Friday 15 July 2016

HALMASHAURI YA SIHA YAENDELEA KUPATA HATI SAFI





Siha yapongezwa kwa kupata Hati Safi
Halmashauri ya Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro imepongezwa kwa kupata hati safi kutokana na ripoti ya mkaguzi  na mthibiti Mkuu  wa hesabu za Serikali

Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Said Meck Sadiki wakati alipohudhuria kikao maalumu cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Siha kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo katikati ya Juma. 

Mkutano huo maalum uliitishwa kwa agenda moja ya kupitia ripoti ya Mkaguzi na mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha 2014/2015.

Katika Mkutano huo maalum wa Baraza la Madiwani, mkuu huyo wa Mkoa wa Kilimanjaro aliwapongeza Baraza la Madiwani la kipindi kilichopita kwa usimamizi mzuri wa shughuli za Serikali hasa rasilimali fedha

Alieleza kuwa hati safi inapatikana baada ya kila mtu kutimiza wajibu wake, na hivyo aliwataka Madiwani wa Halmashauri ya Siha  kama wasimamizi wakuu wa shughuli za maendeleo wahakikishe wanasimamia kwa ukaribu fedha zote zinazotumwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Ndugu zangu kama halmashauri itashindwa kukusanya mapato ya kutosha kitakachoendelea ni kushindwa  kujiendesha na  ninyi kama Madiwani mtakuwa mmeshindwa kutimiza  wajibu wenu na mnaweza kusababisha Halmashauri yenu kufutwa kama lilivyo agizo la Serikali ”alisema Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro
“Mimi pamoja na Mkuu wenu wa Wilaya ya Siha kama wasimamizi wa Halmashauri tutaendelea kuhakikisha kuwa malengo ya Serikali yanatekelezwa katika viwango vinavyostahili hasa usimamizi wa miradi ya maendeleo ikiwemo barabara,miundombinu ya maji ,Elimu na shughuli nyingine zote” alibainisha Meck Sadiki

Awali akiwasilisha ripoti hiyo ya Mkaguzi na Mthibiti mkuu wa Hesabu  za Serikali, Mkuu wa Idara ya Fedha na Biashara kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo  Peter Temba aliliambia Baraza  kuwa, Halmashauri ya Siha ni miongoni mwa Halmashauri 49 hapa Nchini na miongoni mwa Halmashauri mbili pekee katika Mkoa wa Kilimanjaro  zilizopata hati safi kwa mwaka 2014/2015

Alieleza kuwa hii,imetokana na ushirikiano mzuri uliokuwepo kati ya wasimamizi wa Halmashauri yaani baraza la Madiwani na Wataalam wa Halmashauri pamoja  na Wananchi na Wadau mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya wilaya hiyo.

Halmashauri ya Wilaya ya Siha imekuwa ikifanya vizuri katika usimamizi wa fedha za maendeleo na kufanya halmashauri hiyo kupata hati safi kwa zaidi ya miaka saba mfululizo tangu ilipoanzishwa rasmi mwaka 2007

No comments:

Post a Comment