Tuesday, 30 May 2017

Wanaowapa Wanafunzi mimba watangaziwa Kiama Siha




Halmashauri ya Wilaya ya Siha Mkoa wa Kilimanjaro leo tarehe 30 mei,2017 imefanya maazimisho ya juma la elimu kwa kufanya maonesho mbalimbali ya kielimu na kujumuisha wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari Wilayani hapa.

Maazimisho hayo yamefanyika Kiwilaya katika shule ya Msingi Sanya juu ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Onesmo Buswelu.

Katika hotuba yake katika maazimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe.Onesmo Buswelu alisema kuwa wale wote wanaosababisha mimba kwa wanafunzi sasa wakati umefika wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Mkuu wa Wilaya aliongeza kuwa wapo  baadhi ya wazazi kwa kushirikiana na walimu wamekuwa wakiwaficha wahalifu hao mara baada ya kutenda makosa yao.

Aliongeza kuwa kuanzia sasa mtu yeyote atakayesababisha mimba kwa mwanafunzi wa shule Serikali ya Wilaya ya Siha itamsaka popote atakapokwenda na kuhakikisha mtu huyo anachukuliwa hatua za kisheria.

Mhe Onesmo Buswelu Mkuu wa Wilaya ya Siha ametoa wiki mbili kwa wakuu wote wa shule za Sekondari Wilaya ya Siha kumpelekea taarifa za miaka mitatu iliyopita kuhusu hali ya mimba katika shule.

Aliongeza kuwa iwapo atabaini kuwa tatizo la mimba limekuwa likijirudia katika shule moja kwa miaka miwili au mitatu mfululizo basi hata sita kumchukulia hatua stahiki mkuu wa shule husika.

Mkuu wa Wilaya ambaye pia alikuwa mgeni rasmi wa siku ya Elimu Siha alitoa wito kwa  Wazazi kushirikiana na Walimu ili kuboresha kiwango cha ufaulu cha wanafunzi katika shule za msingi na Sekondari Wilayani Siha. Wilaya ya Siha inajumla ya shule 59 za Msingi na  shule 19 za Sekondari.

Thursday, 25 May 2017

Taarifa kwa Umma kuhusu Kazi zilizotekelezwa na Serikali Wilayani Siha-Mkoa wa Kilimanjaro



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS TAMISEMI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KAZI ZILIZOTEKELEZWA NA SERIKALI WILAYANI SIHA

Ndugu Wanahabari,na Wananchi
Napenda kuchukua fursa hii  kuwakaribisha sana katika Wilaya ya Siha  ili niweze kukutana nanyi kwa lengo la kutoa taarifa  ya mambo mbalimbali ya maendeleo yanayoendelea katika Wilaya ya Siha tangu Serikali ya Awamu ya tano ilipoingia madarakani chini ya Mhe. Dkt John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kabla sijaanza kutoa taarifa yangu naomba kuishukuru Serikali yetu kwa kutupatia fedha  za kutekeleza miradi ya maendeleo katika Wilaya yetu ya Siha.

Pili napenda kuwashukuru Wananchi wote wa Wilaya ya Siha kwa kushirikiana na Serikali yao katika shughuli za miradi ya  maendeleo pamoja  na suala zima la utunzaji wa Amani katika Wilaya yetu.

Ndugu Wanahabari
Nianze na hali ya ulinzi na usalama, kwa ujumla Wilaya ya Siha ni salama kabisa na hakuna tukio lolote ambalo limetokea la kuhatarisha amani na hii imetokana na tabia njema ya Wananchi wa  Wilaya ya Siha kama walivyo Watanzania wengine kuwa na utamaduni wa kudumisha amani, kipekee nawashukuru Wananchi na wakazi wa Wilaya ya  Siha kwa kuendelea kudumisha amani wakati wote hasa katika sikukuu ya Pasaka  mwaka huu 2017 iliyofanyika tarehe 16-17/04/2017, ambapo kuwepo kwa amani kumesaidia  Wananchi   kuendelea na shughuli za kiuchumi ambazo zinawapatia kipato ikiwemo shughuli za  Kilimo,Ufugaji  na biashara ndogondogo.
Ndugu Wanahabari,
Katika kutekeleza miradi ya maendeleo Serikali ya awamu ya tano imewezesha miradi mbalimbali kukamilika na mingine inaendelea kukamilishwa katika hatua mbalimbali. Miongoni mwa miradi iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya Tano Chini ya Mhe.Dkt John Pombe Magufuli ni kama ifuatavyo;-

