Thursday 25 April 2019

BARABARA ZA SIHA ZABORESHWA

Wakala wa usimamizi wa barabara za mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Siha wameendelea kutekeleza azma ya Serikali ya awamu ya tano kwa vitendo kwa kuzifanyia matengenezo barabara za vijijini katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Siha.
Kwa Ujumla barabara zote katika Vijiji na Vitongoji Wilayani Siha zinapitika wakati wote na kusaidia shughuli mbalimbali za wananchi katika kusafiri na kusafirisha mazao mbalimbali ya biashara na chakula

Hii ni barabara ya Siha Sango hadi Kijiji cha Mese Wilayani Siha ikiendelea kufanyiwa matengenezo makubwa  kupitia TARURA

WAZAZI WATAKIWA KUWAPA ELIMU WATOTO BILA UBAGUZI-SIHA

Wananchi wa Wilaya ya Siha wameshauriwa kuwapa watoto wote elimu bila ubaguzi wa aina yoyote
Hayo yamesemwa na Mwalimu Rose Sandi  Afisa elimu shule za Msingi katika Halmashauri ya Wilayani  ya Siha  leo tarehe 2.04.2019 aliposhiriki na watoto wenye mahitaji maalumu (siku ya Usonji) katika maazimisho ya siku yao duniani.
Watoto wenye usonji wakishirikiana na wazazi wao katika zoezi la kupanda miti mapema leo katika shule ya msingi Sanya Juu
Maazimisho hayo katika Wilaya ya Siha yamefanyika katika shule ya Msingi Sanya juu na kujumuisha watoto wenye mahitaji maalumu kutoka shule mbalimbali za msingi Wilayani Siha ikiwemo shule ya Msingi  Faraja Siha .
Wanafunzi wa shule ya msingi Sanya Juu wakishiriki maazimisho ya siku ya Usonji dunia leo tarehe 2.4.2019
Katika Maazimisho hayo wazazi na jamii imetakiwa kuwapa elimu watoto wote katika familia bila   ubaguzi wa jinsia,maumbile au uwezo wa watoto katika kuelewa na kuchanganua mambo mbalimbali.

SIHA YAPATA MAFANIKIO UTOAJI ELIMU MAALUM

SIHA YAPATA MAFANIKIO ELIMU MAALUM
Halmashauri ya Wilaya ya Siha Mkoa wa Kilimanjaro imekuwa miongoni mwa Halmashauri za mfano katika kutoa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu (watoto wenye Usonji).Hayo yamebainika katika maazimisho ya siku ya Usonji dunia ambayo kila mwaka hufanyika tarehe 2 April,,ambapo katika Wilaya ya Siha mwaka 2019 yamefanyika katika Shule ya Msingi Sanya Juu.
Katika kutekeleza uboreshaji wa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum,Halmashauri ya Wilaya ya Siha inazo jumla ya shule 4 za msingi zinazotoa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum(Usonji) ,shule hizo ni pamoja na Shule ya Msingi Nuru,Sanya Juu,Faraja na shule ya Msingi Naibili.
Katika shule hizo kwa mwaka huu 2019 zina jumla ya watoto 147 ambapo watoto wote wanaosoma wana mahitaji maalum(Usonji) ,Aidha walimu wenye taaluma ya kutosha na waliobobea wanafundisha shule hizo kulingana na mahitaji ya watoto husika.
Kuwepo kwa mafanikio haya kumetokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya wazazi na wadau mbalimbali wa elimu ikiwemo Serikali ya awamu ya tano ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo mdau namba moja katika kufanikisha zoezi hili muhimu la kuwapatia elimu watoto wa Kitanzania bila kujali tofauti za kijinsia,maumbile wala maeneo mtoto anapotoka.
Katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tano (2015 hadi sasa 2019) tumeshuhudia ongezeko kubwa la wanafunzi wenye mahitaji maalum wakipelekwa mashuleni na wazazi pamoja na walezi wao, hii imetokana na Sera nzuri ya Serikali ya awamu ya Tano ya utoaji wa elimu bila malipo katika shule zote za Serikali kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya kidato cha nne.
Watoto wenye mahitaji maalum wakishiriki zoezi la upandaji wa Miti katika eneo la shule ya Msingi Sanya Juu tarehe 2.4.2019

Watoto wa  darasa la Nne na Tatu katika shule ya Msingi Sanya Juu wakifurahia kushiriki katika maazimisho ya siku ya Usonji Duniani tarehe 2.4.2019,ambapo Kiwilaya yalifanyika shule ya Msingi Sanya Juu.

