Wednesday, 6 September 2017

Wanafunzi 2304 kuhitimu elimu ya msingi Wilaya ya Siha 2017

Jumla ya Wanafunzi 2304 wanatarajiwa kumaliza elimu ya msingi katika shule mbalimbali za msingi Halmashauri ya Wilaya ya Siha kwa mwaka 2017. Kati ya wanafunzi hao wavulana ni 1137 na wasichana ni 1167.

Wanafunzi hao wanatarajiwa kufanya  mitihani hiyo ya taifa ya kuhitimu masomo ya shule za msingi  kwa muda wa siku mbili tarehe 6/09/2017 na tarehe 07/09/2017.

Mitihani hiyo ya taifa itafanyika katika vituo 55 vilivyopangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Siha, kati ya vituo hivyo 52 ni shule za Serikali  ambao watafanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na vituo 3 binafsi na Taasisi za Kidini ambazo ni English Medium .

Thursday, 10 August 2017

Siha kutumia tekinolojia kuendeleza kilimo na ufugaji Bora
Halmashauri ya Wilaya ya Siha kueneza tekinolojia mpya  ya kilimo  na ufugaji bora katika ngazi ya Halmashauri , Kata na  hatimaye katika vijiji vyote. 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha Valerian Juwal alipokuwa katika kilele cha maonesho ya nanenane yaliyofanyika kikanda katika viwanja vya Njiro Arusha ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Siha ilipata fursa ya kuonesha tekinolojia mbalimbali ya kilimo na mifugo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha alisema kuwa Halmashauri ya Siha itahakikisha kuwa mashamba Darasa yaliyopo kila kata yanaendelezwa ili kuwanufaisha wananchi wa maeneo husika na vijiji jirani.

Alieleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Siha itawatumia wataalam wa kilimo na mifugo waliopo katika ngazi ya Halmashauri ,Kata na Vijiji kuhakikisha wakulima wanapatiwa utaalam na ushauri wa kilimo na ufugaji wa kisasa ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na ufugaji.

Juwal aliwataka wananchi kuondokana na kilimo  na ufugaji wa kitamaduni na badala yake wabadilike na kuanza kulima na kufuga kwa kufuata tekinolojia mpya ambazo zitawasaidia kuongeza kipato na kuondokana na kuwa na vipato duni.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Siha ametoa wito kwa viongozi mbalimbali Wilayani Siha kuendelea kuwahamasisha wananchi kuzingatia ushauri wanaopewa na wataalam wa kilimo na mifugo waliopo katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo pia.

Zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Wilaya ya Siha wanategemea kilimo na ufugaji kama shughuli kubwa za kiuchumi kwa wananchi hao.mazao yanayolimwa kwa wingi zaidi ni Mahindi,maharage,viazi,ndizi,ngano,shairi na mazao ya mbogamboga.


Tuesday, 1 August 2017

Jukwaa la Wanawake yazinduliwa rasmi SihaJukwaa la Wanawake yazinduliwa rasmi Siha
Wilaya ya siha mkoa wa Kilimanjaro limefanikiwa kuzindua jukwa la wanawake kufuatia agizo la serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kuwa kila wilaya kuwa na jukwaa hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Siha mhe Onesmo Buswelu amezindua jukwa hilo rasmi leo tarehe 01 Agosti 2017 ambapo uzinduzi huo umefantika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki uliopo katika Kata ya Sanya Juu.

Katika hotuba aliyoitoa kwa wanawake wa Wilaya ya Siha,mhe Onesmo Buswelu ambaye pia alikuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo aliwataka wanawake kujiamini na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ya Tanzania katika kujiletea maendeleo ndani ya jamii.

Alieleza kuwa Serikali inatambua kuwa mwanamke akipata elimu jamii itakuwa imeelimika kwa ujumla,hivyo wanawake wachangamke katika kujiunga na vikundi mbalimbali ili waweze kupatiwa mikopo na elimu ya ujasilia mali na ukuzaji wa uchumi.

Aidha,mkuu huyo wa Wilaya ya Siha aliwaambia wanawake kuwa Halmashauri ya Siha inatenga bajeti ya asilimia 5 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya wanawake na asilimia 5 ya mikopo kwa vijana  kila mwaka wa fedha.

Katika uzinduzi huo wa jukwaa la Wanawake pia uongozi wa wilaya ulichaguliwa na viongozi waliochaguliwa walikuwa kama ifuatavyo:- Mwenyekiti wa jukwaa la wanawake alichaguliwa Christina P kavishe na Katibu wa Jukwaa la wanawake ni Aisha S.  Mwiru.

Baada ya uchaguzi huo, mwenyekiti wa jukwaa la wanawake wilaya ya Siha Christine Kavishe aliwashukuru kinamama wote waliomchagua na kuahidi kuwaunganisha wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa na imani zao za madhehebu ya  dini.