1.   Katika sekta ya Kilimo,Ushirika na Umwagiliaji,Serikali imewezesha na kuleta fedha Wilayani Siha  kiasi cha Tshs. 165,000,000/= zilizowezesha kukamilisha ujenzi wa mita 1000 za mfereji wa maji ya Umwagiliaji Kijiji cha Kishisha Kata ya Ivaeny.  Pia Serikali imetoa fedha kiasi cha Tshs 165,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa  mfereji wa umwagiliaji Kijiji cha Mowonjamu Kata ya Livishi  wenye urefu wa mita 700 na kujenga bwawa la kuhifadhia maji . Baadhi ya Kazi zimekamilika na nyingine zipo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.  Vile vile kama mnavyoona mvua kwa sasa ni nyingi na mazao mashambani yanaendelea vizuri na matajio yetu kama Wilaya ya Siha  ni kupat tani 102,705 kwa mazao ya chakula na Biashara, Pia Wilaya inategemea kupata tani 10,126 kwa mazao ya Bustani na mbogamboga. Pia kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika Wilaya yetu ya Siha naomba kutoa wito kwa Wananchi kuchukua tahadhari ili kujiepusha na madhara yanayoweza kujitokeza hasa kuangalia Wanafunzi wanaokwenda shuleni asubuhi wasije kuzolewa na maji.
2.   Mfuko wa Wanawake na Vijana. Katika kipindi kifupi tangu Serikali ya awamu ya Tano kuingia madarakani Jumla ya FedhaTsh. 75,000,000/= zimetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Siha Siha kwa ajili ya Kusaidia vikundi mbalimbali vya Wanawake na Vijana. Katika Fedha hizo jumla ya vikundi 20 vya Wanawake vyenye wanufaika 316 wamepatiwa mikopo, Pamoja na vikundi 7 vya vijana vyenye wanufaika 130 vimewezeshwa kupitia asilimia 10 ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri ya Siha. Hata hivyo Nimetoa agizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa asilimia 5 ya vijana na 5 ya Wanawake inatolewa katika Makusanyo ya Mapato ya ndani ya Halmashauri ili kuwezesha  kuongeza wanufaika wengi zaidi katika Makundi ya Vijana na Wanawake.

3.   Katika Sekta ya Afya; Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia fedha jumla ya Tsh. 250,000,000/= kwa ajili ya kukamilisha jengo la OPD sakafu ya juu katika Hospital yetu ya Wilaya ya Siha. Kazi hii inafanyika kwa kupitia “force account” na inasimamiwa na Wataalam  na Watumishi wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwezi Juni,2017. Serikali ya Wilaya ya Siha imeamua kutumia “force account” ili kuhakikisha kuwa fedha za Serikali zinatumika vizuri na kutoa thamani halisi ya fedha. Aidha kwa upande mwingine Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Siha kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji imepanga kufanya harambee ambayo itawezezesha ujenzi wa majengo matatu (Wodi ya Wazazi,Wodi ya Watoto na Jengo la upasuaji) Majengo haya yana thamani ya Fedha za Kitanzania 880,000,000/=. Mpango huu umeshirikisha  Wanannchi wa Wilaya ya Siha, wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya Halmashauri pamoja na Watumishi wa Wilaya ya Siha. Lengo la mpango huu ni kuwaondolea usumbufu na kuwapunguzia  Wananchi wa Siha gharama za matibabu kwa wagonjwa wao hasa wanapopewa rufaa  katika Hospital ya Mkoa Mawenzi na Hospital ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi.
Hata hivyo hadi sasa Jumla ya Tsh. 52,000,000/= zimepatikana  na vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Tsh 11,000,000/= vimetolewa na wadau mbalimbali na Wananchi ,huku ahadi zenye thamani ya Tsh milioni 62 zikitarajiwa kupokewa ili kukamilisha ujenzi huo. Hata hivyo michango iliyotolewa, ahadi na vifaa vilivyotolewa zinafikia jumla ya Tshs 125,000,000/=.Hadi sasa ujenzi wa wodi ya wazazi  umeanza na ujenzi wa  Msingi umekamilika na kazi ya ujenzi inategemewa kukamilika mwezi Julai,2017 kama wadau na wananchi waliotoa ahadi zao watakamilisha kwa wakati. Hata hivyo Serikali imeongeza kiwango cha ununuzi wa dawa katika Zahanati na vituo vya Afya vya Serikali kutoka asilimia 25% mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 85% mwaka huu.

