Monday 27 February 2017

TAARIFA YA MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA SIHA BARAZA LA MADIWANI TAREHE 24.2.2017





OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
HALMASHAURI YA WILAYA YA SIHA


TAARIFA YA MWENYEKITI  WA HALMASHAURI   MKUTANO  WA KAWAIDA WA  BARAZA LA MADIWANI  KATIKA KIPINDI CHA ROBO YA PILI (OKTOBA -DESEMBA,2016).
v  Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Siha,
v  Mwakilishi Ofisi ya RAS-Mkoa wa Kilimanjaro,
v  Mh. Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Siha,
v  Mh. Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Siha,
v  Waheshimiwa Madiwani,
v  Mkurugenzi Halmashauri ya Siha,
v  Viongozi wa Dini,
v  Wageni Waalikwa,
v  Ndugu Wataalamu,
v  Waandishi wa Habari,
v  Wananchi wa Wilaya ya Siha,
v  Mabibi na Mabwana,

Wasalaam Alekumu,Tumsifu Yesu Kristo,Bwana Yesu asifiwe


  
Wah. Madiwani ,  na Ndugu  Wananchi;
Naomba tusimame kwa dk moja ili kuwakumbuka wale wote waliopoteza maisha katika kipindi cha mwisho wa  mwaka 2016 na hasa mwenzetu Mheshimiwa Anna A Masaki diwani wa viti maalum (W) alifariki mapema mwaka huu 2017
Habarini za mwaka mpya 2017, ni matumaini yangu kuwa mmevuka mwaka salama na wote mnaendelea na majukumu yenu  ya kuwatumikia wananchi kama kawaida.

 (1)UTUNZAJI WA CHAKULA
Waheshimiwa Madiwani na ndugu Wananchi.
Napenda kuwaomba na kuwakumbusha tena Wananchi wa Halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa tunakuwa na tabia ya kutunza chakula kilichopo kwani hali ya hewa kama mnavyoiona kuwa siyo nzuri sana  hasa baada ya mvua ya vuli kukosekana. Mimi kama mwenyekiti wa Halmashauri ya Siha napenda kutoa rai kwa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wengine katika ngazi za Kata na Vijiji tushirikiane kwa pamoja kuwaelimisha wananchi kuhusu elimu ya utunzaji wa chakula hasa katika ngazi ya Kaya na Vijiji. Pia nawaomba viongozi wa Madhehebu ya Dini tushirikiane kwa pamoja katika kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa  utunzaji na uhifadhi wa chakula . Kipekee namshukuru Mkuu wetu wa Wilaya ya Siha kwa kuweka agizo la kuzuia matumizi ya mahindi katika kutengenezea pombe za kienyeji hasa Dadii(nzuga) kama sehemu ya kunusuru matumizi ya nafaka yasiyo ya  lazima.

(2)UKUSANYAJI WA MAPATO
Waheshimiwa Madiwani,
Pamoja na Halmashauri yetu kukabiliwa na tatizo ya vyanzo vichache na vya kudumu vya mapato yake ya ndani, Halmashauri imeendelea kukusanya mapato yake ya ndani kwa kutumia  Vijiji vilivyopo katika maeneo yenye  vyanzo vya mapato na kwa kutumia mashine za kieletroniki kukusanya mapato hayo kama ilivyoagizo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Hata hivyo Halmashauri ya Siha bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa vyanzo vya uhakika na  vya kudumu vya  mapato hali ambayo inatufanya sisi sote kama viongozi kuendelea kubuni vyanzo mbadala vya kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri yetu.

