WA HALMASHAURI   MKUTANO  WA KAWAIDA WA  BARAZA LA MADIWANI  KATIKA KIPINDI CHA ROBO YA PILI (OKTOBA -DESEMBA,2016).
v  Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Siha,
v  Mwakilishi Ofisi ya RAS-Mkoa wa Kilimanjaro,
v  Mh. Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Siha,
v  Mh. Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Siha,
v  Waheshimiwa Madiwani,
v  Mkurugenzi Halmashauri ya Siha,
v  Viongozi wa Dini,
v  Wageni Waalikwa,
v  Ndugu Wataalamu,
v  Waandishi wa Habari,
v  Wananchi wa Wilaya ya Siha,
v  Mabibi na Mabwana,

Wasalaam Alekumu,Tumsifu Yesu Kristo,Bwana Yesu asifiwe


  
Wah. Madiwani ,  na Ndugu  Wananchi;
Naomba tusimame kwa dk moja ili kuwakumbuka wale wote waliopoteza maisha katika kipindi cha mwisho wa  mwaka 2016 na hasa mwenzetu Mheshimiwa Anna A Masaki diwani wa viti maalum (W) alifariki mapema mwaka huu 2017
Habarini za mwaka mpya 2017, ni matumaini yangu kuwa mmevuka mwaka salama na wote mnaendelea na majukumu yenu  ya kuwatumikia wananchi kama kawaida.

 (1)UTUNZAJI WA CHAKULA
Waheshimiwa Madiwani na ndugu Wananchi.
Napenda kuwaomba na kuwakumbusha tena Wananchi wa Halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa tunakuwa na tabia ya kutunza chakula kilichopo kwani hali ya hewa kama mnavyoiona kuwa siyo nzuri sana  hasa baada ya mvua ya vuli kukosekana. Mimi kama mwenyekiti wa Halmashauri ya Siha napenda kutoa rai kwa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wengine katika ngazi za Kata na Vijiji tushirikiane kwa pamoja kuwaelimisha wananchi kuhusu elimu ya utunzaji wa chakula hasa katika ngazi ya Kaya na Vijiji. Pia nawaomba viongozi wa Madhehebu ya Dini tushirikiane kwa pamoja katika kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa  utunzaji na uhifadhi wa chakula . Kipekee namshukuru Mkuu wetu wa Wilaya ya Siha kwa kuweka agizo la kuzuia matumizi ya mahindi katika kutengenezea pombe za kienyeji hasa Dadii(nzuga) kama sehemu ya kunusuru matumizi ya nafaka yasiyo ya  lazima.

(2)UKUSANYAJI WA MAPATO
Waheshimiwa Madiwani,
Pamoja na Halmashauri yetu kukabiliwa na tatizo ya vyanzo vichache na vya kudumu vya mapato yake ya ndani, Halmashauri imeendelea kukusanya mapato yake ya ndani kwa kutumia  Vijiji vilivyopo katika maeneo yenye  vyanzo vya mapato na kwa kutumia mashine za kieletroniki kukusanya mapato hayo kama ilivyoagizo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Hata hivyo Halmashauri ya Siha bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa vyanzo vya uhakika na  vya kudumu vya  mapato hali ambayo inatufanya sisi sote kama viongozi kuendelea kubuni vyanzo mbadala vya kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri yetu.

(3) UTUNZAJI WA MAZINGIRA
Waheshimiwa Madiwani,ndg  Wananchi na Wataalam.
Ndugu zangu hali ya ukame mnayoiona katika Wilaya yetu imetokana na  shughuli za kibinadamu zilizosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira. Ili kunusuru hali hii isiendelee katika maeneo yetu ya Wilaya ya Siha, naomba kutoa mapendekezo ya kila kaya kuotesha angalau miti 5 kila mwaka na kama inawezekana tuweke kwenye sheria ndogo za Halmashauri ambazo zitamtaka kila mwenye eneo la ardhi kuotesha miti ya kutosha kulingana na ukubwa wa eneo lake. Kwa hili naomba kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa Watendaji wa Kata na Vijiji katika Halmashauri ya Siha  kupitia vikao vya Vijiji na Vitongoji wanawaelimisha wananchi kuhusu upandaji wa miti katika maeneo yao. Pia wenye mashamba makubwa tutafanya utaratibu wa kuwaomba waotesha miti angalau 500 kila mwaka ili kunusuru Wilaya ya Siha kugeuka kuwa jangwa.
Aidha, najua adui mkubwa wa miti ni mifugo,naomba wote kwa pamoja tusaidiane kulinda mifugo  yetu ili isiharibu miti tunayopanda kila mwaka. 

