Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya
Siha Mkoa wa Kilimanjaro Upendo Mangali amewaagiza Watendaji wa Vijiji vyote 60
katika Halmashauri ya Wilaya ya Siha kubuni vyanzo vipya vya mapato na
kusimamia vema ukusanyaji wa mapato katika maeneo ya Vijiji husika.
Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 22.9.2022 katika
ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha alipokuwa na kikao kazi na
watendaji wote wa Vijiji 60 vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Siha
ambapo amewataka kusimamia kwa ukaribu ukusanyaji wa mapato ya ndani ya
Halmashauri katika vyanzo vilivyomo maeneo yao
"Napenda kuwakumbusha watumishi wenzangu
kuwa ninyi ndio wakurugenzi katika vijiji vyenu na ndio maofisa masuhuli katika
maeneo yenu ya Vijiji hivyo ni budi mhakikishe kuwa mnakusanya mapato ya
Halmashauri kwa ukamilifu ili yasaidie shughuli za maendeleo na
uboreshaji wa utoaji wa huduma katika Halmashauri yetu" alisema Mangali
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Siha.
Lengo la kikao kazi kilichoandaliwa na
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Siha kwa Watendaji wa Vijiji
ni pamoja na kuwakumbusha wajibu mbalimbali pamoja na kupatiwa mafunzo
Watendaji wa Vijiji kuhusu mfumo wa ulipaji wa fedha za Serikali kwa ngazi ya
Vijiji