Monday, 17 October 2016

UTENZI WA KUMUENZI BABA WA TAIFA MWL JULIUS K NYERERE











UTENZI WA KUMUENZI HAYATI BABA  WA TAIFA MWL JULIUS K NYERERE 14/10/2016

1. Naanza kwa kumsifu,
Mungu wetu Mtukufu,
Yeye ni fundi Sanifu,
Sisi tumeumbwa naye.

2. Namtaja wetu Mungu,
Aliyekuwe tangu ,
Amezitundika Mbingu,
Ardhi katugawia.

3. Kwake yeye tunaishi,
Sisi kwake watumishi,
Wala hakuna ubishi,
Pumzi katujalia.

4. Mungu huyu ana utu,
Anazo nafsi tatu,
Roho,mwana,baba yetu,
Mola mmoja sikia.

5. Huyu ni wetu mkubwa,
Anayetoa ubwabwa,
Siriye imesiribwa,
Hakuna wa kufasiri.

6. Ba’da ya kumshukuru,
Mungu bila ya kukufuru,
Sasa ninayanukuru,
Niliyoyakusudia.

7. Nianze kusimulia,
Tendo la kihistoria,
Kifupi nitayasogoa,
Sikilizeni kwa makini.

8. Kwanza twarejea nyuma,
Kwa makini kutozama,
Tulivyofanywa wanyama,
Katika yetu aridhi.

9. Mkoloni kang’ang’ania,
Nchi akaikalia,
Wakaumia raia,
Wasijue la kufanya.

10. Akatokea kijana,
Mwenye upeo mpana,
Kasema tutapambana,
Tanganyika tuwe huru.

11. Namtaja Juliasi,
Huyu ndiye muasisi,
Kasema siyo rahisi,
Lakini tutaupata.

12. Mkoloni kakasirika,
Akaitwa kibaraka,
Mroho wa madaraka,
Tena asiyetosheka.

13. Wakoloni wauaji,
Ni wakubwa wanyonyaji,
Baba kawavua taji,
Uhuru tukaupata.

14. Tarehe tisa disemba,
Wananchi tukaimba,
Tukacheza na sindimba,
Uhuru kushangilia.

15. Falsafa ya ujamaa,
Ndiyo ilikuwa taa,
Pia kujitegemea,
Iwe ndio yetu njia.

16. Lugha yetu Kiswahili,
Ni mkubwa mhimili,
Juliasi kakubali,
Iunganishe raia.

17. Ni mwana diplomasia,
Mpenda Demokrasia,
Haki zote za raia,
Yeye aliyepigania.

18. Usawa wa Binadamu,
Kaka dada na binadamu,
Sote tushike hatamu,
Kuleta maendeleo

19. Na elimu ya Msingi,
Aliyesema mambo mengi,
Isiwekewe vigingi,
Ni haki  ya kila mtu.

20. Nchi zote kapitia,
Afrika nzimasikia,
Hamasa akiwatia,
Lazima wajitawale.

21. Kasema Afrika viva,
Kongo mambo yakaiva,
Msumbiji,Angola viva,
Zimbabwe na Namibia.

22. Pote aliheshimika,
Wakawa na uhakika,
Bendera wakasimama,
Hongera baba Nyerere.

23. Jama huu ni utenzi,
Una nyingi sana beti,
Ninalikunja busati,
Wengine wamalizie,

24. Mengi nimeelezea,
Kuwachosha siyo nia,
Kwa hapa nitakomea,
Hadi wakati mwingine.

Imeandaliwa na kusomwa na:
MWL JUSTINA MOHAMED NGOLINDA
SHULE YA Sekondari Oshara-SIHA KILIMANJARO

No comments:

Post a Comment