Ndg Wanahabari. Napenda kuwashukuru Wananchi wa Siha kwa ushirikiano wa dhati walionesha katika ujenzi wa  kazi hii muhimu, na napenda kutoa wito kwa Wananchi,Watumishi na Wadau wengine wa maendeleo kukamilisha ahadi zao walizotoa ili kufanikisha mpango huu wa ujenzi kwa wakati. Vilevile natoa wito kwa Wananchi na wadau wengine nje na ndani ya Wilaya kutuunga mkono katika ujenzi wa Hospital ya Wilaya ya Siha. 

4.   Sekta ya Elimu. Serikali ya awamu ya Tano imeendelea kutimiza azma yake ya kutoa elimu bure kuanzia darasa la awali hadi kidato cha Nne kwa kuhakikisha kuwa Mahitaji muhimu ya shule yanapatikana  kama vile vitabu,mishahara ya Watumishi,vifaa muhimu vya maabara mpya zilizojengwa, mafunzo kwa watumishi hasa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari yametolewa ili kuwajengea uwezo. Katika sekta ya Elimu, Serikali ya awamu ya tano imeweza kujenga nyumba mbili za Walimu(Six in one) katika shule za Sekondari Suumu na Namwai kwa gharama ya Tsh.300,000,000/=, hadi sasa nyumba hizo zimekamilika na  zimeanza kutumika na Walimu wa shule husika. Pia Serikali imetoa fedha  jumla ya Tsh. 24,000,000/= za ukarabati wa  madarasa matatu katika shule ya Sekondari Suumu na kazi imekamilika. Vile vile Serikali imetoa Tsh. Milioni 36 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 18 ya vyoo katika shule ya Sekondari Namwai na Suumu(Namwai matundu 16 na Suumu matundu 2). Kwa kipindi hiki pia Serikali imetoa Jumla ya Tsh milioni 71 za ujenzi wa Bweni la Wanafunzi katika shule ya Sekondari Oshara, kazi hii inaendelea na inatarajiwa kukamilika mwezi Julai 2017. Katika kuboresha Elimu  Serikali imetoa jumla  ya madawati 537 Wilayani Siha ili kuonesha kwa vitendo azma ya kuboresha elimu kwa jamii ya watanzania. Madawati haya yamegawanywa katika shule za Msingi na Sekondari za Serikali Wilaya ya Siha na kusaidia kuondoa upungufu wa  madawati uliokuwepo hapo awali. Hadi sasa Wilaya ya Siha inayo madawati ya ziada 747 kwa kujumuisha Elimu Msingi na Sekondari. Halmashauri ya Wilaya ya Siha inapokea kila mwezi jumla ya Kiasi cha Fedha za Kitanzania shilingi  38,093,000/= Katika kutekeleza elimu bila malipo katika shule za Sekondari na Kiasi cha Shilingi 29,187,000/= hutolewa na Serikali Kila mwezi ili kugharamia   elimu kwa shule za msingi. Pia Serikali imetoa jumla ya vitabu 6834 kwa shule za  Sekondari Wilaya ya Siha katika masomo ya Sanaa na Sanyansi. Wito wangu kwa Wanafunzi wote waliopo mashuleni kuhakikisha kuwa wanasoma kwa bidii na maarifa kwani jamii na Taifa linawategemea wao katika kuleta maendeleo ya familia zao,Jamii na Taifa kwa Ujumla wake. Pia nawahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii ili kuondokana na kuwa na vyeti Feki kama baadhi ya watumishi wa Umma walivyogundulika katika maeneo mbalimbali hapa Nchini kuwa na vyeti feki, hii ilitokana na wao kutosoma kwa bidii wakati wakiwa wanafunzi. 