(3) UTUNZAJI WA MAZINGIRA
Waheshimiwa Madiwani,ndg  Wananchi na Wataalam.
Ndugu zangu hali ya ukame mnayoiona katika Wilaya yetu imetokana na  shughuli za kibinadamu zilizosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira. Ili kunusuru hali hii isiendelee katika maeneo yetu ya Wilaya ya Siha, naomba kutoa mapendekezo ya kila kaya kuotesha angalau miti 5 kila mwaka na kama inawezekana tuweke kwenye sheria ndogo za Halmashauri ambazo zitamtaka kila mwenye eneo la ardhi kuotesha miti ya kutosha kulingana na ukubwa wa eneo lake. Kwa hili naomba kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa Watendaji wa Kata na Vijiji katika Halmashauri ya Siha  kupitia vikao vya Vijiji na Vitongoji wanawaelimisha wananchi kuhusu upandaji wa miti katika maeneo yao. Pia wenye mashamba makubwa tutafanya utaratibu wa kuwaomba waotesha miti angalau 500 kila mwaka ili kunusuru Wilaya ya Siha kugeuka kuwa jangwa.
Aidha, najua adui mkubwa wa miti ni mifugo,naomba wote kwa pamoja tusaidiane kulinda mifugo  yetu ili isiharibu miti tunayopanda kila mwaka. 

 (4) MIFUGO KUTOKA NJE YA WILAYA
Waheshimiwa Madiwani,Ndugu Wananchi;
 Naomba kutoa agizo kwa Viongozi wa Vijiji na Kata hasa watendaji wa Vijiji kuhakikisha kuwa hakuna mifugo inayoingia ndani ya vijiji na kata zetu kutoka Wilaya au mikoa jirani. Kimsingi  mifugo hii inasababisha kuongezeka kwa uharibifu wa mazingira Wilayani Siha na kusababisha kuongezeka kwa magonjwa ya mifugo kwa  mifugo yetu,mfano mzuri ni ugonjwa hatari wa kimeta ambao kimsingi umetoka nje ya Wilaya yetu.naomba viongozi wenzangu tusaidiane kulisimamia hili na pale inapopatikana mifugo kutoka nje ya maeneo yetu basi hatua za kisheria zichukuliwe hasa za kutoza faini stahili kulingana na sheria zilizopo  ili kuongeza mapato ya Halmashauri. Ofisi yangu inamwomba Mkuu wa Wilaya ya Siha kutusaidia jambo hili kwani wakati mwingine litahitaji nguvu za dola katika kulitekeleza ipasavyo.

(5) UTUNZAJI WA BARABARA
Waheshimiwa Madiwani,Ndugu Wananchi;
 Naomba tena kuwakumbusha wananchi wa  Halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa kila mmoja anashiriki kikamilifu katika  kuzitunza barabara zilizojengwa na Serikali katika Kata na Vijiji vyetu. Serikali inatoa pesa nyingi kutengeneza barabara hizo ambazo zimeanza kuharibiwa na baadhi ya watu kwa kuzikata kwa kupitisha mifereji au mabomba bila kibali cha Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji. Naomba Mkurugenzi uwaagize watendaji wako wa Kata na Vijiji kwa kushirikiana na Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji kulisimamia agizo hili  kwa ukaribu zaidi. Naomba kutoa agizo kuwa kuanzia sasa ni marufuku kwa mtu yeyote  kukata barabara bila kibali cha Mkurugenzi Mtendaji  na yeyote atakayekiuka hilo achukuliwe hatua ili iwe fundisho kwa wenzake.

(6)UWAJIBIKAJI KAZINI
Waheshimiwa Madiwani,Ndugu Wananchi;
Napenda kuwakumbusha tena Watumishi wa Serikali waliopo Wilaya ya Siha kuwa Serikali ya awamu ya tano imeshasema kuwa haitawavumilia watumishi wazembe na wabadhirifu kazini. Naomba kila mtumishi atimize wajibu wake kwa mujibu wa taaluma aliyosomea na kwa kufuata sheria na taratibu za utumishi wa Umma. 

