Wednesday 25 October 2017

Siha yafanikiwa zoezi la utoaji wa chanjo mwaka 2016/2017




Utoaji wa Chanjo Wafanikiwa  Wilaya ya Siha mwaka 2016/2017
Halmashauri ya Wilaya ya Siha Mkoa wa Kilimanjaro imefikia zaidi ya asimia 96 ya huduma  ya utoaji wa chanjo mbalimbali ya kujikinga na magonjwa kwa watoto Wilayani hapa.

Katika taarifa ya mwaka 2016/2017 iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji  wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha  Valerian Juwal katika mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani lililokutana mwezi Oktoba katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Siha.

Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji ilieleza kuwa katika huduma ya utoaji wa chanjo mbalimbali kwa watoto, halmashauri ya Wilaya ya Siha imefanikiwa kutoa chanjo ya matone ya vitamin A na dawa za minyoo hadi kufikia asilimia 96.7

Aidha taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji ilieleza kuwa,katika huduma ya utoaji wa chanjo ya kansa ya shingo ya kizazi kwa watoto wa kike wenye umri  chini ya miaka 14,zoezi hilo pia  lilifanikiwa kwa  zaidi ya asilimia 87.

Mkurugenzi Mtendaji alieleza  Baraza la Madiwani kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Siha ni  miongoni mwa Halmashauri za Wilaya hapa nchini zilizofanya vizuri katika usimamiaji wa zoezi zima la utoaji chanjo kwa watoto.

Alieleza kuwa siri ya mafanikio  ya zoezi hilo ni ushirikiana wa dhati  baina ya Wananchi ,viongozi na wadau wengine wa maendeleo katika Wilaya ya Siha.

Hata hivyo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Siha aliwaomba wananchi na viongozi wa Siha kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuboresha afya ya wananchi wake hasa utoaji wa chanjo unaosaidia kutoa kinga mbalimbali kwa watoto.

Vile vile,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha alieleza Baraza la Madiwani kuwa huduma ya chanjo zote alizozitaja hutolewa bure kwa kugharamiwa na Serikali na hivyo kuwataka wananchi kutoa taarifa mara moja iwapo watatokea watu wanaowadai fedha za kulipia huduma hiyo.


Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012 Halmashauri ya Wilaya ya Siha inajumla ya watu 116,313 wakiwemo wanaume 56,500 na wanawake 59,813.


No comments:

Post a Comment