Ndugu Wanahabari;
Vilevile katika kuboresha miundombinu ya barabara Serikali ya Awamu ya tano chini ya uongozi bora wa Mhe John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza ujenzi wa barabara ya kiwango cha  Lami kutoka Sanya Juu hadi Elerai yenye urefu wa Km 32.2 kwa gharama  ya fedha za Kitanzania shilingi bilioni 52.3. Ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha Lami umeanza rasmi mwezi Machi mwaka huu na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba,2018. Kukamilika kwa barabara hii kutasaidia kufungua fursa za uchumi katika Tarafa ya Siha Magharibi na Wilaya ya Siha kwa ujumla, hasa kusaidia kupitisha watalii zaidi wanaopanda mlima Kilimanjaro kupitia lango la Londorosi pamoja na kurahisisha kusafirisha mazao mbalimbali yanalimwa kwa wingi katika mashamba makubwa ya West Kilimanjaro. Pia Serikali imeendelea kutoa fedha za kuwezesha  ujenzi wa barabara ndani ya wilaya ya Siha  kwa viwango vya Changarawe, miongoni mwa barabara hizo ni kama ifuatavyo;-i)Ujenzi wa barabara ya Kifufu Mowonjam na Ngirini, Nsherehehe hadi Ngarony yenye urefu wa km 14.6 kwa gharama ya fedha za Kitanzania shilingi 829,954,000/= na  kazi ya ujenzi imekamilika. (ii)Barabara ya Karansi Tanki la maji yenye urefu wa  Km 6.4 iliyogharimu kiasi cha Tshs.  633,024,100/=imekamilika (iii) Pia  Serikali  imetoa fedha zilizowezesha ujenzi wa Kalvati kubwa la Kisube Kirisha na ujenzi wa  barabara yenye urefu wa  Km 2.5 kwa gharama ya shilingi za Kitanzania 920,172,587.50/= kazi hii ya ujenzi imekamilika na ipo katika kipindi cha uangalizi.

Ndugu Wanahabari:
Aidha, katika miradi ya Maji Serikali ya awamu ya tano imetoa fedha Kiasi cha Tsh. 1,682,062,000/= Wilayani Siha kwa ajili ukarabati na upanuzi wa mradi wa maji Magadini Makiwaru katika vijiji vya (Wiri,Mawasiliano,Lekrimuni,kandashi na Orkolili) na mradi wa Maji lawate Fuka katika vijiji vya Kishisha,Donyomuruak,Embukoi,Ngaritati na Naibili). Kazi za ukarabati katika miradi hii ya maji imekamilika na Wananchi wa Siha wanapata maji safi na Salama katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Siha.
Ndugu Wanahabari,
Katika mpango wa Serikali wa kunusuru Kaya Maskini kupitia Mradi wa TASAF III,Jumla ya Kaya Maskini 1871 Wilaya ya Siha zimewezeshwa na kunufaika na mpango huu wa Serikali wa kunusuru Kaya Maskini na Jumla ya Fedha za Kitanzania Shilingi 691,638,636/= zimetumika. Kwa niaba ya Wananchi wa Wilaya ya Siha napenda kutoa shukrani za dhati kwa Serikali yetu tukufu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusaidia jamii ya Watanzania hasa kaya zisizo na uwezo. Wito wangu kwa wanufaika wa mpango huu, napenda kuwaasa wanufaika wote kuwa na nidhamu bora ya matumizi ya fedha wanazopatiwa na Serikali kupitia mpango huu. 