Aidha ,naomba kuwakumbusha tena wazazi/walezi kuwa shule za msingi na sekondari zimeshafunguliwa  tangu mwezi wa Januari,2017 na wajibu wao  ni kuhakikisha kuwa watoto wote wanakwenda shuleni na ni jukumu lao  kuwawezesha watoto wao  kupata chakula mashuleni. Naomba viongozi wote tushirikiane  kuwaelimishe wazazi/walezi ili kutimiza majukumu ya kuwapatia mahitaji muhimu watoto wao hasa mlo wa mchana.Elimu ni ufunguo wa maisha kila  mtu atimize wajibu wake.
Waheshimiwa  Madiwani na ndg Wananchi;
Kabla ya kufika mwisho wa Taarifa yangu, napenda  kuwashukuru tena Wananchi wa Wilaya ya  Siha na Waheshimiwa Madiwani  kwa ushirikiano  wenu wa dhati mnaoendelea kunipatia kwa ajili ya kutekeleza majukumu yangu ya Kila siku. Naomba kuchukua fursa hii kuwahimiza wananchi wa Siha kujiandaa vema na msimu mkubwa wa mvua za masika ambao  tumezoea unaanza mwezi Machi kila mwaka. Naomba wote kwa umoja wetu tufanye kazi kwa bidii kwa maendeleo ya Familia zetu , Wilaya ya Siha na Taifa kwa ujumla wake.
Mwisho ,nichukue fursa hii kwa niaba ya baraza la Madiwani, kuwashukuru tena kwa usikivu wenu mkubwa mlionesha tangu mwanzo wa taarifa yangu, naomba usikivu na utulivu huu uendelee hadi mwisho wa mkutano wetu na hatimaye tumalize na kuagana kwa upendo na furaha. Aidha,Napenda kuishukuru tena Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Siha kwa ushirikiano mzuri hasa wa kuhamasisha shughuli za maendeleo katika Wilaya yetu
Asanteni sana kwa kunisikiliza
Imetolewa na:
Frank K. Tarimo
Mwenyekiti wa Halmashauri (W)
SIHA
 Tarehe 24.2.2017

Friday 24 February 2017

Mkutano wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Siha unafanyika leo tar 24.2.2017

 Mkutano wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Siha unaendelea katika ukumbi wa mikutano ya Halmashauri ya Siha. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Siha Mhe.Frank Tarimo akitoa taarifa  yake kwa wajumbe.
 Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Onesmo Buswelu akiongea na Madiwani ktk Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya  Siha leo ijumaa
Wajumbe wa mkutano wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Siha unaendelea katika ukumbi wa mikutano Halmashauri ya Siha.

Thursday 23 February 2017

Uboreshaji wa Elimu Wilayani Siha

 Wanafunzi na wazazi wa shule wa shule ya Msingi Lemosho wakifurahia kufunguliwa kwa madarasa matatu mapya katika Shule hiyo. ufunguzi huo umefanywa leo na mhe. Onesmo Buswelu Mkuu wa Wilaya ya Siha .Shule ya msingi Lemosho ina jumla ya wanafunzi 1082
Wanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Lemosho wakimwonyesha mhe Onesmo Buswelu Mkuu wa Wilaya ya Siha umahiri wao katika suala la taaluma shuleni hapo.

Picha za matukio ya ufunguzi wa madarasa matatu shule ya msingi Lemosho - Tarafa ya Siha Magharibi

 Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe: Onesmo Buswelu akiwa na wanafunzi wa darasa la kwanza katika moja ya madarasa aliyoyafungua Mkuu huyo wa Wilaya ya Siha.tukio hilo limefanyika leo alasiri
 Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe.Onesmo Buswelu akimfuatilia kwa makini mwanafunzi ya darasa la kwanza akifanya moja ya mazoezi ya darasa  katika moja ya madarasa aliyoyafungua leo katika Shule ya msingi Lemosho

 Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe Onesmo Buswelu akikata utepe katika madarasa matatu aliyoyazindua leo katika Shule ya msingi Lemosho Tarafa ya Siha Magharibi

 Mkuu wa Wilaya ya Siha akiongea na wananchi na jumuia ya shule ya msingi Lemosho. Mkuu huyo wa Wilaya alifungua madarasa matatu na kuagiza madarasa hayo kuanza kutumika mara moja na wanafunzi wa shule hiyo ili kupunguza msongamano wa wanafunzi  madarasani.
 Wanafunzi wa shule ya msingi Lemosho wakifurahia kufunguliwa kwa madarasa matatu ya shule hiyo,ambazo ufunguzi ulifanywa na mhe Onesmo Buswelu Mkuu wa Wilaya ya Siha.
 Wazazi na wanafunzi wa shule ya msingi Lemosho wakimpokea kwa Shangwe Mkuu wa Wilaya ya Siha alipofika katika Shule hiyo ili kufungua madarasa matatu mapya  ya shule hiyo.
Madarasa  matatu mapya ya shule ya msingi Lemosho yaliyofunguliwa leo na Mhe. Onesmo Buswelu Mkuu wa Wilaya ya Siha .madarasa haya yamejengwa kwa ushirikiano wa Serikali,nguvu za wananchi ,Wahisani na wadau wa Elimu.

