Monday 24 July 2017

Mabingwa wa baseball Tanzania waendelea na mazoezi Siha





Mabingwa wa mchezo wa baseball Tanzania  Shule ya sekondari Sanya Juu (Sanya day) iliyopo wilaya ya siha Mkoa wa kilimanjaro wamewaongoza wanafunzi na walimu wa wilaya za mkoa wa Kilimanjaro katika mazoezi ya mchezo wa baseball yaliyofanyika katika uwanja wa shule ya sekondari Sanya juu.
Wanafunzi wa Sanya day ambao ni mabingwa wa Tanzania kwa mchezo wa Baseball,waliongoza mazoezi hayo kwa muda wa siku tatu mfufulizo kuanzia tarehe mwishoni mwa wiki chini ya mkufunzi wa michezo kutoka Japan Hiroki Iwasaki.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika siku ya kufunga mazoezi hayo,afisa michezo mkoa wa Kilimanjaro ndugu Antony  Ishumi  alieleza kuwa Serikali ya Japan imetoa zaidi ya shilingi milioni 160 kwa ajili ya kuendeleza mchezo huo hapa nchini.
Afisa wa michezo mkoa alieleza kuwa, mchezo wa baseball ni mchezo ambao bado haujulikani sana hapa nchini ndiyo maana Serikali ya Japan kupitia shirika lake la maendeleo JICA limeamua kutoa elimu kwa walimu wa michezo kwa shule za msingi na Sekondari hapa nchini.
Ndugu Ishumi alimweleza mgeni rasmi kuwa mchezo wa baseball  utakuwa miongoni mwa michezo itakayojumuishwa katika michezo ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo Japan 2020.
Pia afisa huyo wa michezo  mkoa  Kilimanjaro alieleza kuwa, mkoa wa Kilimanjaro umechaguliwa na kuwa kituo kikuu cha kambi ya timu ya wachezaji chini ya umri wa miaka 12 ambao kimsingi watakuwa wanafunzi wa shule za msingi. Pia alimweleza mgeni rasmi kuwa kambi ya wachezaji chini ya miaka 23 hapa Tanzania itakuwa katika mkoa wa Mwanza.
Mgeni rasmi katika siku ya kufunga mafunzo hayo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Siha Valerian Juwal  alianza kwa kuipongeza shule ya sekondari Sanya Juu kwa kuwa mabingwa wa Tanzania kwa mchezo wa baseball na kuiletea sifa Wilaya ya Siha na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla wake.
Mkurugenzi mtendaji Siha alisema kuwa ,Halmashauri ya Siha itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha kuwa shule hiyo inaendelea kufanya vizuri katika mchezo huo na shule za jirani kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kuimarisha kikosi cha Wilaya ya Siha kitakachoshiriki mchezo huo mwezi Desemba 2017.
Vilevile, Valerian Juwal alimpongeza mchezaji wa shule ya sekondari Sanya Juu mwanafunzi Noel Mmari kwa kuwa mchezaji bora wa mchezo wa baseball hapa nchini Tanzania na kujumuishwa katika wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania kwa mchezo huo.
Alitoa wito kwa wanafunzi wengine kuiga mfano wa mwanafunzi huyo Noel Mmari kwani ameiletea sifa kubwa Wilaya ya Siha na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.
Mafunzo ya mchezo wa Baseball mkoa wa Kilimanjaro yalianza rasmi tarehe 21/07/2017 na kuhitinishwa  tarehe 24/7/2017 na zaidi ya wanamichezo 60 wakiwemo walimu na wanafunzi kutoka Wilaya za Rombo,Moshi,Siha na Mwanga walishiriki na kutunukiwa vyeti.

No comments:

Post a Comment