Friday 2 November 2018

SERIKALI KUMALIZA KERO YA MAJI MUNGE


Serikali kuwapatia Maji Wananchi wa  Munge

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa fedha  zaidi ya shilingi  milioni 638 (638,000,000/-) kwa ajili ya kuondoa kero ya maji kwa wananchi wa kijiji cha Munge kata ya Donyomuruak Wilayani Siha.

Hayo yamesemwa leo tarehe 01/11/2018 na mkuu wa Wilaya ya Siha mhe. Onesmo  Buswelu  alipokuwa akimtambulisha kwa wananchi wa kijiji cha Munge  mkandarasi  atakayefanya kazi hiyo  kuanzia mwezi Novemba 2018 hadi Augusti 2019.
 Mkuu wa Wilaya ya Siha mhe. Onesmo Buswelu (katikati) akikagua miundombinu ya maji kijiji cha Munge
 Wananchi wa kijiji cha Munge wakimsiliza mkandarasi aliyepewa kazi na Serikali ya kupeleka  na kujenga mradi mkubwa wa maji  wenye thamani ya shilingi milioni 638
Matarajio ya mradi kukamilika ni mwezi Agosti,2019

Mkuu wa Wilaya ya Siha aliwaeleza wananchi kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi shupavu wa mhe. Rais John Pombe Magufuli imedhamiria kuondoa kero zote zinazoikabili jamii ikiwemo kero ya maji.

Hata hivyo mkuu wa Wilaya ya Siha alitoa wito kwa wananchi wa kijiji cha Munge na wale wa vijiji jirani kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa mkandarasi aliyepewa kazi hiyo ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuwaletea maendeleo.

Awali akimkaribisha mkuu wa Wilaya ya Siha mhandisi wa maji Halmashauri ya Wilaya ya Siha Joyce Bahati kwa niaba ya mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha alieleza kuwa, mradi utakapokamilika utawanufaisha kaya zaidi ya 200 katika kijiji cha Munge kwa kuwapatia maji safi na salama.

Mhandisi huyo Alieleza kuwa,  mradi huo unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 10 kuanzia mwezi Novemba,2018, na jumla ya vilula 6 (vituo vya maji) vitajengwa katika maeneo mbalimbali ya kijiji cha Munge ili kusogeza  huduma ya maji karibu na wananchi.

Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa Halmashauri zilizopata mafanikio makubwa katikaaidi sekta ya maji ambapo hadi mwezi Oktoba 2018,usambazaji na upatikanaji wa maji umefikia zaidi asilimia 85.


No comments:

Post a Comment