Tuesday 18 July 2017

Familia 18 zaathirika na Janga la Moto kijiji cha Ngarenairobi

Moto mkubwa ulizuka jana tarehe 17.07.2017 na kuteketeza makazi ya watu katika kijiji cha Ngarenairobi,kata ya Ngarenairobi tarafa ya Siha magharibi Wilaya ya Siha.

Taarifa za awali za kuzuka kwa moto huo zilipatikana kutoka uongozi wa Kijiji cha Ngarenairobi kupitia ofisa mtendaji wa kijiji  hicho ndugu Seif Mwigamba ilieleza kuwa moto huo ulizuka mnamo saa saba mchana na kuteketeza makazi ya familia 18 zenye wakazi 42

Mwenyekiti wa kijiji hicho Stanley Nkini alisema kuwa wananchi walishirikiana kwa pamoja kuuzima moto huo ambao ungeweza kuteketeza nyumba nyingi zilizokuwa katika eneo hilo.

Mwenyekiti huyo aliwashukuru wananchi wa kijiji cha ngarenairobi pamoja na kampuni ya wachina(CGC) wanayojenga barabara ya Lami karibu na eneo hilo kwa msaada wao mkubwa wa kusaidiana na wananchi katika kukabiliana na moto.

 Nyumba moja  ya mbao yenye vyumba 16 na  nyumba nyingine  yenye vyumba vitano iliteketea kabisa na moto huo na kuacha familia hizo 18 zenye wakazi 42 bila ya kuwa na kitu chochote alisema Nkini.

Hata hivyo,kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ilifika eneo la tukio na kujionea uharibifu uliofanywa na moto huo na kutoa maelekezo kwa ofisi ya kata na vijiji kuwapa hifadhi wananchi waliopatwa na janga la moto.
 Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na ufuatiliaji bado unaendelea kujua kiini halisi cha kutokea kwa moto.

No comments:

Post a Comment