Sunday 19 June 2016

ASANTE AFRICA YACHANGIA MADAWATI 48 WILAYANI SIHA







Katika kuunga mkono jitihada za serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania za kupambana na uhaba wa madawati katika shule za msingi na Sekondari Wilayani siha
Shirika lisilo la Kiserikali asanteAfrica kutoka nchini Marekani na lenye makao makuu mjini Arusha Tanzania kwa ukanda huu wa afrika Mashariki  limechangia jumla ya madawati 48 Wilayani Siha yenye thamani ya fedha za Kitanzania shilingi  3.6 milioni.
Akikabidhi msaada huo kwa Halmashauri ya Siha mwakilishi wa shirika hilo ndugu Tesha alisema kuwa shirika lake limeamua kuchangia katika madawati ili kunusuru matatizo wanayopata wanafunzi mashuleni ya kukaa kwa msongamano madarasani.
Alieleza kuwa wakati taifa linapambana na kuondoa uhaba wa madawati mashuleni,shirika la asante Africa limeona ni vema kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano chini ya rais wa Tanzania  Mheshimiwa  John Joseph Pombe Magufuli.

Alisema kuwa shirika lake limeona kwa wakati huu ni vema kushirikiana na Serikali katika kuboresha suala la elimu kwa kutambua kuwa taifa ili lipate maendeleo ya kweli watu wake wanatakiwa kupata elimu bora na siyo bora elimu,alisema Tesha
Akipokea msaada huo mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Siha Rashid Kitambulio  alishukuru shirika hilo kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano katika kuboresha suala la elimu kwa watoto wa kitanzania.
Alieleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya  Siha itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo  kutoka ndani na nje ya nchi ili kuwaletea wananchi wa Siha maendeleo yanayotakiwa katika Nyanja mbalimbali ikiwemo suala la elimu
Mkurugenzi wa Siha alieleza kuwa hadi sasa Halmashauri yake imebakiza kiasi cha madawati 1744 tu ili kuondoa tatizo hilo katika shule zote za msingi na sekondari Wilayani humo.
Kitambulio aliwataka wadau wengine wa maendeleo wilayani Siha kuiga mfano wa shirika la AsanteAfrika katika kuchangia madawati na miundombinu mingine katika shule za msingi na Sekondari ili kuboresha kiwango cha elimu katika Wilaya ya Siha.
Alielza kuwa Wilaya ya Siha kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2012 hadi 2015 kiwango cha elimu kimekuwa kikiendelea kupanda kwa mjongea chanya hasa katika shule za msingi nakuifanya Halmashauri ya Siha kushika nafasi ya tatu kwa Mkoa wa Kilimanjaro.
Halmashauri ya Wilaya ya Siha inajumla ya shule za  Msingi  za Serikali 54 na 13 za Sekondari ambazo nyingi zinahitaji kuboreshwa zaidi katika miundombinu yake ili kuendana na wakati na maendeleo ya Sayansi na Tekinolojia.

No comments:

Post a Comment