Thursday 10 August 2017

Siha kutumia tekinolojia kuendeleza kilimo na ufugaji Bora




Halmashauri ya Wilaya ya Siha kueneza tekinolojia mpya  ya kilimo  na ufugaji bora katika ngazi ya Halmashauri , Kata na  hatimaye katika vijiji vyote. 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha Valerian Juwal alipokuwa katika kilele cha maonesho ya nanenane yaliyofanyika kikanda katika viwanja vya Njiro Arusha ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Siha ilipata fursa ya kuonesha tekinolojia mbalimbali ya kilimo na mifugo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha alisema kuwa Halmashauri ya Siha itahakikisha kuwa mashamba Darasa yaliyopo kila kata yanaendelezwa ili kuwanufaisha wananchi wa maeneo husika na vijiji jirani.

Alieleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Siha itawatumia wataalam wa kilimo na mifugo waliopo katika ngazi ya Halmashauri ,Kata na Vijiji kuhakikisha wakulima wanapatiwa utaalam na ushauri wa kilimo na ufugaji wa kisasa ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na ufugaji.

Juwal aliwataka wananchi kuondokana na kilimo  na ufugaji wa kitamaduni na badala yake wabadilike na kuanza kulima na kufuga kwa kufuata tekinolojia mpya ambazo zitawasaidia kuongeza kipato na kuondokana na kuwa na vipato duni.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Siha ametoa wito kwa viongozi mbalimbali Wilayani Siha kuendelea kuwahamasisha wananchi kuzingatia ushauri wanaopewa na wataalam wa kilimo na mifugo waliopo katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo pia.

Zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Wilaya ya Siha wanategemea kilimo na ufugaji kama shughuli kubwa za kiuchumi kwa wananchi hao.mazao yanayolimwa kwa wingi zaidi ni Mahindi,maharage,viazi,ndizi,ngano,shairi na mazao ya mbogamboga.


No comments:

Post a Comment