Ndugu Wanahabari:
Soko la Sanya Juu, katika kuboresha miundombinu ya soko kuu la Wilaya ya Siha yaani    soko la Sanya Juu,Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosimamiwa na Chama Cha Mapinduzi  imetoa jumla ya shilingi 71,161,200/= kwa Halmashauri ya siha ili kusaidia kuboresha miundombinu katika soko hilo. Kwa sasa taratibu zinaendelea na kazi hiyo inatarajiwa kuanza mwezi wa Juni,2017. Mimi Mkuu wa Wilaya ya Siha na msimamizi wa shughuli za Serikali Wilaya ya Siha nimemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa viwango vinavyotakiwa ili kuonyesha thamani halisi ya fedha za Umma zilizotolewa.

Ndugu Wanahabari:
Katika hatua za kuharakisha maendeleo ya Wananchi Wilaya ya Siha,Serikali kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017 imetoa  Fedha za mfuko wa Jimbo jumla shilingi 29,084,000/= kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ya Wananchi katika Kata na vijiji mbalimbali Wilayani Siha. Kwa niaba ya Wananchi wa Siha napenda tena  kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuletea fedha za mfuko wa Jimbo ambazo kimsingi zinatusaidia sana katika maendeleo ya Wananchi ya Wilaya yetu ya Siha.
Ndugu Wanahabari:
Serikali ya Wilaya ya Siha inapenda kuwashukuru Wananchi na Wakazi wa wote wa Wilaya Siha, wadau wa maendeleo pamoja na Sekta Binafsi  kwa kutoa ushirikiano hasa katika shughuli za maendeleo bila kujali tofauti za itikadi za Kisiasa ,maeneo watu wanapotoka na imani zetu za madhehebu ya Dini. Kwa kufuata misingi ambayo baba wa Taifa mwalimu Julius K Nyerere alituachia, Wilaya ya Siha tunategemea kuendelea  kupata maendeleo makubwa ndani ya muda mfupi ujao. Naomba kutoa wito kwa Wananchi, Wadau wa maendeleo  na Viongozi wote Wilayani Siha kudumisha mshikamano uliopo ili kutimiza malengo ya Serikali ya awamu ya tano katika kuwaletea Wananchi wake maendeleo ya kweli. 

Ndugu Wanahabari:
Vilevile, kabla ya kufikia mwisho wa taarifa yangu,naomba kutoa wito kwa Watumishi wote wa Umma kufanya kazi za kuwahudumia Wananchi  kwa uadilifu na weledi mkubwa ili kulinda heshima ya Watumishi wa Umma na Serikali kwa ujumla.  Serikali ya awamu ya tano haipo tayari kuwavumilia watumishi wazembe,wavivu ,walarushwa pamoja na wale wote wanaofanya kazi kwa mazoea.

Ndugu Wanahabari,
Mwisho Serikali ya Wilaya ya Siha kwa kuzingatia muongozo wa Ilani ya Chama  cha Mapinduzi (2015-2020) itaendelea kusimamia na kuratibu miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha kuwa fedha za Serikali zinatumika kwa malengo tu yaliyokusudiwa. Natoa wito kwa watumishi wote wa Umma Wilayani Siha kuhakikisha kuwa wanasimamia Ilani ya Chama Tawala na kutimiza malengo yaliyowekwa na Serikali ya awamu ya Tano chini ya uongozi bora wa Mheshimiwa John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mungu ibariki  Afrika,Mungu ibariki Tanzania na Mungu ibariki Wilaya ya   Siha
asanteni sana kwa kunisikiliza
Imetolewa na:-
Mhe; ONESMO M. BUSWELU
MKUU WA WILAYA YA SIHA
Leo tarehe 12/05/2017

Wednesday, 24 May 2017

Taarifa ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha katika Baraza la Madiwani Kipindi cha Januari hadi Machi 2017



OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

HALMASHAURI YA WILAYA YA SIHA



TAARIFA YA MWENYEKITI  WA HALMASHAURI   MKUTANO  WA KAWAIDA WA  BARAZA LA MADIWANI  KATIKA KIPINDI CHA ROBO YA TATU (JANUARI -MACHI,2017).
v  Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Siha,
v  Mwakilishi Ofisi ya RAS-Mkoa wa Kilimanjaro,
v  Mh. Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Siha,
v  Mh. Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Siha,
v  Waheshimiwa Madiwani,
v  Mkurugenzi Halmashauri ya Siha,
v  Viongozi wa Dini,
v  Wageni Waalikwa,
v  Ndugu Wataalamu,
v  Waandishi wa Habari,
v  Wananchi wa Wilaya ya Siha,
v  Mabibi na Mabwana,

Wasalaam Alekumu,Tumsifu Yesu Kristo,Bwana Yesu asifiwe

Wah. Madiwani ,  na Ndugu  Wananchi;
Kwanza kabisa napenda kuwakaribisha Waheshimiwa Madiwani,Wananchi,Wadau wa maendeleo,Wataalam wa Halmashauri na Waandishi wa Habari katika  Mkutano  wa Kawaida wa Baraza la Madiwani katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2016/2017 (Januari hadi Machi,2017). Katika kipindi hiki tumeshuhudia Halmashauri yetu ikiendelea na shughuli zake za kuwapatia Wananchi wa Wilaya ya Siha huduma mbalimbali zikiwemo za Afya,Elimu,Maji na huduma nyinginezo. Kipekee napenda kuwapongeza Waheshimiwa Madiwani na Wataalam wa Halmashauri ya Siha kwa kuiwezesha Halmashauri ya Siha kupata hati Safi na kuwa miongoni mwa Halmashauri za Mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania. Naomba kwa pamoja tuendelee kushirikiana  Viongozi na Watumishi ili kuhakikisha kuwa Halmashauri yetu inaendelea kufanya vizuri na kupata hati safi kwa miaka mingi ijayo.  

(1)UKUSANYAJI WA MAPATO
Waheshimiwa Madiwani,
Kama mnavyojua Waheshimiwa Madiwani na ndugu  Wananchi wa Siha kuwa bado Halmashauri yetu inakabiliwa na kuwa na tatizo la kuwa na vyanzo vichache na vya kudumu kwa ajili kukusanya Mapato ya ndani ya Halmashauri. Nawaomba tena kwa umoja wetu tuendelee kubuni vyanzo mbalimbali vya kuongeza mapato ya ndani ya  Halmashauri  yetu ili itusaidie kuboresha huduma mbalimbali kwa Wananchi wetu. Ukweli ni kwamba vyanzo  vya mapato ya ndani vilivyopo sasa  kama vile ushuru wa Masoko,Ushuru wa mazao,Leseni na Vituo vya Mabasi siyo vyanzo vya kutegemewa sana kwani mapato tunayopata kutoka vyanzo hivi bado ni kidogo sana. Napenda kutoa Rai kwa viongozi wenzangu tufikirie zaidi nakuwa wabunifu zaidi hasa namna ya  kupata fedha kutoka kwa Mashamba makubwa yaliyopo Wilayani Siha na tufanye juhudi kuhakikisha masuala ya uwekezaji katika Wilaya yetu yanaimarika zaidi hasa ule mradi mkubwa wa kituo cha Utalii. Tusipofanya juhudi za makusudi kwenye suala la kuongezaukusanyaji wa Mapato ya ndani ya Halmashauri naona uwezekano mkubwa wa Halmashauri yetu kushindwa kutoa huduma zinastahili za kuwaletea Wananchi maendelea hasa katika Kata na Vijiji vyetu.

