Thursday, 6 October 2016

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MIRADI YA MAENDELEO ILIYOKAMILIKA WILAYA YA SIHA ROBO YA KWANZA YA MWAKA WA FEDHA 2016/2017





HALMASHAURI YA WILAYA YA SIHA
TAARIFA KWA UMMA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha Valerian M Juwal anapenda kuwajulisha  Wananchi na Wadau wa maendeleo katika Wilaya ya Siha kuwa katika mpango wa muda mfupi wa Serikali  wa kutekeleza shughuli za maendeleo kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Siha,Halmashauri ya Wilaya ya Siha imefanikiwa kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi. Mpango huu mfupi wa kukamilisha miradi hiyo ya maendeleo umetekelezwa kwa kipindi cha Robo ya kwanza (Julai hadi Septemba,2016) kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Kwa kipindi kifupi cha robo ya kwanza ya mwaka wa Fedha 2016/2017 Halmashauri ya Wilaya ya Siha kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa Wananchi. 

Katika taarifa yake kwa Umma Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya  amesema kuwa, Jumla ya miradi mitano mikubwa  imekamilika kwa kipindi hicho, na alitoa ufafanuzi wa majina ya miradi  iliyokamilika kuwa ni miradi miwili ya barabara,mmoja wa Afya,mmoja wa Maji na mmoja wa Elimu Sekondari.

Pamoja na miradi mingine inayoendelea kukamilishwa na Halmashauri ya Wilaya ya Siha ,mkurugenzi wa halmashauri ya Siha alitaja miradi iliyokamilishwa na Halmashauri ya Siha kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba,2016  na  kubainisha kiasi cha fedha kilichotumika  na kutaja  majina ya   wachangiaji wa Fedha hizo kama ifuatavyo:-

1.     Ujenzi wa Zahanati ya Magadini: ujenzi wa Zahanati ya Magadini kata ya Gararagua umekamilika na umeanza kutumika. Ujenzi huu umekamilika kwa gharama ya shilingi za Kitanzania 201,830,749/= na wachangiaji ni Serikali Kuu ilichangia Tsh. 30,889,000/=,Halmashauri ya Wilaya ya Siha ilichangia Tsh. 17,500,000/=,TANAPA Tsh. 150,536,749/= na Wananchi walichangia Tsh. 2,905,000/=.

2.     Ujenzi wa Tanki la Maji. Ujenzi huu umefanyika katika kijiji cha Kandashi Kata ya Karansi na Tanki lenye ujazo wa lita 50,000 limejengwa na kukamilika. Ujenzi wa tanki hili la maji umekamilika kwa gharama ya fedha ya Kitanzania shilingi 65,000,000/= nafedha zote zimetolewa na Serikali kuu.

3.     Ukarabati mkubwa wa barabara ya Karansi-Tenki la Maji: Ukarabati huu mkubwa wa barabara inayounganisha kata za Karansi na Biriri umekamilika kwa gharama ya Fedha za kitanzania shilingi 633,024,100/= na fedha za ukarabati huu zimetoka Serikali kuu.

4.     Ujenzi wa Nyumba za Walimu Namwai Sekondari(six in one): ujenzi wa miundombinu ya nyumba za walimu katika shule ya sekondari Namwai kata ya Ngarenairobi umekamilika kwa gharama ya fedha za kitanzania shilingi 150,000,000/=na fedha hizi zote zimetoka Serikali Kuu.

5.     Ukarabati mkubwa wa barabara ya Kifufu-Mowonjam na Ngirini-Nsherehehe-Ngaroni. Ujenzi wa mradi huu umekamilika kwa gharama ya fedha za kitanzania shilingi 829,954,000/= na fedha za mradi huu zimetoka Serikali Kuu.

NB: Katika utawala bora, Halmashauri ya Wilaya ya Siha inalo jukumu la kuwajulisha Wananchi na Wadau wa maendeleo shughuli zote za maendeleo na za kijamii zinazotekelezwa na Halmashauri yao kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Imetolewa na

Mkurugenzi Mtendaji (W) Siha kupitia Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Tarehe 06 oktoba,2016

No comments:

Post a Comment