Monday, 24 July 2017

Mabingwa wa baseball Tanzania waendelea na mazoezi Siha

Mabingwa wa mchezo wa baseball Tanzania  Shule ya sekondari Sanya Juu (Sanya day) iliyopo wilaya ya siha Mkoa wa kilimanjaro wamewaongoza wanafunzi na walimu wa wilaya za mkoa wa Kilimanjaro katika mazoezi ya mchezo wa baseball yaliyofanyika katika uwanja wa shule ya sekondari Sanya juu.
Wanafunzi wa Sanya day ambao ni mabingwa wa Tanzania kwa mchezo wa Baseball,waliongoza mazoezi hayo kwa muda wa siku tatu mfufulizo kuanzia tarehe mwishoni mwa wiki chini ya mkufunzi wa michezo kutoka Japan Hiroki Iwasaki.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika siku ya kufunga mazoezi hayo,afisa michezo mkoa wa Kilimanjaro ndugu Antony  Ishumi  alieleza kuwa Serikali ya Japan imetoa zaidi ya shilingi milioni 160 kwa ajili ya kuendeleza mchezo huo hapa nchini.
Afisa wa michezo mkoa alieleza kuwa, mchezo wa baseball ni mchezo ambao bado haujulikani sana hapa nchini ndiyo maana Serikali ya Japan kupitia shirika lake la maendeleo JICA limeamua kutoa elimu kwa walimu wa michezo kwa shule za msingi na Sekondari hapa nchini.
Ndugu Ishumi alimweleza mgeni rasmi kuwa mchezo wa baseball  utakuwa miongoni mwa michezo itakayojumuishwa katika michezo ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo Japan 2020.
Pia afisa huyo wa michezo  mkoa  Kilimanjaro alieleza kuwa, mkoa wa Kilimanjaro umechaguliwa na kuwa kituo kikuu cha kambi ya timu ya wachezaji chini ya umri wa miaka 12 ambao kimsingi watakuwa wanafunzi wa shule za msingi. Pia alimweleza mgeni rasmi kuwa kambi ya wachezaji chini ya miaka 23 hapa Tanzania itakuwa katika mkoa wa Mwanza.
Mgeni rasmi katika siku ya kufunga mafunzo hayo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Siha Valerian Juwal  alianza kwa kuipongeza shule ya sekondari Sanya Juu kwa kuwa mabingwa wa Tanzania kwa mchezo wa baseball na kuiletea sifa Wilaya ya Siha na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla wake.
Mkurugenzi mtendaji Siha alisema kuwa ,Halmashauri ya Siha itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha kuwa shule hiyo inaendelea kufanya vizuri katika mchezo huo na shule za jirani kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kuimarisha kikosi cha Wilaya ya Siha kitakachoshiriki mchezo huo mwezi Desemba 2017.
Vilevile, Valerian Juwal alimpongeza mchezaji wa shule ya sekondari Sanya Juu mwanafunzi Noel Mmari kwa kuwa mchezaji bora wa mchezo wa baseball hapa nchini Tanzania na kujumuishwa katika wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania kwa mchezo huo.
Alitoa wito kwa wanafunzi wengine kuiga mfano wa mwanafunzi huyo Noel Mmari kwani ameiletea sifa kubwa Wilaya ya Siha na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.
Mafunzo ya mchezo wa Baseball mkoa wa Kilimanjaro yalianza rasmi tarehe 21/07/2017 na kuhitinishwa  tarehe 24/7/2017 na zaidi ya wanamichezo 60 wakiwemo walimu na wanafunzi kutoka Wilaya za Rombo,Moshi,Siha na Mwanga walishiriki na kutunukiwa vyeti.

DC siha aagiza kufunguliwa kwa duka la dawa hospital ya Wilaya
Mkuu wa wilaya ya siha mkoa wa Kilimanjaro mhe Onesmo Buswelu amemwagiza mganga mkuu wa hospital ya Wilaya ya siha kuhakikisha anafungua duka la dawa katika hospital ya Wilaya ya siha haraka iwezekanavyo.

Mkuu  wa wilaya ya Siha ameyasema hayo hivi karibuni alivyokuwa katika zoezi la kufungua mfumo wa kieletroniki(GoTHOMIS) katika hospital ya wilaya ya siha.

Alieleza kuwa kuwepo kwa duka la dawa ndani ya hospital ya Wilaya kutasaidia kuboresha huduma zilizopo na kwa upande mwingine ni kutimiza agizo la Serikali  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma zilizo katika viwango vya juu.

Mhe Onesmo buswelu aliwataka wataalam wa afya kuhakikisha wanautumia vema mfumo huo katika kuboresha utoaji wa  huduma bora kwa wagonjwa wanaofika katika hospital hiyo.

Wilaya ya Siha inajumla ya vituo vya afya 5,zahanati 14 na Hospital 2 ambazo zinawahudumia zaidi ya wakazi wa Siha 116,313.