Kupata ushauri uliotolewa kwa wazazi katika maazimisho hayo bofya 
1. Hapa

KINAPA WATOE MSAADA AJALI YA MOTO VISITATION GIRLS -SIHA

Mamlaka ya hifadhi ya mlima Kilimanjaro (KINAPA) leo tarehe 5.4.2019 wametoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana Visitation kutokana na janga la moto lililotokea hivi karibuni na kuunguza vifaa mbalimbali vya wanafunzi wa shule hiyo.
Akiwasilisha msaada huo kwa Mkuu wa shule hiyo,Mwakilishi wa hifadhi ya Taifa ya mlima Kilimanjaro KINAPA ndugu Elibariki Eliangilisa alieleza kuwa KINAPA wametoa vifaa mbalimbali kwa wanafunzi wa shule hiyo  vyenye thamani ya shilingi milioni 2 ikiwa ni sehemu ya mchango wao kama wadau wakubwa wa elimu na lengo likiwa ni  kuwapa pole wanafunzi waliopoteza vifaa vyao wakati wa janga la moto.
Alieleza kuwa msaada walioutoa ni juhudi za Mhe. Onesmo Buswelu Mkuu wa Wilaya ya Siha ambaye aliwashirikisha kuhusu tukio la wanafunzi wa shule ya Wasichana Visitation kupoteza vifaa vyao mara baada ya tukio la moto kutokea katika bweni moja la wanafunzi,ambapo taarifa zinasemekana kuwa huenda ilitokana na hitilafu ya umeme,tunashukuru Mungu kuwa katika tukio hilo hakana madhara yoyote ya mwanafunzi kupata madhara bali ni vifaa tu ndio vilivyoteketea kwa moto.
“Naomba mpokee msaada wetu mdogo kwenu uwe kama chachu ya kuendelea kudumisha mahusiano yetu kama wahifadhi wa mlima na jamii ya watu wa Kilimanjaro” alisema Elibariki
Miongoni mwa vifaa vilivyokabidhiwa kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Visitation na Mwakilishi wa KINAPA kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ni pamoja na mashuka 100,Madaftari 150,Kalamu boksi 10, pamoja na vifaa vingine vingi vitakavyowezesha wanafunzi kujikimu


Wanafunzi wa shule ya wasichana Visitation  leo tarehe 5.4.2019 wakipokea msaada wa vifaa mbalimbali vilivyotolewa na mamlaka ya hifadhi ya mlima Kilimanjaro (KINAPA)
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Visitation wakishiriki katika kupokea vifaa mbalimbali vya msaada vilivyotolewa na mamlaka ya hifadhi ya Taifa ya mlima Kilimanjaro
wanafunzi wa shule ya wasichana Visitation wakishuhudia vifaa mbalimbali vya msaada vilikabidhiwa shuleni hapo na mwakilishi wa KINAPA

Vifaa mbalimbali vya msaada  vilivyotolewa na hifadhi ya Taifa ya mlima Kilimanjaro vikishushwa katika gari ,huku wanafunzi wa shule ya Visitation wakifurahia

