Siha yapongezwa kwa kupata Hati Safi
Halmashauri ya Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro imepongezwa
kwa kupata hati safi kutokana na ripoti ya mkaguzi na mthibiti Mkuu wa hesabu za Serikali
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Said
Meck Sadiki wakati alipohudhuria kikao maalumu cha Baraza la Madiwani la
Halmashauri ya Wilaya ya Siha kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa
Halmashauri hiyo katikati ya Juma.
Mkutano huo maalum uliitishwa kwa agenda moja ya kupitia
ripoti ya Mkaguzi na mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha
2014/2015.
Katika Mkutano huo maalum wa Baraza la Madiwani, mkuu huyo wa
Mkoa wa Kilimanjaro aliwapongeza Baraza la Madiwani la kipindi kilichopita kwa
usimamizi mzuri wa shughuli za Serikali hasa rasilimali fedha
Alieleza kuwa hati safi inapatikana baada ya kila mtu
kutimiza wajibu wake, na hivyo aliwataka Madiwani wa Halmashauri ya Siha kama wasimamizi wakuu wa shughuli za maendeleo
wahakikishe wanasimamia kwa ukaribu fedha zote zinazotumwa na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ndugu zangu kama halmashauri itashindwa kukusanya mapato ya
kutosha kitakachoendelea ni kushindwa
kujiendesha na ninyi kama
Madiwani mtakuwa mmeshindwa kutimiza
wajibu wenu na mnaweza kusababisha Halmashauri yenu kufutwa kama lilivyo
agizo la Serikali ”alisema Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro
“Mimi pamoja na Mkuu wenu wa Wilaya ya Siha kama wasimamizi
wa Halmashauri tutaendelea kuhakikisha kuwa malengo ya Serikali yanatekelezwa
katika viwango vinavyostahili hasa usimamizi wa miradi ya maendeleo ikiwemo
barabara,miundombinu ya maji ,Elimu na shughuli nyingine zote” alibainisha Meck
Sadiki
Awali akiwasilisha ripoti hiyo ya Mkaguzi na Mthibiti mkuu wa
Hesabu za Serikali, Mkuu wa Idara ya
Fedha na Biashara kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Peter Temba aliliambia Baraza kuwa, Halmashauri ya Siha ni miongoni mwa
Halmashauri 49 hapa Nchini na miongoni mwa Halmashauri mbili pekee katika Mkoa
wa Kilimanjaro zilizopata hati safi kwa
mwaka 2014/2015
Alieleza kuwa hii,imetokana na ushirikiano mzuri uliokuwepo
kati ya wasimamizi wa Halmashauri yaani baraza la Madiwani na Wataalam wa
Halmashauri pamoja na Wananchi na Wadau
mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya wilaya hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Siha imekuwa ikifanya vizuri katika
usimamizi wa fedha za maendeleo na kufanya halmashauri hiyo kupata hati safi
kwa zaidi ya miaka saba mfululizo tangu ilipoanzishwa rasmi mwaka 2007
No comments:
Post a Comment