Tuesday, 16 May 2017

Siku za Wateka Bodaboda Zinahesabika Wilayani Siha

Mkuu wa Wilaya ya Siha  Mhe Onesmo Buswelu awaonya  wale wote wanaojihusisha na utekaji wa waendesha bodaboda  Wilayani Siha na kuchukua pikipiki zao kuwa siku zao zinahesabika.

Mkuu huyo wa Wilaya    ya Siha aliyasema hayo  katika mkutano wa Wananchi wa Kata ya Kirua pamoja na wazazi wa wanafunzi wanaosoma shule ya Sekondari Fuka leo jumanne tarehe 16.5.2017. 

Alieleza kuwa hivi karibuni kuna tukio moja la kusikitisha lilitokea kwa bodaboda mmoja kutekwa katika Kijiji cha Sanya Juu na kisha kuuwawa na pikipiki yake kuchukuliwa na watu wanaosemekana kuwa ni  watekaji.

alisema Serikali ya Wilaya ya Siha imeshawakamata  watu watatu waliohusika na tukio hilo na wapo katika mikono ya sheria ili wachunguzwe na kisha wapatiwe  adhabu kulingana na makosa yao waliyotenda.

Aliwataka Wananchi na raia wema kuendelea kutoa taarifa za  matukio na maandalizi yote ya makundi ya kihalifu kwa Jeshi la Polisi ili hatua za Haraka zichukuliwa kwa Wahalifu kabla hawajatimiza malengo yao.

Aliwataka vijana kujishughulisha na shughuli halali za kujipatia kipato kwani Matendo ya kihalifu kwa Serikali ya Mhe Magufuli hayana nafasi tena na badala yake vijana watekeleze kaulimbiu ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania HAPA KAZI TU

Siha yaweka mkakati wa kuendeleza zao la Kahawa




Wakulima wa Wilaya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro wameweka mikakati ya kulirudisha katika ubora wake zao la kahawa kama ilivyokuwa hapo miaka ya 1970 na mwaka 1960.

Mpango huo umewekwa na wakulima wa zao la Kahawa Wilayani Siha leo tarehe 15.5.2017 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha walipokutana na kufanya kikao cha pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Onesmo Buswelu.

Katika kikao hicho cha kazi Wakulima hao walimweleza Mkuu wa Wilaya ya Siha changamoto mbalimbali zilizosababisha kushuka kwa uzalishaji wa zao la Kahawa Wilayani Siha.Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na:-
·        Kushuka kwa bei ya kahawa kutoka kwa wanunuzi binafsi pamoja na vyama vya ushirika
·        Ukame wa muda mrefu katika Wilaya ya Siha
·        Kukosekana kwa mbegu bora ya zao la  kahawa
·        Hali ya kukata tama kwa baadhi ya wakulima na badala yake kutafuta zao mbadala
Akishiriki katika kikao hicho,Mkuu wa Wilaya ya Siha aliwataka wakulima kutokata tamaa ya bei kwani Serikali itasimamia kwa karibu kuhakikisha kuwa wakulima wanapata haki yao kulingana na bei ya soko.


Waliochukua Mashamba ya Kahawa watakiwa kuyaendeleza



Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe.Onesmo Buswelu awataka wanaomiliki mashamba kwa ajili ya kilimo cha kahawa kuyaendeleza mashamba hayo kwa mujibu wa mikataba yao kabla ya Serikali haijawachukulia hatua za Kisheria ikiwa ni pamoja na kuyachukua mashamba hayo.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema hayo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha leo tarehe 15.5.2017 alipokuwa akiongea na Wakulima na Wamiliki ya mashamba yanayoendesha kilimo cha Kahawa Wilayani Siha.

Mhe. Onesmo Buswelu aliwataka maofisa ugani wote pamoja na vyama vya ushirika kuhakikisha kuwa vinawapatia wananchi elimu ya kutosha kuhusu utunzaji wa zao la kahawa kwani ndiyo zao la kiuchumi linaloweza kuwakomboa Wananchi katika umaskini wa kipato kama ilivyokuwa hapo miaka1960 na 1970.

Aliwataka wanunuzi binafsi kutoa bei nzuri kwa wakulima na kuacha tabia za kuwanyonya Wakulima  kwa kuwapa bei za chini ambazo kimsingi ndizo zinawakatisha tamaa ya kulima zao hilo.

Mhe. Onesmo Buswelu Mkuu wa Wilaya ya Siha ametoa wito kwa  Wananchi wa Siha kutumia vema mvua zinazoendelea kunyesha katika kupanda mazao ya kudumu kama vile zao la Kahawa ,Matunda na mazao mengine kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Wananchi kukamilisha Ujenzi wa Maabara



Wananchi wa Kata ya Kirua Wilayani Siha pamoja na Wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule ya Sekondari Fuka wamekubaliana kwa kauli moja kukamilisha kazi ya ujenzi wa maabara tatu za masomo ya Sayansi katika shule hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Wananchi hao walipokuwa Wakiongea katika Mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Siha alioufanya katika shule ya Sekondari Fuka tarehe 16.5.2017.