WANANCHI SIHA MAGHARIBI WAFURAHIA BARABARA YA LAMI

Wananchi wa Tarafa ya Siha Magharibi wameendelea kupata mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano kutokana na kuunganishwa na barabara kiwango cha lami inayotoka Sanya Juu kupitia Ngarenairobi hadi Elerai. Barabara hiyo inayotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni mara baada ya ujenzi  wake kukamilika muda wowote kuanzia sasa.
Kwa pamoja Madiwani wanaotoka katika Kata za Ngarenairobi,Ndumet na Mitimirefu wameeleza  kufurahishwa na utendaji kazi  uliotukuka wa Mhe  Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa kwa kuwajengea barabara bora na ya kisasa kwa kiwango cha Lami. 
Akielezea ujenzi huo Diwani wa Kata ya Ndumeti Mhe. Jackson Rabo amesema kuwa Wananchi wa Kata yake wanampongeza Rais Magufuli kwa jinsi alivyofanikisha ujenzi huo ambao ulishindikana katika awamu zote zilizopita lakini umewezekana katika Serikali ya  awamu hii ya tano. Sisi kama wananchi hatuna cha kumpa Mhe. Rais wetu bali tutazidi kumwombea Mungu ili azidi kumpa nguvu na maisha marefu zaidi.  
Kujengwa kwa barabara hiyo kumeanza kuongeza msafara mkubwa wa Watalii wanaopita barabara hiyo kupanda mlima  Kilimanjaro kupitia lango la Londrosi . kwa upande wa mazao ya chakula  kama vile viazi mviringo,karoti,Maharage,ngano,na aina mbalimbali za mboga yanayopatikana kwa wingi katika eneo la West Kilimanjaro na kusafirishwa katika mikoa ya Arusha,Tanga,Dar es salaam na Nchi jirani ya Kenya yanasafirshwa kwa urahisi kwa sasa kutokana na sehemu kubwa ya  ujenzi wa barabara hiyo kukamilika . 
Kujengwa kwa barabara hii kumetokana na juhudi za  Serikali ya awamu ya tano za kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo mengi ya Nchi ya Tanzania ikiwemo Wilaya ya Siha. Kwa mara ya kwanza tangu Uhuru ya Tanzania upatikane mwaka 1961 wananchi wameshuhudia kujengwa kwa barabara ya lami kutoka Sanya Juu  hadi Ngarenairobi kuelekea Elerai yenye jumla ya Kilomita 32.3 kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bil 52.3 kutoka Serikali ya Tanzania.
BARABARA YA LAMI WEST INAVYOONEKANA PICHANI HAPA CHINI
Muonekano wa barabara hiyo karibu na Makao Makuu ya Halmashauri ya Siha
Muonekano wa barabara mpya ya lami kuelekea West Kilimanjaro hapa ni eneo la karibu na barabara ya NARCO
kipande cha barabara hii kuelekea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Siha kama inavyoonekana pichani hapo juu
Ubora wa barabara hii karibu na barabara inayoelekea TALIRI

SANYA JUU SEKONDARI WAPEWA TUZO MCHEZO WA BASEBALL

Timu ya shule ya Sekondari Sanya Juu(Sanya Day) Kata ya Nasai  kwa mchezo wa Baseball wamepewa tuzo ya heshima baada ya kufanikiwa kushika nafasi ya pili ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa shule za Sekondari mwishoni mwa mwaka 2018.
Tuzo hiyo imetolewa na Mhe. Anna Mghwira Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro alipokuwa katika maazimisho ya juma la elimu mkoa wa Kilimanjaro lililofanyika tarehe 11.4.2019 katika uwanja wa mashujaa mjini Moshi ambapo Halmashauri zote Saba za Mkoa wa Kilimanjaro zimeshiriki kikamilifu na kuonesha mafanikio makubwa.
Katiba hotuba yake fupi ya ufunguzi wa wiki ya elimu mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Mkuu wa Mkoa alieleza kufurahishwa na mafanikio ya kitaaluma yaliyopatikana katika mkoa wa kilimanjaro kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ambapo mkoa umeshika nafasi za juu kimasomo na kimichezo pia.
Alieleza kuwa kipekee naipongeza shule ya Sanya Juu Sekondari kwa kufanikiwa kushika nafasi ya pili Kitaifa mwaka 2018 katika mchezo wa Baseball. Nimeambiwa kuwa mwaka 2017 ndio mlikuwa mabingwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mchezo huu, ambapo mlituletea heshima kubwa mkoa wa Kilimanjaro pamoja na Wilaya ya Siha
Katika utoaji wa tuzo hiyo jumla ya wanafunzi 10 na walimu wawili walioleta heshima Mkoa wa Kilimanjaro  walivalishwa nishani kila mmoja mbele ya umati mkubwa wa watu waliofurika kwa wingi katika uwanja wa mashujaa mjini Moshi.
Shule ya Sekondari Sanya Juu ipo Wilaya ya Siha na inawanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita huku wanafunzi wa kidato cha 5 na 6 wakiwa wanasoma masomo ya Sayansi pekee(PCM,PCB,PGM na CBG).
wachezaji wa Timu ya Baseball Sanya Juu Sekondari wakivalishwa nishani na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ktk kilele cha juma la elimu uwanja wa mashujaa Moshi