Monday 20 February 2017

Asilimia 100 ya wanafunzi waliofaulu darasa la saba 2016 wachaguliwa kuendelea na Elimu ya Sekondari Wilayani Siha-Kilimanjaro

Jumla ya wanafunzi 2264 walisajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba kati yao wavulana walikuwa 1045 na wasichana 1219 sawa na asilimia 90.1 ya walioandikishwa mwaka 2010.

Jumla ya wanafunzi 2250 walifanya mtihani wa kumaliza Elimu ya msingi Wilayani Siha mwaka 2016 katika Shule za msingi 55 zenye wanafunzi wa darasa la saba. Kati ya wanafunzi waliofanya mtihani wavulana walikuwa 1037 na Wasichana walikuwa 1213 sawa na asilimia 99.38 ya walioandikishwa kufanya mtihani huo.

Aidha,katika mtihani huo jumla ya wanafunzi 1641 kati yao wavulana 729 na wasichana 912 waliofaulu kwa kiwango cha daraja A- C ambapo ni sawa na asilimia 72.93 ya waliofanya mtihani huo.

Wanafunzi wote 1641, kati yao 729 wavulana na 912  wasichana waliofaulu walichaguliwa kujiunga na masomo ya Elimu ya Sekondari katika shule za kutwa na Bweni ndani na Nje ya Wilaya ya Siha,hii ni sawa na asilimia 100 ya waliofaulu walipata nafasi ya kuchaguliwa katika Shule za Serikali.

Wastani wa Ufaulu kwa matokeo ya Darasa la saba mwaka 2016 ni 72.93 na masomo yaliyoongoza kwa ufaulu ni pamoja na  Sayansi (80%), Maarifa ya jamii(78.5),Kiswahili (77%),Kiingereza(40.2%), na somo la mwisho kwa ufaulu ni Hisabati (39.2%)

Tangazo la mkutano wa Baraza la Madiwani Halmashauri Wilaya ya SIHA- Kilimanjaro

HALMASHAURI YA WILAYA YA SIHA
TANGAZO LA MKUTANO WA BARAZA LA MADIWANI

MKURUGENZI MTENDAJI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA  SIHA  MKOA WA KILIMANJARO ANAWATANGAZIA WANANCHI NA WAKAZI WOTE WA WILAYA YA SIHA KUWA,KUTAKUWA NA MKUTANO WA KAWAIDA WA  BARAZA LA MADIWANI SIKU YA ALHAMIS TAREHE 23/02/2017 NA  SIKU YA IJUMAA TAREHE 24/02/2017.

MKUTANO HUO  WA BARAZA LA MADIWANI NI KWA AJILI YA KUPITIA TAARIFA MBALIMBALI ZA UENDESHAJI WA HALMASHAURI KWA KIPINDI CHA ROBO YA PILI YA MWAKA WA FEDHA 2016/2017.

AIDHA, MKUTANO UTAFANYIKA KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA HALMASHAURI YA SIHA MUDA KUANZIA SAA 4:00 ASUBUHI.

WANANCHI NA WAKAZI WOTE  WA SIHA MNAKARIBISHWA.


Limetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano(W)
                                                       SIHA
                                             Tarehe 20.02.2017

Friday 17 February 2017

UFAULU KIDATO CHA TANO NA SITA WAFIKIA ZAIDI ASILIMIA 99 MWAKA 2016 WILAYANI SIHA



Ufaulu wa wanafunzi katika Shule za Sekondari za kidato cha 5 na 6 wafikia zaidi ya asilimia 99 katika mwaka wa 2016 Wilayani Siha.

Wilaya ya Siha imeweka inazo jumla ya Sekondari nne za wanafunzi wa kidato cha tano na sita na wanafunzi wa shule hizo wanasoma masomo ya Sanaa na Sayansi.

