Monday 19 June 2017

Sanya Hoyee wapongezwa kwa ujenzi wa Shule



Wananchi wa Kijiji cha Sanya hoyee Kata ya Sanya Juu  wapongezwa kwa ujenzi  wa madarasa mawili ya shule mpya ya msingi katika kijiji cha Sanya Hoyee.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Onesmo Buswelu alipofika eneo linapojengwa shule hiyo leo tarehe 19 Juni,2017 na kukagua shughuli za ujenzi zinazoendelea.

Mkuu wa Wilaya ya Siha aliwapongeza viongozi wa Kata na Vijiji kwa kazi nzuri aliyoiona hasa ujenzi wa madarasa na matundu ya choo cha wanafunzi,aliwataka wananchi na Wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kuunga mkono juhudi za Jamii katika kujiletea maendeleo.

Katika ujenzi huo hadi Juni,2017 wananchi wameshachangia zaidi ya shilingi milioni 5 ambazo zimetumika katika shughuli mbalimbali za ujenzi huo.

Hata hivyo mkuu huyo wa Wilaya ya Siha ametoa shilingi laki mbili kama mchango wake wa kuunga mkono juhudi za wananchi  za kujiletea maendeleo.

Hadi sasa ujenzi umefikia katika hatua ya umaliziaji wa kuweka rangi,kuweka vioo pamoja na umaliziaji wa vyoo vya wanafunzi ikiwa ni  pamoja na ujenzi wa choo wa walimu.

Kukamilika kwa shule hiyo kutasaidia kupunguza msongamano wa Wanafunzi katika shule za msingi Meral,Sanya Juu na Kilingi. Shule hiyo mpya ya msingi inatarajiwa kuanza rasmi mwezi januari mwaka 2018.

No comments:

Post a Comment