Cheti cha Pongezi kilichotolewa kwa shule ya Sanya Juu Sekondari
Mkuu wa Shule ya Sanya Juu Mwl Elieta Kaaya akipokea cheti za pongezi kwa niaba ya timu hiyo na uongozi mzima wa shule

Wanafunzi wachezaji  wa Walimu wakifurahi mara baada ya kuitwa kuchukua zawadi zao mbele ya mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro
Mwalimu wa mchezo wa Baseball Sanya juu Sec mwl Nuiya Ally akipokea zawadi yake kutoka kwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro

WANAWAKE WILAYA YA SIHA WAPATIWA MIL 59

Halmashauri ya Wilaya ya Siha Mkoa wa Kilimanjaro imetoa mikopo kwa vikundi 20 vya Wanawake yenye thamani ya shilingi milioni 59
Zoezi la utoaji wa mikopo limefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha tarehe 16.4.2019 ambapo Kaimu mkuu wa Wilaya ya Siha mhe. Agnes Hokororo ambaye pia ni mkuu wa Wilaya ya Rombo alikuwa mgeni rasmi katika Zoezi hilo. 
Katika hotuba yake mhe. Hokororo Alitoa pongezi nyingi kwa halmashauri ya Siha kwa kupata mafanikio makubwa katika utoaji wa mikopo kwa vikundi vya Wanawake.
Napenda kuwaasa kinamama wa Wilaya ya Siha kuendelea kudumisha umoja wenu katika kuendeleza vikundi mlivyonavyo huku Serikali kupitia halmashauri itaendelea kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu alisema Mhe. Hokororo
Pia mhe. Hokororo alitoa wito kwa halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa,  inatoa mikopo kwa watu wenye ulemavu bila kusahau vikundi vya vijana kama ilivyo agizo la Serikali yetu.
Akizungumza kabla ya utoaji wa mikopo hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha ndugu Valerian Juwal ,alieleza kuwa mikopo inayotolewa kwa vikundi 20 vya Wanawake itawanufaisha  zaidi ya  watu 479 ndani ya Wilaya ya Siha.  Leo tunawapatia vikundi 19 kila kimoja shilingi milioni 3 na kikundi kimoja kinapata shilingi milioni 2 alisema Juwal
Alieleza kuwa kwa miaka miwili iliyopita (2016/2017 & 2017/2018) Halmashauri ya Wilaya ya  Siha imekuwa ikipata tuzo kwa kuwa miongoni mwa Halmashauri za mfano hapa Tanzania kwa kutoa mikopo kwa kiwango kikubwa.
”Napaenda kueleza kuwa katika mwaka huu wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Siha imedhamiria kushika nafasi za juu kabisa miongoni mwa Halmashauri zitakazofanikiwa kutoa mikopo kwa wingi  kwa vikundi vya  Wanawake” alisema Juwal.
Utoaji wa mikopo kwa wanawake katika Halmashauri hapa nchini ni utekelezaji wa agizo la Serikali ya awamu ya tano kuwa ,asilimia 4 za mapato ya ndani ya kila Halmashauri zitolewe kama mikopo kwa Wanawake,asilimia 4 mikopo kwa vijana na asilimia 2 itolewe kama mikopo kwa watu wenye ulemavu.
Baadhi ya Wanawake waliopatiwa mikopo wakiwa  katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha wakifurahia zoezi la utoaji wa mikopo

Wah. Madiwani wanawake Halmashauri ya Siha wakishuhudia zoezi la utoaji wa mikopo kwa vikundi 20 vya wanawake,zoezi lilifanyika tarehe 16.4.2019 ktk ukumbi wa Halmashauri ya Siha

Mkurugenzi Mtendaji H/W Siha ndugu Valerian Juwal (kulia) akisoma orodha ya vikundi 20  vya wanawake vilivyopatiwa mikopo ya shilingi Mil.59  na Halmashauri ya Siha