 (2) UTUNZAJI WA MAZINGIRA
Waheshimiwa Madiwani,ndg  Wananchi na Wataalam.
Napenda kuendeleza kuwahimiza Wananchi na Wakazi wote wa Wilaya ya Siha kutumia vizuri baraza za Mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa katika Wilaya yetu kwa  kupanda miti ya kutosha ili kuimarisha mazingira yetu na kurudisha uoto wa asili kama ilivyokuwa hapo miaka ya nyuma. naomba kurudia tena ombi langu kwa Wananchi na Wakazi wa Wilaya ya Siha kuhakikisha  kila kaya kuotesha angalau miti 5 kila mwaka na kama inawezekana tuweke kwenye sheria ndogo za Halmashauri ambazo zitamtaka kila mwenye eneo la ardhi kuotesha miti ya kutosha kulingana na ukubwa wa eneo lake. Kwa hili naomba kurudia kwa kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa Watendaji wa Kata na Vijiji katika Halmashauri ya Siha  kupitia vikao vya Vijiji na Vitongoji wanawaelimisha wananchi kuhusu upandaji wa miti katika maeneo yao. Ndugu Mkurugenzi agizo langu hili nitalifuatilia kwa karibu kuona jinsi gani Serikali za Vijiji na Kata limelitekeleza kwa Vitendo na wale wote watakaoshindwa kutekeleza naomba wachukuliwa hatua stahiki kwani wanapinga suala zima la kuboresha mazingira ya Wilaya yetu. Nawaomba Viongozi wenzangu tushirikiane kwa pamoja kuwaelimisha Wananchi katika Kata na Vijiji tunapotoka ili kufanikisha zoezi hili muhimu kwa ustawi wa Wilaya yetu ya Siha..
Aidha, najua adui mkubwa wa miti ni mifugo,naomba wote kwa pamoja tusaidiane kulinda mifugo  yetu ili isiharibu miti tunayopanda kila mwaka katika maeneo yetu. 

Waheshimiwa Madiwani,Ndugu Wananchi;
(3)ELIMU
Katika suala la Elimu,Naombakutoa wito kwa wazazi na Walezi kutimiza wajibu wao ili kuhakikisha kuwa watoto wao mashuleni wanapata mahitaji muhimu kama vile,Madaftari,Kalamu,Sare za shule pamoja na chakula cha mchana wakiwa shuleni. Hili nalirudia mara kwa mara kwa kuzingatia umuhimu wa elimu katika maisha ya kila siku ya binadamu,Jamii na Taifa kwa ujumla wake.Sambamba na hilo hivi karibuni kumefanyika Mtihani wa  Taifa wa Kidato cha Sita katika shule zetu za Oshara,Nuru,Sanya Juu na Magadini na taarifa nilizopata ni kuwa mitihani hiyo imefanyika kwa utulivu wa hali ya juu na hakuna jambo lolote lililo nje ya utaratibu limeripotiwa. Kwa hili naipongeza ofisi ya Mkurugenzi kwa kusimamia zoezi hili hadi limefanyika kwa ufanisi Mkubwa,Hata hivyo ni matumaini yetu kuwa matokeo ya Mtihani  huo yatakuwa mazuri katika shule zetu za Wilaya ya Siha pindi yatakapotangazwa na Idara/Wizara husika. Vilevile nimepata taarifa kuwa Mitihani ya Majaribio ya Mkoa kwa Wanafunzi wa Kidato cha nne (Mock) inatarajiwa kuanza hivi karibuni katika shule zetu za Sekondari Wilaya ya Siha. Naomba kuwatakia Wanafunzi wote wa Kidato cha Nne kwa mwaka huu kujiandaa vema kwa mitahani hiyo na Hatimaye kupata matokeo mazuri yatakayoiwezesha Wilaya ya Siha kupata ufaulu mzuri. ’’ Elimu ni ufunguo wa maisha kila  mtu atimize wajibu wake ’’.