Shule zenye kidato cha tano na sita Wilaya ya Siha ni kama ifuatavyo-:
1.Nuru Sekondari
2.Magadini Sekondari
3.Sanya Juu Sekondari
4.Oshara Sekondari

Picha za watumishi wa Umma Wilaya ya Siha wakishiriki katika michezo mbalimbali


Watumishi wa idara ya Afya Halmashauri ya Wilaya ya Siha wakishiriki katika mchezo wa kuvuta kamba hivi karibuni

Watumishi ofisi ya Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya Siha wakishiriki katika mchezo wa kuvuta kamba


Watumishi wa Serikali Idara ya Afya wakishiriki vema mchezo wa kuvuta kamba.wanawake wanashiriki vema katika michezo mbalimbali Wilayani siha


Watumishi wa Umma Wilaya ya Siha wakishiriki Mchezo wa riadha ,hii ni katika Hali ya kutunza na kuboresha afya ya mwili na akili pia. 

Miongoni mwa Timu ya mpira wa Pete ya watumishi Wilaya ya siha ikifanya mazoezi hivi karibuni
Watumishi wa Umma wakishiriki mchezo wa kukimbia kwa gunia .mchezo huu ni kivutio kikubwa kwa watazamaji

Thursday 16 February 2017

TAMBUA KIASI CHA PEMBEJEO ZA RUZUKU ILICHOPATA WILAYA YA SIHA MSIMU 2016/2017

Katika msimu wa mwaka 2016/2017 Wilaya ya Siha imekuwa miongoni mwa Wilaya 141 hapa Nchini Tanzania zilizonufaika na Pembejeo za Ruzuku ya Kilimo.
Kiasi ilichopata Wilaya ya Siha katika pembejeo hizo ni kama ifuatavyo-:

1. Mbegu za mahindi tani 10.8  ambayo ni  sawa na kilo 10800
2.Mbolea ya kupandia tani 39.3 ambayo ni sawa na mifuko 786 ya kilo 50 kila moja
3.mbolea ya kukuzia tani 53.98 ambayo ni  sawa na mifuko 1080 ya kilo 50 kila moja  

BEI ELEKEZI YA PEMBEJEO ZA RUZUKU MSIMU 2016/2017 WILAYA YA SIHA-KILIMANJARO

  AINA YA PEMBEJEO.                                            KIASI.                  .             BEI   (TSH)  

 1.Mbegu bora ya mahindi Chotara.                     Kilo 10.                            47,000/=
 2.Mbegu Bora ya Mahindi Mchanganyiko.        Kilo 10.                             29,500/)=
3.Mbolea ya Kupandia (DAP).                                Kilo 50.                            43,000/=
 4.Mbolea ya kukuzia (UREA).                                 Kilo 50.                             31,000/=


NB: Fidia ya Ruzuku inayotolewa na Serikali imepungua kutoka asilimia 50% mwaka 2015/2016 hadi asilimia 30% mwaka 2016/2017.

Kamati ya pembejeo za Kilimo Vijiji vyote Wilayani Siha yafanya kikao kufanikisha zoezi la ugawaji wa Ruzuku mwaka 2016/2017

Katibu Tawala Wilaya ya Siha Mhe. Nicodemus Bei kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Siha akifungua kikao cha kamati ya pembejeo ya kilimo  kwa Vijiji vya Wilaya ya  Siha. Viongozi  wa kamati za vijiji ni wenyeviti na makatibu waliochaguliwa na kuidhinishwa na mikutano mikuu ya Kila kijiji Wilayani Siha. Siha inajumla ya Vijiji 60 vyenye Wajumbe 6 kwa kila kijiji  wenye majukumu ya kusimamia ugawaji wa Ruzuku za pembejeo za Kilimo





Wajumbe wa kusimamia pembejeo za Ruzuku katika vijiji 60 Wilayani Siha wakimsikiliza Katibu Tawala wa Wilaya ya Siha wakati akitoa neno la ufunguzi katika kikao cha ugawaji wa Ruzuku za Kilimo kwa mwaka 2016/2017. Kikao hicho kinaendelea katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha leo tarehe 16.2.2017

Wednesday 15 February 2017

Halmashauri ya Siha yaagizwa kutoa 5% Mapato ya Ndani kwa VIJANA NA WANAWAKE

Mkuu wa Wilaya ya Siha mheshimiwa Onesmo Buswelu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa asilimia 5 ya Mapato ya ndani ya Halmashauri ya Siha zinatengwa kwa ajili ya mikopo ya vijana na wanawake.