 (4) MIFUGO KUTOKA NJE YA WILAYA
Waheshimiwa Madiwani,Ndugu Wananchi;
 Naomba kutoa agizo kwa Viongozi wa Vijiji na Kata hasa watendaji wa Vijiji kuhakikisha kuwa hakuna mifugo inayoingia ndani ya vijiji na kata zetu kutoka Wilaya au mikoa jirani. Kimsingi  mifugo hii inasababisha kuongezeka kwa uharibifu wa mazingira Wilayani Siha na kusababisha kuongezeka kwa magonjwa ya mifugo kwa  mifugo yetu,mfano mzuri ni ugonjwa hatari wa kimeta ambao kimsingi umetoka nje ya Wilaya yetu.naomba viongozi wenzangu tusaidiane kulisimamia hili na pale inapopatikana mifugo kutoka nje ya maeneo yetu basi hatua za kisheria zichukuliwe hasa za kutoza faini stahili kulingana na sheria zilizopo  ili kuongeza mapato ya Halmashauri. Ofisi yangu inamwomba Mkuu wa Wilaya ya Siha kutusaidia jambo hili kwani wakati mwingine litahitaji nguvu za dola katika kulitekeleza ipasavyo.

(5) UTUNZAJI WA BARABARA
Waheshimiwa Madiwani,Ndugu Wananchi;
 Naomba tena kuwakumbusha wananchi wa  Halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa kila mmoja anashiriki kikamilifu katika  kuzitunza barabara zilizojengwa na Serikali katika Kata na Vijiji vyetu. Serikali inatoa pesa nyingi kutengeneza barabara hizo ambazo zimeanza kuharibiwa na baadhi ya watu kwa kuzikata kwa kupitisha mifereji au mabomba bila kibali cha Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji. Naomba Mkurugenzi uwaagize watendaji wako wa Kata na Vijiji kwa kushirikiana na Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji kulisimamia agizo hili  kwa ukaribu zaidi. Naomba kutoa agizo kuwa kuanzia sasa ni marufuku kwa mtu yeyote  kukata barabara bila kibali cha Mkurugenzi Mtendaji  na yeyote atakayekiuka hilo achukuliwe hatua ili iwe fundisho kwa wenzake.

(6)UWAJIBIKAJI KAZINI
Waheshimiwa Madiwani,Ndugu Wananchi;
Napenda kuwakumbusha tena Watumishi wa Serikali waliopo Wilaya ya Siha kuwa Serikali ya awamu ya tano imeshasema kuwa haitawavumilia watumishi wazembe na wabadhirifu kazini. Naomba kila mtumishi atimize wajibu wake kwa mujibu wa taaluma aliyosomea na kwa kufuata sheria na taratibu za utumishi wa Umma. 

Aidha ,naomba kuwakumbusha tena wazazi/walezi kuwa shule za msingi na sekondari zimeshafunguliwa  tangu mwezi wa Januari,2017 na wajibu wao  ni kuhakikisha kuwa watoto wote wanakwenda shuleni na ni jukumu lao  kuwawezesha watoto wao  kupata chakula mashuleni. Naomba viongozi wote tushirikiane  kuwaelimishe wazazi/walezi ili kutimiza majukumu ya kuwapatia mahitaji muhimu watoto wao hasa mlo wa mchana.Elimu ni ufunguo wa maisha kila  mtu atimize wajibu wake.
Waheshimiwa  Madiwani na ndg Wananchi;
Kabla ya kufika mwisho wa Taarifa yangu, napenda  kuwashukuru tena Wananchi wa Wilaya ya  Siha na Waheshimiwa Madiwani  kwa ushirikiano  wenu wa dhati mnaoendelea kunipatia kwa ajili ya kutekeleza majukumu yangu ya Kila siku. Naomba kuchukua fursa hii kuwahimiza wananchi wa Siha kujiandaa vema na msimu mkubwa wa mvua za masika ambao  tumezoea unaanza mwezi Machi kila mwaka. Naomba wote kwa umoja wetu tufanye kazi kwa bidii kwa maendeleo ya Familia zetu , Wilaya ya Siha na Taifa kwa ujumla wake.
Mwisho ,nichukue fursa hii kwa niaba ya baraza la Madiwani, kuwashukuru tena kwa usikivu wenu mkubwa mlionesha tangu mwanzo wa taarifa yangu, naomba usikivu na utulivu huu uendelee hadi mwisho wa mkutano wetu na hatimaye tumalize na kuagana kwa upendo na furaha. Aidha,Napenda kuishukuru tena Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Siha kwa ushirikiano mzuri hasa wa kuhamasisha shughuli za maendeleo katika Wilaya yetu
Asanteni sana kwa kunisikiliza
Imetolewa na:
Frank K. Tarimo
Mwenyekiti wa Halmashauri (W)
SIHA
 Tarehe 24.2.2017

No comments:

Post a Comment