Thursday 20 July 2017

Mfumo wa kieletroniki wazinduliwa rasmi Hospital ya Wilaya ya Siha





Hatimaye hospital ya Wilaya ya siha yaanza kutumia mfumo mpya wa kieletroniki katika utoaji wa huduma za matibabu hospitalini hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Siha mhe Onesmo Buswelu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tukio hilo ,amezindua mfumo huo rasmi leo tarehe 20.7.2017 katika hospital ya wilaya ya siha na kuagiza mganga mkuu wa Hospital ya Wilaya kuhakikisha kuwa mfumo huo unatumika katika malengo yaliyokusudiwa.
Mhe Mkuu wa Wilaya ya Siha amewataka waganga na wauguzi katika hospital ya Wilaya na maeneo mengine wajitahidi kufanya kazi za kuwahudumia wananchi  kwa uadilifu na kuwaonya wale wachache wanaotumia kauli zisizofaa kwa wagonjwa kuwa siku zao zinahesabika.
Mimi nawaamini sana waganga na wauguzi waliopo katika zahanati na vituo vyote vya kutolea huduma katika wilaya ya siha kwani sijapata malalamiko mengi kuhusu lugha mbaya kwa wagonjwa mnaowahudumia,alisema Buswelu.
Mganga mkuu wa Hospital ya Wilaya ya Siha Dr Andrew Method alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa,mfumo uliozinduliwa umegharamiwa na halmashauri ya Wilaya ya Siha kwa kutumia mapato ya ndani na jumla ya shilingi milioni 15 zimetumika.
Alieleza kuwa kukamilika  kwa mfumo huo kutasaidia kuboresha huduma katika hospital ya wilaya ya siha hasa uhifadhi wa takwimu na kumbukumbu za wagonjwa na kuachana na mfumo wa hapo nyuma ambapo kumbukumbu za wagonjwa zilikuwa zinahifadhiwa katika mafaili  na majalada.
Pia mganga mkuu alisema faida nyingine ya mfumo ni pamoja na kuharakisha utoaji wa vipimo,kuonesha akiba ya madawa iliyopo na kusaidia katika ukusanyaji wa mapato yanayotokana na uchangiaji wa huduma kutoka kwa wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha Valerian Juwal alisema kuwa kuwekwa kwa mfumo wa kieletroniki katika hospital ya Wilaya ya Siha ni agizo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa, kila hospital ya wilaya ifunge na kutumia mfumo wa kieletroniki ifikapo Juni 30 2017.
Valerian Juwal Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Siha alimweleza mgeni rasmi kuwa,japo halmashauri yake inakusanya vyanzo vichache vya mapato lakini wamejibana hadi kufikia hatua za kupata fedha za kutimiza agizo la Serikali.


No comments:

Post a Comment