Tuesday 14 March 2017

Wananchi Wilayani siha washauriwa kufanya mazoezi mara kwa mara

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Siha Valerian Juwal  kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Siha  aliwataka wananchi wa Wilaya ya Siha na watumishi wa  Umma kushiriki vema katika mazoezi ya kila mwezi kama sehemu ya kutii wito wa makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliagiza wananchi wote kushiriki mazoezi walau kila jumamosi ya pili ya kila mwezi

Alieleza kuwa Wilaya ya siha imeshazindua siku ya kufanya mazoezi kwa wananchi ambapo uzinduzi huo ulifanyika uwanja wa isanja Nasai. Aliwapongeza wananchi ,watumishi na viongozi wa wananchi walioshiriki vema katika mazoezi hayo na kuwataka kuwa kichocheo kwa wananchi mahali wanakotoka.

Aliongeza kuwa kufanya mazoezi kuna faida nyingi zikiwemo kutunza AFYA bora,kuwa mkakamavu,mchangamvu na mazoezi ya pamoja pia yanasaidia kuongeza mahusiano miongoni mwetu.

Alisema kwa mfano,katika mazoezi tumekuwa pamoja na wenzetu wa Polisi ,Madaktari,wanasiasa,watumishi wa Umma na wananchi wengine pia,kimsingi tumepata fursa ya kujuana na kusalimiana.

Aliongeza kuwa,Halmashauri ya Siha imejipanga kuhakikisha kuwa usimamizi wa mazoezi unakwenda hadi ngazi ya kata na vijiji ili kila mwananchi apate fursa ya kushiriki katika mazoezi kila mwezi.

Aliwataka watendaji wa Kata na Vijiji vyote Siha kuhakikisha kuwa wanapanga utaratibu mzuri kwa kuwashirikisha wananchi kushiriki vema katika mazoezi katika kila kata. Naomba watendaji wangu muwe wabunifu kuchagua eneo katika kata yenu ambayo wananchi watashiriki vema na ikiwezekana kila kijiji wachague  eneo watakaloona linafaa kufanyia mazoezi.

Mwisho Mkurugenzi wa Halmashauri ya Siha kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya aliwataka viongozi wote kushirikiana na Serikali kwa kuwahamasisha wananchi kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuepukana na magonjwa nyemelezi kama vile shinikizo la damu,kisukari na mengine mengi.
 wananchi na watumishi Wilayani Siha wakishiriki katika mazoezi ya pamoja tarehe 11.3.2017 uwanja wa Isanja kata ya Nasai

Mazoezi yakiendelea kwa kasi kubwa siku ya uzinduzi Wilayani Siha

No comments:

Post a Comment