Vikundi
22 Wanawake vyapatiwa mikopo 2016/2017
Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoa wa
Kilimanjaro imefanikiwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi 22 vya
wanawake Wilayani Siha katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha
Valerian Juwal alieleza hayo katika mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani uliofanyika
hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha.
Taarifa ya Mkurugenzi mtendaji ilieleza
kuwa,katika mwaka wa fedha 2016/2017 halmashauri ya Wilaya ya Siha imetoa
mikopo kwa vikundi 22 vya wanawake Wilayani
Siha yenye thamani ya shilingi 56 ,000,000/=
zikiwa ni fedha kutoka mchango wa Halmashauri wa asilimia tano (5%) ya mapato yake
ya ndani.
Aidha, Mkurugenzi katika taarifa yake
alieleza Baraza kuwa pamoja na changamoto ya halmashauri kukabiliwa na vyanzo
vichache vya ukusanyaji wa mapato lakini Halmashauri imejitahidi kutoa kiasi
hicho cha fedha kwa vikundi vilivyoomba mikopo na vilivyotimiza vigezo vya
kupata mikopo hiyo kwa kuzingatia sheria na taratibu mbalimbali.
Ametoa wito kwa vikundi vya wanawake katika
wilaya ya Siha kutumia fursa hiyo ya Serikali ya kuomba mikopo yenye masharti nafuu katika kujikwamua kiuchumi katika ngazi ya
Familia na jamii kwa ujumla wake.
Hata hivyo,Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Siha ametoa wito kwa vikundi mbalimbali vilivyopatiwa mikopo kutumia mikopo
hiyo kwa shughuli waliojipangia badala
ya kutumia mikopo waliyopewa katika
mambo yasiyoleta tija.
Alieleza kuwa pamoja na jitihada za
halmashauri kutoa mikopo hiyo kwa wanawake lakini wahusika bado wanayo wajibu mkubwa wa
kuhakikisha kuwa mikopo hiyo inarejeshwa kwa wakati ili iweze kuwasaidia
wanufaika wengine katika halmashauri ya Wilaya ya Siha.
Halmashauri ya Wilaya ya Siha katika
upangaji wa mipango na bajeti kila mwaka inatenga asilimia 5 ya mapato ya ndani
kwa ajili ya mikopo ya kuwawezesha wanawake na asilimia 5 ya mapato ya ndani ya
Halmashauri mikopo kwa vikundi vya
vijana.
Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri
ilitenga bajeti ya Tsh 87,051,850 kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya wanawake.
Ambapo hadi kufikia Juni 2017 jumla ya vikundi ishirini na mbili (22) vya
wanawake vilipatiwa mkopo wenye thamani ya Tshs 56,000,000/= zikiwa ni fedha
kutoka mchango wa Halmashauri wa asilimia tano (5%) ya mapato ya ndani.
No comments:
Post a Comment