Awali Mkuu wa Shule hiyo  mwalimu Swalehe Kombo  alisoma taarifa fupi ya maendeleo ya ujenzi wa Maabara katika shule hiyo ambapo alieleza kuwa zaidi ya shilingi milioni 5 zimetumika katika kuendeleza ujenzi wa maabara katika kipindi cha Novemba,2016 hadi Mei 15,2017.

Mkuu wa Shule hiyo alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa,  Wananchi wa Kata ya Kirua wameweka mpango wa kupata michango ya Shilingi elfu tano kwa kila kaya ,ambapo kupatikana kwa fedha hizo kutasaidia kuendeleza ujenzi wa Maabara katika shule hiyo.

Akiongea na Wananchi na Wazazi wa wanafunzi wanaosoma shule ya Sekondari Fuka iliyopo   Kata ya Kirua,Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Onesmo Buswelu aliwapongeza Wananchi kwa kuwa kuonyesha hali ya kujituma na moyo  ya kuchangia maendeleo hasa katika suala la elimu kwa watoto wao.

Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa Serikali itaendelea na jitihada zake za kushirikiana na Wananchi pamoja na wadau wa maendeleo katika kuleta maendeleo, na katika ujenzi wa maabara Serikali imeahidi kuleta vifaa vyote katika maabara hizo.  Alifafanua kuwa vifaa vya maabara vitakavyoletwa na Serikali ni vya gharama kubwa na vitahitaji kutunzwa na kuhifadhiwa kwa uangalifu na shule husika zitakazokabidhiwa.

Wilaya ya Siha inajumla ya shule 13 za Serikali ambapo kila shule inahitaji kuwa na maabara 3 kwa masomo ya Biolojia,Chemia na Fizikia kama ilivyo agizo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Friday, 12 May 2017

Serikali Wilaya ya Siha kuboresha miundombinu ya soko Sanya Juu

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa  jumla ya fedha za kitanzania milioni  71  ili kuboresha miundombinu katika soko la Sanya Juu Wilayani Siha.

Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe.Onesmo Buswelu akitoa taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyasema hayo leo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha.

Alieleza kuwa kazi hiyo inatarajiwa kuanza hivi karibuni na kutaka taratibu na kuanza kazi hiyo zifanyike kwa haraka na kwa kuzingatia taratibu zilizopo ili kuepukana makosa na hoja mbalimbali za ukaguzi.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa fedha zilizotolewa na Serikali zinatumika vizuri ili kutoa thamani halisi ya fedha hizo.

Kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo kutasaidia kuondoa adha na changamoto mbalimbali zilizopo katika soko hilo hasa nyakati za mvua nyingi kama ilivyo sasa.

Siha yaboresha ongezeko la Dawa katika Zahanati na Vituo vya Afya vya Umma

Hospital ya Wilaya ya Siha imeongeza manunuzi na upatikanaji wa Dawa za binadamu kwa asilimia 85 hadi kufikia mwezi Mei ,2017 kutoka asilimia 25 mwaka 2016.

Ongezeko hili limetokana na usimamizi mzuri unaofanywa na viongozi wa Serikali katika Wilaya ya Siha hasa katika kuhakikisha kuwa Wananchi na Wakazi wa Siha wanaendelea kupata dawa na matibabu ya uhakika katika Hospital za Umma.

Taarifa ya kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa katika Zahanati,Vituo vya Afya na Hospital ya Serikali imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Onesmo Buswelu alipokuwa akiongea na vyombo vya habari kuhusu shughuli za maendeleo zilizotekelezwa na Serikali Wilaya ya Siha tangu Oktoba ,2015 chini ya Serikali ya awamo ya tano inayoongozwa na Mhe.Dkt John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wananchi Wilayani Siha watakiwa kuchukua tahadhari ya Mvua zinazoendelea kunyesha

Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Onesmo Buswelu amewataka wakazi na Wananchi wa Wilaya ya Siha kuchukua tahadhari ya kutosha wakati huu mvua zinapoendelea kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo.

Hayo ameyasema wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo wa Serikali Wilayani Siha. Mhe Mkuu wa Wilaya ya Siha ameyasema hayo leo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha wakati alipohudhuria ufungaji wa mafunzo ya wataalam wa ugavi na manunuzi yaliyofanyika kimkoa katika Wilaya ya Siha.

Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi kuwalinda watoto wao nyakati za kwenda shule na wakati wa kurudi nyumbani ili wasipatwe na janga la kuzolewa na maji ya Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Wilayani hapa.