Mkuu wa Wilaya ameyasema hayo wakati akipitia taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kipindi cha mwezi Julai 2016 hadi mwezi Desemba 2016

Alieleza kuwa Halmashauri ya Siha kama zilivyo Halmashauri nyingine hapa Nchini ni lazima ihakikishe kuwa inatekeleza agizo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutenga asilimia tano ya Mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa vijana na Wanawake.

Alieleza kuwa ni mategemeo yake kuona kuwa asilimia hizo tano zinatengwa na kutolewa kwa wahusika kwa wakati ili mradi tu taratibu zote zifuatwe kwa kuzingatia Sheria na miongozo ya Serikali.

Hadi kufikia mwezi Desemba mwaka 2016 zaidi ya Shilingi milioni 40 fedha za Mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Siha  zimetolewa kama mikopo kwa vijana na wanawake

WANAOWAPA WANAFUNZI MIMBA SASA KUKIONA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha Valerian Juwal amewaonya wale wote watakaowasababishia MIMBA wanafunzi katika Shule za MSINGI na sekondari Wilayani siha watachukuliwa hatua kali za kinidhamu bila kujali vyeo,nafasi zao wala mahali wanaosoma.

Mkurugenzi huyo aliyasema hayo wakati akiongea na wadau wa Elimu Wilayani siha hivi karibuni kwa lengo la kujadili maendeleo na ustawi wa Elimu katika jamii ya wanaSiha.

Alisema mbali na changamoto nyingine zilizopo ambazo kimsingi zinasababisha kudorora na kushusha kiwango cha Elimu ni tatizo la baadhi ya watu kuwarubuni watoto na kuwasababishia mimba ambazo zinawakatiza watoto hao wasiendelee na masomo.

Aliwaagiza wakuu wa Shule zote za Sekondari na walimu wakuu wa shule za msingi kuhakikisha kuwa wanawachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaosababisha mimba kwa wanafunzi.

Aliwataka walimu hao wakuu na wakuu wa Shule Wilayani siha kushirikiana na watendaji wa vijiji na Kata ili kufanikisha agizo hilo MUHIMU kwa maendeleo ya Wilaya ya Siha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Siha aliongeza kuwa hata wazazi wataonyesha wanaungana na waalifu hao pia wachukuliwe hatua za kisheria.

Wanafunzi 16 wa shule za msingi na Sekondari Wilayani Siha  walipata mimba kwa mwaka 2016 na kusababisha wanafunzi hao kukatiza ndoto zao za maisha.

Mkurugenzi akitoa wito kwa wazazi na walezi kuunga mkono jitihada za Serikali Wilayani Siha za kuhakikisha kuwa tatizo la mimba kwa wanafunzi linapungua na hatimaye baada ya muda mfupi libakie kama historia katika Shule zetu zote za msingi na Sekondari.

Watumishi wa Umma Wilayani Siha watakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea

Mkuu wa Wilaya ya Siha mhe:Onesmo Buswelu amewataka watumishi wa Umma ndani ya Wilaya ya Siha kufanya kazi kwa bidii na kuachana na mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea

Hayo yamesemwa  na Mkuu huyo wa Wilaya ya Siha leo tar 15.2.2017 wakati akijadili na kupitia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi wa Chama Tawala alipokuwa katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha.

Alieleza kuwa muda wa kufanya kazi kwa mazoea Sasa umefika mwisho wake na kuwataka watumishi kubadilika na kuwatumikia wananchi na wakazi wa Siha kwa nguvu na juhudi zaidi ili kutimiza malengo yaliyowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alieleza kuwa ,Serikali inawategemea watumishi wa Umma kwa kuzingatia kuwa wapo katika ujuzi na maarifa mbalimbali yanayoweza kutoa huduma bora kwa JAMII na siyo bora huduma.