(4) UTUNZAJI WA BARABARA
Waheshimiwa Madiwani,Ndugu Wananchi;
 Naomba tena kuwakumbusha wananchi wa  Halmashauri ya Siha kuhakikisha kuwa kila mmoja anashiriki kikamilifu katika  kuzitunza barabara zilizojengwa na Serikali katika Kata na Vijiji vyetu. Pamoja na kuwa na Changamoto ya mvua zinazoendelea kunyesha katika Wilaya yetu bado tunao wajibu wa kuendeleza kuzitunza barabara zilizopo katika maeneo yetu. Kwa mfano utakuta mfereji wa maji umepasuka na maji yanaelekea barabarani lakini mara nyingine kwa mshangao Serikali za maeneo husika hazichukui hatua zinazotakiwa za kuziba maji hayo. Naomba kutoa Wito kwa Watendaji wa Vijiji na Kata kwa kushirikiana na Wananchi wahakikishe kuwa barabara zote zilizopita maeneo ya Vijiji na Kata zao zinalindwa hata kwa kuwapa adhabu wale wote wanaoharibu barabara kwa makusudi.   
Naomba kutoa agizo kuwa kuanzia sasa ni marufuku kwa mtu yeyote  kukata barabara bila kibali cha Mkurugenzi Mtendaji  na yeyote atakayekiuka agizo hili basi  achukuliwe hatua ili iwe fundisho kwa wenzake. Mkutano wa baraza lililopita liliagiza tena hili lakini sijapata taarifa ya Waharibifu wangapi wa barabara wamechukuliwa hatua za kisheria.

(5)UWAJIBIKAJI KAZINI
Waheshimiwa Madiwani,Ndugu Wananchi;
Kama ilivyokuwa katika taarifa zangu kwa Baraza la Madiwani,napenda kuwakumbusha tena Watumishi wa Serikali waliopo Wilaya ya Siha kuwa Serikali ya awamu ya tano imeshasema kuwa haitawavumilia Watumishi wazembe na wabadhirifu kazini. Naomba kila mtumishi atimize wajibu wake kwa mujibu wa taaluma aliyosomea na kwa kufuata sheria na taratibu za utumishi wa Umma. 

Aidha ,naomba kumwagiza Mkurugenzi kuwa Watumishi wote waliobainika kuwa na vyeti visivyo sahihi(vyeti Feki) wasiruhusiwa kuwepo maeneo ya kazi katika halmashauri yetu kama agizo la Mhe. Dkt John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa siku ya Mei Mosi katika uwanja wa Chuo cha Ushirika Mjini Moshi. Mheshimiwa Rais aliagiza kuwa watumishi hao wasionekane maeneo ya kazi ifikapo Mei 15,2017 na atakayeonekana atachukuliwa hatua za kisheria. Mkurugenzi hili ni lako nakuomba usimamie kwa karibu kama bado unaipenda kazi yako ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji,mimi kama Mwenyekiti wa Halmashauri ya Siha nimeona nikukumbushe hilo ili ufuatilie kwa karibu zaidi.

Waheshimiwa  Madiwani na ndg Wananchi;
Kabla ya kufika mwisho wa Taarifa yangu, napenda  kuwashukuru tena Wananchi wa Wilaya ya  Siha na Waheshimiwa Madiwani  kwa ushirikiano  wenu wa dhati mnaoendelea kunipatia kwa ajili ya kutekeleza majukumu yangu ya Kila siku. Naomba kuchukua fursa hii kuwahimiza Wananchi wa Siha  kuzitumia vema mvua zinazonyesha kwa ajili ya mazao ya chakula na biashara bila kusahau uoteshaji wa miti katika maeneo yetu ili kulinda mazingira. Kwani ipo kauli ya mazingira inayosema ’’MISITU NI UHAI’’. Naomba wote kwa umoja wetu tufanye kazi kwa kushirikiana ili kuharakisha maendeleo yetu pamoja na maendeleo ya  Familia zetu , Wilaya ya Siha na Taifa kwa ujumla wake.
Mwisho kabisa  ,nichukue fursa hii kwa niaba ya baraza la Madiwani, kuwashukuru tena kwa usikivu wenu mkubwa mlionesha tangu mwanzo wa taarifa yangu, naomba usikivu na utulivu huu uendelee hadi mwisho wa Mkutano wetu na hatimaye tumalize na kuagana kwa upendo na furaha.
Asanteni sana kwa kunisikiliza
Imetolewa na:
Frank K. Tarimo
Mwenyekiti wa Halmashauri (W)
SIHA