"Nawaombeni tena kama nilivokuwa nawataka mara zote kuwa,kila mtumishi katika idara yake aone namna gani anaweza kufanikisha utoaji wa huduma nzuri kwa maendeleo ya Siha na wakazi wake,aliongeza Mkuu wa Wilaya"

Mkuu wa Wilaya mhe. Onesmo Buswelu aliwataka pia watumishi wa Umma kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma kama misingi ya utawala bora inavyoeleza.


Sunday 5 February 2017

Matokeo ya mtihani wa Taifa darasa la nne 2016 Siha yafanyika Kweli,tazama taarifa zaidi hapa

Nafasi ya Halmashauri ya Wilaya ya Siha matokeo ya UPIMAJI mtihani wa Taifa Darasa la Nne mwaka 2016 haya hapa:

1. HAI - nafasi ya kwanza mkoa wa KILIMANJARO,nafasi ya (9/184) kitaifa
2. MOSHI MANISPAA- nafasi ya pili mkoa wa KILIMANJARO,nafasi ya (11/184) Kitaifa
3. SIHA- nafasi ya tatu mkoa wa KILIMANJARO ,nafasi ya (18/184) Kitaifa
4. ROMBO- nafasi ya Nne mkoa wa KILIMANJARO, nafasi ya (28/184) Kitaifa
5.SAME- nafasi ya Nne mkoa wa KILIMANJARO, nafasi ya (37/184) Kitaifa
6. MOSHI VIJIJINI - nafasi ya sita mkoa wa KILIMANJARO,nafasi ya (40/184) Kitaifa
7.MWANGA- nafasi ya 7 mkoa wa KILIMANJARO,nafasi ya (41/184) Kitaifa

Saturday 4 February 2017

Tambua Nafasi ya Halmashauri ya Wilaya ya Siha matokeo kidato cha nne 2016.

NAFASI YA HALMASHAURI YA  WILAYA YA SIHA  -KILIMANJARO MATOKEO KIDATO CHA NNE 2016


1.MOSHI VIJIJINI -nafasi ya kwanza mkoa wa KILIMANJARO,nafasi ya (13/178) Kitaifa
2.MOSHI MANISPAA- nafasi ya pili mkoa wa KILIMANJARO,nafasi ya (20/178) Kitaifa
3.MWANGA- nafasi ya tatu mkoa wa KILIMANJARO,nafasi ya (33/178) Kitaifa
4.HAI- nafasi ya nne mkoa wa KILIMANJARO,nafasi ya (38/178) Kitaifa
5. SIHA- nafasi ya tano mkoa wa KILIMANJARO,nafasi ya (40/178) Kitaifa
6.SAME- nafasi ya sita mkoa wa KILIMANJARO,nafasi ya (68/178) Kitaifa
7.ROMBO- nafasi ya saba mkoa wa Kilimanjaro,nafasi ya (69/178) Kitaifa

Siha yapata mjongeo chanya matokeo ya mtihani kidato cha nne 2016

Hatimaye kiwango cha ufaulu ktk  halmashauri ya Wilaya ya Siha Siha kimeimarika kwa shule zake za sekondari na kupanda kwa zaidi ya nafasi 40 katika nafasi za Halmashauri hapa Nchini.

Katika matokeo ya kidato cha nne Mwaka 2015 Halmashauri ya Siha ilishika nafasi ya 80 kati ya Halmashauri 178 zilizopo hapa Nchini. Matokeo yaliyotangazwa na baraza mtihani wa  kidato cha nne mwaka 2016 yanaonyesha kuwa Halmashauri ya Siha katika matokeo hayo imeshika nafasi ya 40 kati ya Halmashauri 178

Aidha,katika matokeo hayo  Halmashauri ya Wilaya ya Siha imeshika nafasi ya 5 katika mkoa wa KILIMANJARO na imefanikiwa kutoa mwanafunzi aliyeingia nafasi ya wanafunzi kumi bora Tanzania.

Pamoja na Wilaya ya Siha kutoa shule moja iliyoingia katika Shule kumi duni kitaifa, kiwango cha ufaulu kwa kulinganisha na Halmashauri ,Majaji na Miji kimeongezeka na nafasi ya Halmashauri imeimarika kwa mjongeo chanya.

Halmashauri ya Siha imejipanga kuendelea kuimarisha kiwango vya ufaulu katika Shule zake za sekondari katika matokeo yajayo ya kidato cha nne na sita